Wikipedia:Makala ya wiki/Ugonjwa wa kuambukiza

Bakteria ya "streptococcus pneumoniae" ni pathojeni inayosababisha kifua kikuu.

Ugonjwa wa kuambukiza (kwa Kiingereza infectious disease) ni ugonjwa wowote unaosababishwa na ambukizo, yaani kuingia na kuenea kwa pathojeni kama bakteria, virusi au fungi katika mwili. Wanadamu, wanyama na pia mimea wanaweza kuambukizwa na pathojeni hizi. Baadhi ya magonjwa hayo yanaweza kupitishwa na mgonjwa mmoja kwenda kiumbehai mwingine. Njia za kuambukizwa (yaani njia ya kufika kwa pathojeni mwilini) ni nyingi, zikiwa pamoja na kugusana, maji, chakula, damu au hata hewani. Pathojeni ni jina kwa bakteria, virusi au fungi zinazoweza kusababisha ugonjwa. Si kila bakteria au fungi inasababisha ugonjwa, kinyume chake tunaishi kwa kuwa na mamilioni ya bakteria katika utumbo ambazo ni lazima kuwepo kwa afya yetu. Vidubini hivi vyote ni vidogo mno, havionekani kwa macho. Magonjwa ya kuambukizwa huwa na dalili tofauti sana. Mara nyingi dalili za ugonjwa hutegemeana na pathojeni iliyosababisha ugonjwa. Dalili zinaweza kuonekana siku chache baada ya kuambukizwa au kuendelea polepole katika kipindi cha wiki, miezi hata miaka. Kwa kawaida mgonjwa anapona mwenyewe na mfumo wa kinga mwilini unajifunza kupambana na pathojeni husika. Kama inarudi mwili unaijua tayari, hivyo si kawaida mtu kugonjeka mara mbili na ambukizo lilelile. Kama mfumo wa kinga ni dhaifu ugonjwa huwa ni hatari hadi kusababisha kifo. ►Soma zaidi