Chiwale
Chiwale ni kata ya Wilaya ya Masasi katika Mkoa wa Mtwara, Tanzania.
Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2022, kata ilikuwa na wakazi wapatao 21,466 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 11,311 waishio humo.[2]
Historia ya kijiji
haririKijiji cha Chiwale ambacho kiko umbali wa kilometa 30, Kaskazini-Magharibi mwa mji wa Masasi, kilianza mnamo 1965 kikiwa kijiji cha asili, mwanzilishi wake akiwa Mwinyi Makolela. Kuanza kwake kulikuwa hivi:
Suedi Sandali, mtoto wa Alimu Tamanda au Mwinyi Makolela (wakati huo akiwa kijana), mwaka 1965, alikwenda kumtembelea rafiki yake Yona Sigalile wa eneo linaloitwa Lilala, kilometa chache tu toka kijiji cha Chiwale katika barabara kuu iendayo Masasi. Sasa hivi Lilala ni kijiji.
Baada ya mzee Sandali kufika Lilala, alimuomba huyo rafiki yake waende kuwinda katika msitu wa Chiwale kwa sababu yeye (rafiki), alikuwa na bunduki. Walipofika Chiwale, walimuua swala na kisha walimchukua hadi eneo ambapo baadaye ilijengwa ofisi ya kijiji cha Ujamaa Chiwale, wakapumzika hapo. Baada ya kuondoka mzee Sandali alirudi Mrashi alikokuwa akiishi.
Katika mwaka huohuo, mzee Alimu Tamanda (mwenye Makolela), alikuja toka Msumbiji eneo liitwalo Nankatali (Chapa), na kuuliza iwapo kuna mahali wanaweza kuishi ndani ya nchi ya Tanzania. Ndipo mzee Sandali akamjulisha kuwa iko sehemu moja jirani na Lilala inaitwa Chiwale.
Mzee Makolela akaomba waende kupaona, wakiwa yeye mzee Makolela, mzee Katambo, mzee Lali na kijana wao wakati huo kwa sasa mzee Swedi Sandali. Walifika na kupaona mahali hapo, ambapo palikuwa na kichuguu na jirani na ziwa (bwawa). "Eneo la bwawa hilo liko mpaka hivi sasa japokuwa kina chake kimetoweka." Hawakuruhusiwa kujenga isipokuwa kuweka uzio tu. Wakakaa hapo kwa siku mbili wakati wakiweka alama za mahali pa kujenga.
Ilipofika siku ya pili, vitabu vya Kur'an vya mzee Makolela vikaungua moto uliodaka kwenye ukuni uliotumika kuzimia moto. Moto huo ulikuwa umewashwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida katika makazi au kambi. Lakini hata hivyo usiku uliofuatia, mwenye Makolela alipokuwa usingizini akaota ndoto kuwa kilichofanyika yaani kuungua kwa vitabu ni utani tu wa watani wake Wamwera. Katika ndoto hiyo, akaelekezwa kuwa asubuhi atakapoamka aelekee upande wa machweo ya jua (Magharibi), akaweke alama. Huko ndiko atakakoishi. Sehemu hiyo ni ng'ambo ya ziwa ambako hadi sasa kuna mti unaoitwa Nsolo kwa lugha ya Kiyao. Huko ndiko yalikokuwa makao makuu ya mwinyi Makolela na baadaye kulijulikana kama Azimio au bwawani. Zoezi la kuweka alama za makazi likaendelea na siku ya tano shughuli yote ikawa imekamilika.
Safari ya kurudi Mrashi ikaanza.
Mwaka huohuo wa 1965, jitihada za kuhamia zilianza ndipo walipata gari la tajiri mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina la Govind toka mjini Masasi, na hivyo kuweza kuhamisha mizigo yao hadi sehemu iitwayo Nangose (Marokopaleni), kwa mwalimu Karlo, kwa sababu hapakuwepo na njia/barabara ya kupita gari. Kazi ya kuhamisha mizigo kwa kichwa ilikamilika ndani ya mwaka huohuo wa '65, na familia ikawa imehamia rasmi Chiwale.
