Vigeuzamawe (pia geuzamawe) ni ndege wa jenasi Arenaria katika familia Scolopacidae. Wanafanana na chamchanga lakini ni wanene zaidi. Rangi yao ni kahawia na nyeusi mgongoni, nyeupe chini na nyeusi kidarini. Kigeuzamawe mweusi ana nyeusi zaidi mgongoni kuliko kigeuzamawe kahawia, na yule wa pili ana kichwa cheupe takriban kabisa. Spishi mbili zote huzaa katika kande za kaskazini za dunia na huhamia kusini nje ya majira ya kuzaa. Hula wadudu hasa wakati wa majira ya kuzaa; chakula kingine ni gegereka, konokono, nyungunyungu, mayai, mizoga na vipande vya mimea na miani. Hugeuza mawe na vitu vingine ili kutafuta mawindo (asili ya jina lao). Jike huyataga mayai 2-5 ardhini katikati ya mafunjo au manyasi karibu na maji.
Spishi ya Afrika (na Ulaya)
hariri