Bikari (kwa Kilatini na Kiingereza Circinus) [1] ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakusi.

Nyota za kundinyota Bikari (Circinus ) katika sehemu yao ya angani

Mahali pake

Bikari lipo karibu na nyota angavu ya Rijili Kantori (Rigili Kentaurus) kwenye ukanda wa Njia Nyeupe. Linapakana na kundinyota za Kantarusi (Centaurus), Nzi (Musca), Ndege wa Peponi (Apus), Pembetatu ya Kusini (Triangulum Australe), Pembemraba (Norma) na Dhibu (Lupus).

Jina

Bikari ni kati ya kundinyota zilizobuniwa katika enzi ya kisasa. Jinsi ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kwenye angakusi pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu, kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Kundinyota hili ilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “le Compas “ lililomaanisha “bikari” yaani kifaa cha kuchorea duara.

Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za anga ya kusini ambazo wakati ule zilianza tu kujulikana kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Alipima nyota 10,000 akazipanga katika makundinyota na kutunga majina kwa makundinyota mpya 14[2]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini kama "Circinus“(Bikari).

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale. Bikari imepokelewa kati ya makundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Circinus. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Cir'.[4]

Nyota

Nyota za Bikari ni chache na dhaifu; angavu zaidi ni Alpha Circini ambayo ni nyota kigeugeu yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.19 ikiwa umbali wa miakanuru 54 kutoka Dunia. [5] Spektra yake inonyesha utokaji wa stronti, chromi na europi [6].

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Circinus " katika lugha ya Kilatini ni "Circini" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Circini, nk.
  2. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. Motz, Lloyd; Nathanson, Carol (1991). The Constellations: An Enthusiast's Guide to the Night Sky. London, United Kingdom: Aurum Press. uk. 387. ISBN 1-85410-088-2. 
  6. Kaler, Jim. "Alpha Circini". Stars. University of Illinois. Iliwekwa mnamo 26 October 2012.  Check date values in: |accessdate= (help)

Viungo vya Nje

  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Bikari (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.