Waliokuwepo katika msafara huo ni hawa wafuatao; 1. Mwinyi mzee Makolela 2. Bi. Aluna Maulana (mke mkubwa wa mwinyi Makolela) 3. Bi. Hadija Izulu (mke mdogo wa mwinyi Makolela). 4. Bw. Suedi Sandali 5. Bw. Thabiti Makolela 6. Bw. Bashiri Makolela 7. Bi. Fatuma Makolela 8. Bi. Rukia Makolela 9. Bi. Dunia Makolela 10. Bw. Waziri Makolela 11. Bw. Abdalla Makolela
Kutokana na hali ya vita vya kupigania uhuru wakati huo nchini Msumbiji kati ya Wareno (wavamizi),na FRELIMO (wazalendo); kulitokea tatizo dhidi ya serikali ya Tanzania. Walitakiwa wahame kutokana na kuhofiwa usalama wao. Jumbe Habilu Limbende akatumwa kuwahamisha. Lakini mwenye Makolela alikataa na kusema maneno haya yafuatayo, "MKITAKA MJE MNIUE HAPAHAPA NA FAMILIA YANGU, MIMI HAPA SIHAMI, KWANI PATAKUWA MJINI HATA NINYI WENYEJI MUTAHAMIA."
Ndipo jumbe Limbende akaondoka. Siku moja mwaka wa 1966, mzee Sandali alikwenda Nambaya (kijiji cha jirani na Chiwale), kutembea akakutana na mwalimu Barzolo Kambona ambaye ndiye alikuwa mwalimu wake wa shule ya msingi huko Mpeta Masasi. Nia ya safari ilikuwa ni kuonana na mwenye Chiwale. Hapo mzee Sandali akatumia fursa ya kuonana na mwalimu Barzolo kumuomba masomo ya kwanza/awali, chaki na mpira wa kuchezea wanafunzi ili aweze kuanzisha darasa la awali kama sehemu ya nyongeza ya masomo ya dini (Kur'an), ya Kiisilamu yaliyokuwa yakitolewa katika familia hiyo ya mwenye Makolela. Baada ya mwalimu Barzolo kumpatia vifaa hivyo aliweza kuanzisha darasa likiwa na watu wanane (8), miongoni mwao wasichana 5 na wavulana 3. Darasa hilo lilijengwa jirani na mwamba ulioko kando ya ziwa.
Hadi wakati huo, wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali walishaanza kuishi katika maeneo yaliyokuwa jirani na kambi hiyo ya Chiwale.
Miaka ya 1970, kijiji cha Chiwale kilianza rasmi. George Banali, wakati huo akiwa Katibu wa Tarafa ya Lisekese wilayani Masasi, ndiye aliyetoa mchango mkubwa katika kuanzishwa kwa Kijiji hicho. Hatimaye uongozi wa kijiji ukapatikana na mwenyekiti kuwa ni mzee Muhidini Elias na makamo wake ni mzee Nkhuterreni. Katibu ni mzee Mahmudu Hokororo.
Mnamo miaka 1970-1972, kazi za ujenzi wa ofisi ya kijiji, na barabara zikaanza rasmi. Sambamba na hayo uanzishwaji wa shule ya msingi na ujenzi wa ghala la kuhifadhia nafaka vikatiliwa mkazo. Kazi ya ujenzi wa shule na ghala zilifanyika na kukamilika kwa siku moja chini ya usimamizi wa balozi mkuu (kiongozi) wa nyumba kumi mzee Mfaume Hassani (marehemu) kwa jina maarufu mzee "Hinchuppi."
Mnamo mwaka 1973, serikali ilikipatia kijiji cha Chiwa le mwalimu wake kwa ajili ya kuanzisha masomo rasmi ya shule ya msingi. Mwalimu huyo aliyeitwa Edward Matayo Kazibure, alihamishiwa toka shule ya msingi Lukuledi. Hadi wakati huo, kijiji kijiji kilikuwa kinakua kwa kasi na kuanza kujipatia umaarufu miongoni mwa vijiji vingi. Hali hiyo hadi sasa inazidi kuongezeka kwani hivi sasa sura ya kijiji inaondoka na kuelekea katika kuwa mji mdogo.
