Bernard Mloka Luanda (anafahamika zaidi kwa jina lake la kisanii kama Easy-B au Big EZ-EZ B; amezaliwa 6 Agosti, 1976) ni msanii wa muziki wa hip hop kutoka nchini Tanzania. Yupo katika kundi la muziki wa hip hop la Kwanza Unit. Easy B ni mmoja kati ya wasanii wa mwanzo kabisa walioshiriki vilivyo katika kuikuza hip hop ya Tanzania.

Eazy B.
Kuanzia kushoto K-Singo (KBC), D-Rob, Fresh G, Y-Thang, Eazy B., Zavara
Kuanzia kushoto K-Singo (KBC), D-Rob, Fresh G, Y-Thang, Eazy B., Zavara
Maelezo ya awali
Jina la kuzaliwa Benard Mloka Luanda
Pia anajulikana kama Big EZ
EZ B
Amezaliwa 6 Agosti 1976 (1976-08-06) (umri 48)
Asili yake Morogoro, Tanzania
Aina ya muziki Hip hop
Kazi yake Rapa
Ala Sauti
Miaka ya kazi 1988-hadi leo
Studio Mawingu Studios
Ame/Wameshirikiana na Kwanza Unit

Historia

hariri

Maisha ya awali

hariri

Easy alizaliwa na jina la Bernard Mloka Luanda mnamo tarehe 6 Agosti 1976 huko jijini London, Uingereza. Yeye ni mtoto wa tatu na wa kiume pekee kutoka kwa Mzee Luanda. Alianza elimu ya awali hadi darasa la nane akiwa hukohuko nchini Uingereza. Mwaka wa 1986, alirudi Tanzania na kujiunga darasa la tano ili aweze kuendana na elimu ya Kitanzania. Huko Dar, alijiunga na shule ya msingi ya Olympio. Hii ilitokana na lugha, wakati alivyorudi Tanzania alikuwa hajui kabisa Kiswahili. Kiingereza tu ndiyo lugha aliyokuwa anaijua. Baada ya kumaliza elimu ya msingi, akajiunga na shule ya Sekondari ya Aga Khan (AKMSS - Aga Khan Mzizima Secondary School).

Maisha ya muziki

hariri

Kabla ya kuanzishwa kwa KU Crew, EZ B alikuwa katika kundi la Tribe X, kundi ambalo lilianzishwa mwaka 1991 - wakati huo EZ akiwa kidato cha tatu pale Mzizima. Kundi lilikuwa na wanachama kama vile Fresh G , Y Thang , Dray B , Killa B na Tuff Jam. Kwa pamoja walishiriki katika shindano la Yo Rap Bonanza la mwaka wa 1992. Shindano hilo lilikuwa likiandaliwa na Kim and the Boyz Promotion. Katika shindano hili, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Saleh Jabri, ya pili Nigga One na tatu ikabebwa na EZ. Kim ni miongoni mwa watu waliohamasisha kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa muziki wa rap nchini Tanzania, hasa katika jiji la Dar es Salaam.

Kuunda kundi la KU

hariri

Hamasa ya muziki wa rap Dar inakua kwa kasi ya ajabu. Makundi mengi na uhasimu ni mwingi vilevile. Wazo la kuunda KU ilikuwa kuwaleta vijana pamoja ili kufanya jambo kubwa zaidi. Ili kuunda KU, ilibidi wasanii kutoka Tribe X, yaani, EZ, Fresh na Y Thang wajiunge na Raiders Posse na Villain Gangstaz - kwa pamoja wakafanikiwa kuanzishwa kwa Kwanza Unit. Katika mchanganuo wa kimakundi, kutoka Raiders Posse kuliwa na wasanii kama vile Nigga One, D-Rob, Eddy Cox, James Paul Wamba, KBC na DJ Mwamba. Vilevile walikuwa na uhusiano wa karibu sana na kina Samia X na Cool Moe Cee. Kwa upande wa kina Villain Gangstaz alikuwemo Rhymson lakabu Zavara (huyu ni mjombake Zaiid), Mr. Bulbo lakabu B-Rock, Mr. Gaddy Groove na MC Eddy.[1]

Kusimama kwa KU

hariri

Wakati KU Crew kila mmoja akijaribu kusimama kivyake, EZ alipata kurekodi nyimbo tatu. Moja ya Kiingereza na mbili za Kiswahili. Ngoma hizo ni "Time is Due", "Nimerudi" na "Mchezo Huu wa Rap". Bahati mbaya, hazikufanya vizuri katika soko - hasa kwa kukosa kutangazwa vyema na vilevile hazikuungwa mkono kivile. Hali halisi KU walipunguza kasi tu, na si kusimama kabisa katika gemu. Kati ya 1998 na 2000 mwanzoni, baadhi ya wanachama wa KU walisafiri zao ughaibuni na wengine wakawa wanafanya shughuli zingine binafsi katika kusukuma gurudumu la maisha. Zavara Mponjika alienda Kanada, Y. Thang na Samia X nchini Uingereza, KBC Marekani na baadaye kurudi tena Tanzania. EZ alikuwa Tanzania kwa kipindi chote.

Muziki na wasanii wengine

hariri

Kwanza kabisa akiwa na Tribe X, wakati huo walivyobaki watatu, yaani, EZ B, Fresh G na Y Thang waliwahi kurekodi wimbo wao mmoja ulioitwa "Put Ya Head". Wimbo ulirekodiwa katika studio za Mawingu chini ya mtayarishaji DJ Bonny Luv. Wimbo huo ulirekodiwa mwaka 1993. Katika hili, hawa ndiyo walikuwa wasanii wa kwanza wa hip hop ya Tanzania kurekodi kwa majaribio katika studio za Mawingu na baadaye wakaja Kwanza Unit na kurekodi albamu nzima. EZ vilevile amewahi kufanya kazi na wasanii wengine mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sugu katika wimbo wake wa "Nimesimama" katika kiitikio. Mbali na kushiriki kuimba kiitikio katika wimbo huo, EZ vilevile amemtungia Sugu wimbo wa "Black Queen" na kuimba beti moja katika wimbo wa "Go You Open". Nyimbo hizo zote zinapatikana katika albamu ya Ndani ya Bongo ya Sugu.

Msanii wa kujitegemea

hariri

Katika zile nyimbo zake tatu, alizipeleka redio Clouds na kumkabidhi DJ Steve B, huko Magic FM alimkabidhi Songa wa Songa na East Africa Radio alimkabidhi John Dellinger (DJ JD). JD aligonga sana ule wimbo wa Kiingereza na kuupa sifa kemkem. Lakini kwa upande wa pili wa Steve B hakuupiga kabisa. Tena kuna siku walikutana lakini Steve alikana kama EZ aliwahi kumpa CD ya nyimbo zake. Angalau Songa alipiga wimbo wake wa "Nimerudi" japo mara tatu, halafu akaipotezea mazima. Harakati hizi za kurekodi nyimbo kwa gharama zako halafu mwisho wa siku hazipigwi redioni zilimvunja moyo EZ kuendelea na muziki. Jambo la ajabu sana kwa msanii mkongwe aliyeitoa sanaa kutoka sifuri hadi ilipo kuona hathaminiwi wala haheshimiki na vyombo vya kukuza muziki kwa kipindi hiko cha mwaka 2002.

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri
  1. Eazy B. katika Mkasi TV. "Mkasi | S15E12 with KBC & EASY B Extended Version"..
  Makala hii kuhusu mwanamuziki fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Eazy B. kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.