Dhibu (kwa Kilatini na Kiingereza Lupus) [1] ni jina la kundinyota linaloonekana kwenye angakusi ya Dunia.

Nyota za kundinyota Dhibu (Lupus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Dhibu - Lupus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kusini

Mahali pake

Dhibu (Lupus) linapatikana angani kati ya nyota angavu za Antara (Antares) na Rijili Kantori (Rigil Kentaurus). Linapakana na makundinyota jirani ya Akarabu (Nge) (Scorpius), Pembemraba (Norma), Bikari (Circinus), Mizani (Libra) na Kantarusi (Centaurus).

Jina

Dhibu (Lupus) lilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu waliosema ذئب dhiʾb kwa maana ya mbwa mwitu wa Ulaya na Asia. [2]. Jina la kawaida kati ya Waarabu ni السبع as-sabuʿ kwa maana ya “mnyama mwitu wa pori” na hii ni namna jinsi gani walivyotafsiri Kigiriki Θηρίον therion cha Ptolemaio aliyetaja nyota hizi vile katika orodha yake ya Almagesti [3]. Ni wafasiri wa baadaye waliotafsiri mnyama huyu kama “mbwa mwitu” yaani Lupus kwa lugha ya Kilatini.

Lupus - Dhibu ni kati ya makundinyota 48 yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika kitabu cha Almagesti wakati wa karne ya 2 BK. Ipo pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [4] kwa jina la Lupus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Lup'.[5]

Nyota

Nyota angavu zaidi ni Alfa Lupi au Kakkab [6]. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 2.3 ikiwa na umbali unaokadiriwa kuwa na miaka nuru 460 kutoka Dunia[7][8].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
α Kakkab 2,30m 500 B1 III
β 2,68m 500 B2 IV
γ 2,80m 400 B2 IV
δ 3,22m 600 B2 IV
ε 3,37m 400 B3 IV
ζ 3,41m 120 G8 + F8
η 3,42m 600 B2 IV
ι 3,55m 400 B3 IV
φ1 3,57m 200 K5 III
κ 3,7m 200 B9 + A2
π 3,91m 400 B5 + B5
χ 5 3,97m
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Lupus" katika lugha ya Kilatini ni "Lupi" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Lupi, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. PAL - Glossary "Lup", tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  6. Kakkab - Naming Stars, tovuti ya Ukia, iliangaliwa Novemba 2017; hapa jinsi ilivyo pia kwa makundinyota mengine jina rasmi la nyota angavu zaidi linatunza hapa jina la Kiarabu lililokuwa kawaida kwa kundinyota lote
  7. Lupus, tovuti ya Constellation Guide, iliangaliwa Oktoba 2017
  8. KAKKAB (Alpha Lupi), tovuti ya Prof. Jim Kaler

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 278 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331