Kijiji cha Chiwale kilipata usajili wa kudumu kama kijiji rasmi cha ujamaa kati ya miaka ya 1973-1975, hivi, wakati huo kilikuwa na wakazi takribani 200 wengi wao wakiwa ni wahamiaji kutoka katika vijiji vya kusini mwa Masasi na wengine Msumbiji. Viongozi wa kwanza wa kijiji wakiwa ni Edmundi Akili (Katibu wa kijiji), Muhidin Alias (Mwenyekiti), Mfaume Hassan Hinchuppi (Mkuu wa mabalozi wa nyumba kumi), pamoja na viongozi wengine. Mwaka 1973, ilianzishwa shule ya msingi ambapo mwalimu Edward George Kazibure alihamishiwa kutoka Lukuledi kwa madhumuni ya kuanzisha shule hiyo.
Kijiji cha Chiwale kilikuwa na mitaa mikuu mitatu, ambayo ni Ufukoni, Matatizo na Azimio. Sababu ya kuwepo kwa majina hayo ni kwamba, Azimio ambao ulikuwa upande wa Kaskazini Magharibi ya ng'ambo ya ziwa Chiwale. Huko ndiko wananchi walikokuwa wakikutana kwa ajili ya kujadili na kuweka maazimio mbalimbali ya shughuli za maendeleo ya kijiji; Ufukoni ni upande wa Kaskazini Mashariki, ambao baada ya kuweka maazimio hayo walivuka nayo na kwenda kuyakabidhi ng'ambo ya ziwa yaani Katani Lukuledi na wilayani Masasi. Majina ya mitaa hiyo sasa hivi hayafahamiki miongoni mwa wakazi wengi wa kijiji hicho cha Chiwale.
Mwaka 2010, kijiji cha Chiwale kilipandishwa hadhi na kuwa kata ikiwa na vijiji vinne, ambavyo ni Chiwale, Kivukoni, Lilala na Nanyindwa. Vilevile kijiji kina shula tatu za msingi: kati ya hizo, mbili zimeshasajiliwa na moja haijapata usajili. Pia, kuna kituo cha afya ambacho kilijengwa kati ya mwaka 1978 - 1983, ambacho kilishakamilika na kwa sasa kinatoa huduma mbalimbali za afya zikiwemo za upasuaji na kulaza wagonjwa mbalimbali. Jitihada za serikali kukiongezea uwezo kituo hicho zinaendelea na kuna matarajio kwamba katika miaka ya hivi karibuni Kituo hicho kitaongezewa uwezo na kuwa hospitali kamili.
Wengi wa wakazi wake ni wakulima na wafugaji wadogowadogo. Shughuli za ufugaji hazisitawi sana kutokana na kuwepo kwa mbung'o wengi kwa hiyo kusababisha uadimu wa ng'ombe. Mazao ya biashara na chakula ni mahindi, mtama, muhogo, korosho, ufuta, kunde na nafaka zinginezo.
Kwa sasa kijiji hiki ambacho kina kituo cha afya, shule ya sekondari, kimepiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi na kimaisha. Licha ya kijiji hicho kuwa miongoni mwa vijiji vilivyojengwa kwa mpangilio, lakini kina sifa ya kuwa na amani, utulivu na ardhi yenye rutuba isiyohitaji mbolea ya kisasa.
Wakazi wake ni wakarimu na wenye kujali na wenye kupenda kujifunza. Hali hiyo imekifanya kukua kwa kasi na kuashiria kuelekea katika kuwa mji mdogo. Fursa za uwekezaji ni kubwa mno katika shughuli za elimu, utafiti, utalii na biashara mbalimbali.
Marejeo
haririKata za Wilaya ya Masasi Vijijini - Tanzania | ||
---|---|---|
Chigugu | Chikoropola | Chikukwe | Chikundi | Chikunja | Chiungutwa | Chiwale | Chiwata | Lipumburu | Lukuledi | Lulindi | Lupaso | Makong'onda | Mbuyuni | Mchauru | Mijelejele | Mitesa | Mkululu | Mlingula | Mnavira | Mpanyani | Mpeta | Mpindimbi | Msikisi | Mwena | Namajani | Namalenga | Namatutwe | Namwanga | Nanganga | Nangoo | Nanjota | Ndanda | Sindano |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mtwara bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Chiwale kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |