Karatasi
Karatasi (kutoka Kigiriki Χαρτί kharti kupitia Kiarabu قرطاص qartas) ni laha bapa na nyembamba ya konge za mimea zilizokandamizwa na kushikamanishwa. Watu huandika kwenye karatasi, vitabu na magazeti hufanywa kwa karatasi, tena vipande vikubwa vya karatasi hutumika kwa kufunga vitu ndani yake.
Karatasi hunywa kiowevu, hivyo hutumiwa pia kwa shughuli za kusafisha.
Karatasi hutengenezwa hasa kutokana na ubao uliosagwa lakini inawezekana kutumia konge za mimea mingine pia. Inawezekana kutumia pia karatasi iliyokwishatumiwa (kwa mfano magazeti ya kale) kwa kutengezea karatasi mpya.
Kwa matumizi mengine kuna pia karatasi nene kama bapa inayotumiwa kutengezea maboksi ya kubebea vifaa.
Watu wa kwanza kutengeneza karatasi walikuwa Wachina.
Karatasi ya wadudu
haririAina ya karatasi asilia hutengenezwa na nyigu na wadudu wengine kwa kujenga mzinga wao. Zinatafuta ubao ulioanza kuoza na kuitafuna halafu kuijenga kwa kuchanganya na mate. Inakauka kuwa kuta za mzinga na sega.
Kutengeneza karatasi
haririUbao husagwa halafu kuchanganywa na maji kuwa aina ya uji. Karatasi ya kuandikia huongezwa madawa ya kuondolea rangi yote ili karatasi itokee nyeupenyeupe. Uji huo unatandikwa na kusukumwa kuwa laha bapa inayofaa kwa ukurasa. Baadaye hukatwa vipande-vipande jinsi vinavyotakiwa.
Karatasi kwa matumizi kwenye mashine kubwa za kuchapa hutengenezwa mfululizo kwa umbo la kanda ndefu linaloviringishwa kuwa vikuto vikubwa. Mashine za kutengeneza karatasi hukausha uji wa konge njiani kwa kuipasha joto.
Madawa mbalimbali huongezwa kwenye uji wa karatasi kuipa sifa zinavyotakiwa kama uso wa kung'aa au rangi mbalimbali.
Karatasi za kusafishia (kwa mfano karatasi ya chooni) zinatakiwa kuwa laini sana.
Fomati za karatasi
haririKwa kawaida karatasi zinakatwa kwa wateja kufuatana na fomati zinazokubaliwa kimataifa katika vipimo vya ISO 216.
Fomati mashuhuri za ISO 216 ni kama vile A4 (karatasi ya kawaida ya mm 148 x 297), A5 (nusu ya A4) au A1 kwa matangazo makubwa.
Matumizi ya karatasi
haririKaratasi hutumiwa kwa madhumuni mengi:
- Karatasi ya kuandikia hutumiwa kwa madaftari na laha zinazouzwa kwa rimu
- Karatasi ya kuchapisha vitabu na magazeti hutengenezwa kwa vikuto
- Karatasi ya kusafishia hutengenezwa pia kwa vikuto
- Karatasi za noti inatakiwa kudumu muda mrefu, hivyo inaungwa pia na nyuzi za metali zinazotakiwa kufanya iwe vigumu kutengeneza pesa bandia
- Karatasi nene kiasi yenye rangi na bombwe hutumiwa kama mapambo ya nyumba ikipakwa kwenye kuta za nyumba
- Karatasi ni muhimu kwa kufunga bidhaa katika masanduku ya karatasi nene
- Katika utamaduni wa Asia kuta za vyumba mara nyingi ni karatasi tu
Historia
haririWatangulizi wa karatasi
haririHata kabla ya kupatikana kwa karatasi yenyewe, mataifa mbalimbali walitengeneza laha kwa maandiko yao.
Katika Misri ya Kale papiri ilitumiwa kwa miaka elfu kadhaa. Ilitengenezwa kwa kutumia kiini laini cha tete fulani (Cyperus papyrus).
Watu wa Meksiko ya Kale walitengeneza laha za amatl. Hapa walitumia ganda laini ya ndani ya mti aina ya mbuyu lililochemshwa na kupigwa hadi kuwa laha.
Karatasi kutoka China
haririKaratasi yenyewe ilibuniwa nchini China. Waziri Tsai-Lun alieleza mnamo mwaka 105 mbinu ya kutengeneza karatasi katika kitabu chake. Mabaki ya hariri yalichanganywa na nguo zilizochakaa na utembo wa miti. Yote yalipondwa na kusagwa halafu kupikwa katika maji na kusafishwa. Nyuzi tupu zilizobaki zilichotwa kwa chujio halafu zikasilibiwa ndani ya chujio na kukandamizwa na kukaushwa.
Kimsingi kazi ya kutengeneza karatasi ndivyo ilivyo hadi leo.
Mataifa jirani walipokea ujuzi kuhusu karatasi kutoka kwa Wachina. Mnamo 750 wafungwa Wachina waliwafundisha Waarabu mtindo huu na kitabu cha kwanza kilichoandikwa juu ya karatasi kilipatikana Baghdad mnamo 870.
Wazungu walipokea ujuzi huu kutoka kwa Waarabu ama waliotawala sehemu za Hispania ama sehemu nyingine.
Kiwanda cha kwanza cha Ulaya kilianzishwa Fabriano (Italia) kabla ya mwaka 1264.
Tangu Johannes Gutenberg abuni mashine ya kuchapa vitabu, mahitaji ya karatasi yaliongezeka sana duniani.
Leo hii njia nyingine za kutunza kumbukumbu kama vile tarakilishi na mtandao zimeanza kupunguza umuhimu wa karatasi kama media ya habari.