Elimuanga ya kimagharibi

Elimuanga ya kimagharibi inataja elimu ya nyota jinsi ilivyopata msingi wake katika utamaduni wa Ugiriki ya Kale. Ni mapokeo ya pamoja kati ya utamaduni wa Waislamu na utamaduni wa Ulaya, tofauti na mapokeo katika sehemu nyingine za Dunia kama vile Bara Hindi au China.

Wagiriki walipokea habari nyingi kutoka wataalamu wa Babeli na Mesopotamia (Iraki ya leo).

Elimu ya Wagiriki iliyokusanywa katika Almagesti ya Klaudio Ptolemaio iliendelezwa kwa karne kadhaa hasa kati ya wataalamu wa nchi za Uislamu katika Asia ya Magharibi (au Mashariki ya Kati) ikaendelea kuwa msingi wa elimuanga ya kisasa iliyokua katika Ulaya tangu karne ya 16 na utafiti wa Kopernikus.

Kwa hiyo kuna mapokeo ya pamoja katika elimu ya nyota ya nchi za Ulaya na nchi za Kiislamu. Inatumia namna ileile ya kupanga nyota katika kundinyota lililo tofauti na maeneo mengine ya Dunia kama Bara Hindi au China pamoja na Asia ya Mashariki. Kutokana na msingi ule kuna pia majina ya nyota yanayotumiwa kwa pamoja katika lugha za Ulaya na Kiarabu. Majina ya nyota nyingi ni ya Kiarabu ilhali majina ya makundinyota yanarejelea mara nyingi mitholijia ya Ugiriki.

Viungo vya Nje

hariri