Ramogi Achieng Oneko (1920 - 9 Juni 2007) alikuwa mpigania uhuru na mwanasiasa katika nchi ya Kenya, alipokuwa anachukuliwa kama shujaa wa kitaifa.

Jomo Kenyatta, Apa Pant and Achieng Oneko

Alizaliwa katika kijiji cha Tieng'a katika eneo ndogo la Uyoma katika Wilaya ya Bondo mnamo mwaka wa 1920.

Kuzuiliwa Kwake

hariri

Oneko alikuwa mmoja wa wapigania uhuru sita ambao walikamatwa na serikali ya kikoloni ya Uingereza wilayani Kapenguria mwaka wa 1952. Wanachama wengine wa kikundi hicho waliokuwa wanajulikana kama "Kapenguria six" walikuwa Jomo Kenyatta, Paul Ngei, Bildadi Kaggia,Kungu Karumba na Fred Kubai. Sita hao walikamatwa kwa madai ya kuhusishwa na harakati ya Uasi ya Mau Mau[1] wakaachiliwa miaka tisa baadaye, mnamo mwaka wa 1961, miaka miwili kabla ya Kenya kupata uhuru.

Uchaguzi wa ubunge wa kwanza ulifanyika mnamo siku ya uhuru mwaka wa 1963 na Achieng Oneko alishinda kiti cha eneo bunge la Mji wa Nakuru. Jomo Kenyatta akawa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya na kwa haraka akamteuwa Achieng Oneko kama Waziri wa Habari, Utangazaji na Utalii. Hata hivyo, mwaka wa 1966 Oneko alijiondoa serikalini na kujiunga na chama kipya cha Kenya People's Union, chama cha kijamii kilichokuwa kinaongozwa na sahibu wake Oginga Odinga

Mnamo mwaka wa 1969 Oneko alikamatwa na rafiki yake wa zamani, Kenyatta, kufuatia machafuko huko Kisumu wakati wa ziara yake (Kenyatta) katika mji huo. Oneko aliachiliwa mwaka wa 1975.

Oneko alirejea siasani mwaka wa 1992 wakati alichaguliwa kama mbunge katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Kenya. Alikiwakilisha chama cha,Ford-Kenya kilichokuwa kikiongozwa na Oginga Odinga. Hata hivyo, alipoteza kiti chake cha eneo bunge la Rarieda katika uchaguzi ujao mwaka wa 1997.

Oneko aliipa dunia mkono wa buriani baada ya kuathiriwa na mshambulio wa moyo akiwa na umri wa miaka 87 mnamo 9 Juni 2007 nyumbani kwake katika kijiji cha Kunya, Rarieda, Wilaya ya Bondo.

Oneko aliacha mjane Loice Anyango. Mkewe mkubwa, Jedida, alifariki mwaka wa 1992. Oneko aliacha watoto 11, wanaume saba na binti wanne. Mwana wake mkongwe ni Dk Ongonga Achieng.

Wakati wa kifo chake, Oneko alikuwa mwanachama pekee wa "Kapenguria six" ambaye alikuwa bado hai. Siku ya Kenyatta, likizo ya kitaifa nchini Kenya, hufanyika ili kuenzi sita hao waliowekwa kizuizini mnamo 20 Oktoba 1952

Marejeo

hariri
  1. The Standard: 16 Juni 2007: Fare thee well Achieng’ Oneko