Wanga
Wanga ni dutu ogania inayojengwa ndani ya seli za mimea.
Kwa matumizi ya kibinadamu ni sehemu muhimu ya chakula katika vyakula kama ugali, ndizi, viazi, pasta na mkate.
Kikemia wanga ni kabohidrati aina ya polisakaridi yenye fomula (C6H10O5)n. Inajengwa kwa molekuli ndogo zaidi za glukosi.
Mimea hujenga molekyuli za wanga kama njia ya kutunza akiba ya nishati. Inaonekana kwa hadubini kama punje ndogo ndani ya seli.
Nje ya matumizi kama chakula wanga imetumiwa pia tangu karne nyingi kama gundi. Ikipashwa moto inapokea maji mengi na muundo wake wa punje-punje hupasuka. Baada ya kukauka huwa imara. Kwa njia hiyo ni muhimu katika utengenezaji wa karatasi hasa.