Bendera ya Tanzania
Bendera ya Tanzania ni ya mstatili unaokatwa pembe kwa pembe na kanda nyeusi yenye milia za njano kandokando[1].
Pembetatu ya juu ina rangi ya majani, pembetatu ya chini ni ya buluu.
Matumizi ya bendera inahifadhiwa chini ya sheria ya "The National Flag and Coat of Arms Act, 15-1971"[2].
Historia ya bendera
Bendera hii imepatikana tangu 30 Juni 1964 kutokana na muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Bendera ya Tanganyika ilikuwa na rangi ya kijani ikiwa na kanda nyeusi katikati yenye milia za njano kando. Buluu imepatikana kutokana na bendera ya Zanzibar ya mwaka 1964 ikimaanisha bahari. Hata hivyo toka mwaka 2005, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kutumia rasmi bendera ya Zanzibar. Hii ni mara ya kwanza toka kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar kwa funguvisiwa la Zanzibar kuwa na bendera yake lenyewe.
Maana ya rangi
Rangi zinasemekana kuwa na maana zifuatazo:
- Kijani kwa ajili ya mashamba, kilimo na misitu. Kijani ni pia rangi ya bendera ya chama cha TANU kilichokuwa chama tawala tangu uhuru.
- Buluu kwa ajili ya bahari na visiwa.
- Nyeusi ni rangi ya Waafrika.
- Njano inakumbusha juu ya utajiri wa madini. Njano ya namna hiyo inaelezwa mara nyingine kuwa ni dhahabu [3], lakini maelezo rasmi mengine kwa Kiingereza yanataja rangi kuwa "Yellow Pantone 116c"[4][5]
Bendera za kihistoria tangu zamani za ukoloni
Flag | Duration | Use | Description |
---|---|---|---|
1856–1963 | Bendera ya Usultani wa Zanzibar | Kitambaa chekundu | |
1888–1890 | Bendera ya Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki | Nyeupe, msalaba mweusi, nyota za Salibu | |
1893-1919 | Bendera ya Mamlaka ya Koloni za Ujerumani | Nyeusi-nyeupe – nyekundu kama Dola la Ujerumani, pamoja na ishara ya tai, ilitumiwa katika koloni zote za Ujerumani | |
1919–1961 | Ramani ya eneo la kudhaminiwa Tanganyika | Bendera nyekundu yenye rangi za Uingereza kwenye kona na ishara ya twiga | |
1961–1964 | Bendera ya Tanganyika | Kijani yenye kanda nyeusi katikati linaloshikwa na milia ya njano-dhahabu | |
1963–1964 | Bendera ya Usultani wa Zanzibar baada ya uhuru | Nyekundu, yenye duara ya kibichi inayoonyesha karafuu mbili za rangi ya njano | |
Januari–Aprili 1964 | Bendera ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hadi maungano | Kanda za buluu, nyeusi na kijani. |
Marejeo
- ↑ National Flag Ilihifadhiwa 27 Septemba 2018 kwenye Wayback Machine., tovuti rasmi ya serikali ya Tanzania, iliangaliwa Desemba 2018
- ↑ Act to prescribe the National Flag and Coat of arms.. Ilihifadhiwa 27 Oktoba 2021 kwenye Wayback Machine., tovuti ya serikali ya Tanzania, iliangaliwa Desemba 2020
- ↑ http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Serikali-yatoa-maelekezo-matumizi--rangi-ya-bendera/1597296-4893496-f15slnz/index.html
- ↑ National Flag, "colour specifications", tovuti rasmi ya serikali ya Tanzania
- ↑ http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Magufuli-afuta-maelekezo-mapya-matumizi-ya-bendera/1597296-4895796-15gjsv1z/index.html