Bahari ya Karibi ni bahari ya pembeni ya Atlantiki iliyoko kusini ya Ghuba ya Meksiko. Upande wa magharibi imepakana na Amerika ya Kati, kusini na Amerika ya Kusini. Pinde la Visiwa vya Karibi linaitenga na Atlantiki yenyewe.

Ramani ya Amerika ya Kati na Bahari ya Karibi

Bahari ya Karibi ina eneo la 2,754,000 km². Inafunika sehemu kubwa ya bamba la Karibi. Kina kikubwa kipo katika mfereji wa Kayman kati ya visiwa vya Kuba na Jamaika mwenye urefu wa 7,686 m chini ya UB.

Kuna hori za bahari na ghuba mbalimbali kama ghuba ya Venezuela na ghuba ya Honduras.

Ekolojia

hariri

Bahari hii inajulikana kwa miamba yake ya tumbawe ambayo ni mazingira ya aina nyingi za mimea, samaki na kasa. Miamba ya tumbawe ni msingi wa uvuvi na zinavuta watalii wengi.

Katika miaka ya nyuma tumbawe ziko hatarini kutokana na kupanda kwa halijoto ya maji. Tayari sehemu za tumbawe zimekufa. Mapatano ya nchi za Karibi yanatafuta njia za kuhifadhi mazingira haya ya pekee.

Hali ya hewa

hariri

Kupanda kwa halijoto ya maji kumesababisha kuongezeka kwa dhoruba za tufani kali. Majira yake ni Juni na Desemba hasa wakati wa Agosti na Septemba. Kwa wastani kuna dhoruba kali 9 kila mwaka na 5 kati yao hufikia kiwango cha tufani. Dhoruba kali huanzia katika sehemu ya mashariki ya bahari ya Karibi kutokana na shindikizo duni la hewa. Dhoruba hizi huelekea mara nyingi upande wa magharibi-kaskazini lakini hugeuza kuelekea mashariki wakati wa kufikia maeneo yenye halijoto ya chini zaidi.

Tufani zinaleta uharibifu mwingi zikipita kwenye visiwa na makao ya watu lakini huharibu pia miamna ya tufani kutokana na kutupa kiasi kikubwa cha machanga na matope kwenye miamba hii.

Historia

hariri

Jina la Karibi limetokana na makabila ya Wakaribi wenyeji waliokalia visiwa nya Antili Ndogo (kati ya kisiwa cha Puerto Rico na pwani la Venezuela) wakati wa kufika kwa Kristoforo Kolumbus mnamo mwaka 1500. Visiwa vikubwa vilikaliwa na wenyeji Waarawaki Wenyeji hawa walipotea kabisa kutokana na magonjwa yaliyoletwa na Wazungu Wahispania na vita dhidi ya wakoloni hawa.

Wahispania hawakuona umuhimu sana kutawala visiwa vyote vidogo hivyo Wazungu wengine walifuata na kuvamia visiwa mbalimbali. Waingereza, Wafaransa, Waholanzi na Wadenmark walishika visiwa mbalimbali na kuvifanya koloni zao.

Hata hivyo maharamia walipata nafasi zao katika visiwa vidogovidogo wakishambilia hasa meli za Wahispania zilizobeba dhahabu na fedha kutoka migodi ya Meksiko na Peru. Kipindi hiki cha uharamia kilianza mnamo mwaka 1560 BK na kuendelea hadi 1720. Kati ya maharamia mashuhuri wa nyakati zile walikuwa Blackbeard ("ndevu mweusi"), Henry Morgan na William Kidd. Aina nyingine ya waharamia walikuwa watu kama Sir Francis Drake aliyetekeleza uharamia wake kwa niaba ya malkia ya Uingereza dhidi ya meli za Wahispania.

Mataifa ya Ulaya yalitumia visiwa vya Karibi kwa ajili ya kilimo hasa cha sukari. Mashamba makubwa yalilimwa kwa kutumia watumwa kutoka Afrika. Kutokana na historia hii visiwa vingi vina idadi kubwa ya watu wenye asili ya kiafrika kama kwa mfano kisiwa cha Hispaniola chenye nchi mbili za Haiti na Jamhuri ya Dominika.

Visiwa vingi vya Karibi vimepata uhuru katika karne ya 20. Athira ya Amerika ni kubwa siku hizi.

  Makala hii kuhusu maeneo ya Bahari ya Karibi bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Bahari ya Karibi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.