Kaptula la Marx
Kaptula la Marx ni tamthiliya iliyotungwa mnamo mwaka 1978 na mwandishi Euphrase Kezilahabi kutoka nchini Tanzania. Ni kejeli kali kuhusu siasa ya Tanzania hasa ya Ujamaa na rais wa wakati ule Julius Nyerere.
Kutokana na ukali wa ukosoaji wake, tamthiliya haikuchapishwa hadi mwaka 1999[1] ingawa ilifanyiwa uigizaji wa kwanza Septemba 1988 huko Bagamoyo kwenye Tamasha la 7 la Sanaa na Utamaduni wa Mtanzania.[2]
Yaliyomo
haririTamthiliya ina sehemu 6 ambako mchezo hubadilisha mahali pake kati ya gereza lenye wafungwa 6 pamoja na kiongozi wao "Mwangaza Africanus" na serikali ya nchi isiyotajwa jina chini ya raisi anayeitwa Kapera.
Chanzo ni jaribio la wafungwa gerezani kukusanya habari nyingi za "dunia ya nje" iwezekanavyo kwa kuiangalia kupitia shimo dogo ukutani.
Wakati huohuo raisi anayeitwa Kapera baada ya kusoma Marx anaamua kubadilisha siasa yake kwa manufaa ya watu wengi. Kwa kusudi hii anaamua kuvaa "kaptula la Marx" na shati ya Mao. Nguo zote mbili ni kubwa mno kwake. Mawaziri wake wanamwitikia na kuvaa vilevile. Pamoja wanaondoka walipo kutafuta nchi ya usawa. Katika sehemu ya 4 wanaondoka kuelekea nchi ya usawa na undugu. Njiani wanakutana na jitu anayeitwa "Korchnoi Brown" na kuwapa maelekezo. Lakini wanashindwa kufika kwa sababu mawaziri hawafai.
Wafungwa gerezani wakati huohuo wanafanya maigizo kati yao wakijadili siasa ya nchi. Mwangaza Africanus anasoma ujumbe kwa viongozi wa Afrika anapokataa siasa zao.
Mawaziri wanaonyeshwa baadaye jinsi walivyo kama vipofu na kutumia mateso ya wafungwa kama mbinu.
Katika sehemu ya mwisho wafungwa wanatoka nje na kupindua serikali ya Kapera anayesalitiwa na mawiziri wake. Kicheko cha Korchnoi Brown kinafunga thamthiliya.
Mazingira ya kuandikwa kwa "Kaptula la Marx"
haririKezilahabi aliandika "Kaputula la Marx" mara baada ya maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tarehe 5 Machi 1978 na azimio la rais Nyerere kuwafukuza wote chuoni na kupioga marifuku umoja wao DUSO.
Kezilahabi aliyekubali hoja za wanafunzi alishtuka sana kutokana na matendo ya viongozi wa chuo na siasa waliokataa kuwasikiliza. Tamthiliya iliandikwa haraka na kusambazwa kwa kopi lakini haikufanyiwa uigizaji wakati ule. Hata hivyo ilisomwa na watu wengi waliipenda. Kampuni ya Tanzania Publishing House ilitaka kuchapisha tamthiliya lakini iliambiwa na serikali kutoendelea.
Nukuu
haririMaelezo ya jitu Korchnoi Brown[3] kwa raisi Kapera na mawaziri waku kuhusu njia ya kufikia nchi ya usawa:
- “Mtakwenda! Halafu mtapinda, mtapinda tena, halafu tena mtapinda, mwishowe mtapindapinda hadi mtakapofika mabonde yenye matope. Mtapita katikati ya matope. Halafu milima, halafu misitu yenye miiba hadi mtakapofika jangwani. Kutoka jangwani mtaingia tena bondeni chini kwa chini hadi baharini. Hakuna mitumbwi wala ngalawa. Mtaogelea, ingawa kuna papa wengi. Mkishavuka mtafika nchi iitwayo Svoboda[4]. Kabla ya kuondoka katika nchi hii itawabidi kupambana na majitu yanayofanana na mimi. Mkitoka hapo mtafika kwenye njia nyembamba. (Akiwaonyesha mawaziri) Hawa hawatapita hawa! Njia hiyo itawafikisha katika nchi iitwayo Fraternite[5]. Kutoka Fraternite mtafika Usawa. Ulizeni tu watu watawaonyesha! Mkifika Usawa mtawakuta Waswahili wenzenu wameketi nje ya ikulu ndogo ya Ravensto” (Kaptula la Marx uk. 20)
Marejeo
hariri- ↑ Kezilahabi, E. 1999. Kaputula la Marx. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press
- ↑ Habari nyingi za makala hii zinafuata maelezo ya Chris Bulcaen katika Swahili-Forum - 4/1997 (taz. chini)
- ↑ "Korchnoi" ni jina la Kirusi, "Brown" ya Kiingereza; hii inarejea njia ya Tanzania ya Nyerere kati ya "mashariki" ya kikomunisti na "magharibi" ya kibeberu
- ↑ Svoboda: neno la Kirusi la kumaanisha "uhuru"; jina la nchi larejea wito wa mapinduzi ya Kifaransa -taz. chini-
- ↑ Fraternite: neno la Kifaransa la kumaanisha "undugu" - ni moja ya wito 3 za mapinduzi ya Kifaransa "liberte, egalite, fraternite" (uhuru, usawa, undugu)
Viungo vya nje
hariri- Chris Bulcaen: "The dialogue of an author: Kezilahabi's Kaptula la Marx" Ilihifadhiwa 22 Aprili 2018 kwenye Wayback Machine.; katika Swahili-Forum - 4(1997), Cologne (imepatikana 8-01-2013 kwenye seva ya qucosa.de)
Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kaptula la Marx kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |