Tamthilia

(Elekezwa kutoka Tamthiliya)
Ukumbi wa maonyesho Colon.
Mchoro unaonyesha namna watu wanavyocheza tamthilia.

Tamthilia (pia: Tamthiliya au Tamthilia-Mchezo, kutoka neno la Kiarabu) ni moja kati ya sehemu za utunzi wa hadithi au fasihi simulizi (ngano au hadithi) ambayo mara nyingi tunaona katika kumbi za maonyesho au kupitia televisheni, au tunasikia kupitia redio.

Tamthilia au mchezo mara nyingi huwa mazungumzo baina ya watu, na kwa kawaida huwa mchezo hatuutazami katika televisheni tu, bali hata kuna watu wengine hufuatilia kwa kupitia maandiko yenye tamthiliya hizo na kuzielewa vyema.

Watu tunaowaona wanafanya tamthilia ni waigizaji; katika ukumbi wa maonyesho husimama juu ya jukwaa na kuanza kutoa burudani yao huku watu wakiwaangalia (watazamaji) wanaweza wakawaona vyema kabisa.

Mwongozaji anawasaidia waigizaji kufanya kazi zao vyema, au anawaeleza namna ya mchezo jinsi unavyotakiwa kuchezwa.

Kuna aina nyingi za michezo au tamthiliya, lakini kuna michezo ambayo inaonekana kuwa muhimu kupita yote:

  1. Trejidia - huu ni mchezo wa huzuni tu, kwa sababu ya mikosi na nuksi, kwa sababu ya mbabe hayuko ngangali, au kwa sababu za kimila au imani fulani.
  2. Komedia - huu ni tamthilia chekeshi: hukusudiwa kuonyesha vituko vya kuchekesha na unaishia na vichekesho tu. Vitu vilivyo katika mchezo huu ni vya kuchekesha; unavunja mbavu. Ujenzi wa wahusika si muhimu, matukio hayawekewi sababu maalumu za kuridhisha. Msuko wake hauna utungamano mzuri. Tamthilia nyingi zenye mgongano wa lugha huwa chekeshi.
  3. Domestiki drama au Igizo la kawaida - huu ni mchezo wa maisha ya kawaida, familia na marafiki.
  4. Trejikomedia - huu ni mchezo mchanganyiko wa vitu vyote viwili, vichekesho na huzuni halikadhalika.
  5. Melodrama - huu mara nyingi ni vichekesho na unaishia na furaha. Ndani yake kunakuwa na maadui - watu wabaya - lakini mbabe hushinda. Msisimko wake unakuwa mkali sana. Ni kinyume cha trejidia/tanzia. Mwisho/hatima ya mhusika huwa ni ushindi. Matokeo yake huwa ya kusisimua hasa kwa hadhira.
  6. Simboliki - huu unahusu fikra za uigizaji au mchezo. Watu wachezao katika mchezo si muhimu. Simboliki pia waweza kuitwa kwa jina la kitaalamu kama "expressionistic". Ni kuhusiana zaidi na waongozaji na watunzi wakiwa wanatoa fikra zao katika mchanganuo tofauti.
  7. Tamthiliya za kihistoria - mhusika anaibua matukio ya kihistoria; k.m. Rise and Fall of Idi Amin Dada.
  8. Tamthiliya tatizo - zinaangazia tatizo linalowakumba wanajamii wakati fulani, kwa mfano, ufisadi. Mifano ya tamthiliya hizi ni k.v. Kigogo (Pauline Kea) na Mstahiki Meya (Timothy Arege).

Mabadiliko na maendeleo ya tamthiliya za KiswahiliEdit

Kwa kutumia muundo wa Shakespeare, waandishi waliandika tamthiliya kwa lugha ya Kiswahili na zilihusisha masuala ya Kiafrika. Wakati wa ukoloni, drama ilikuwa kwa ajili ya Wazungu na Waafrika wachache waliojua Kizungu. Baadaye, waandishi wazalendo waliotaka kuwasiliana na umma, iliwabidi watunge tamthiliya yao kwa lugha ya Kiswahili. Baadaye, licha ya tamthiliya kuzingatia matumizi ya lugha ya Kiswahili, walianza kuzitazama, kuchunguza na kuzifanyia majaribio.

Tamthiliya za awali, k.v. Wakati Ukuta na Heshima Yangu, hazikuwa na utohozi wa matumizi ya fani za sanaa za maonyesho ya jadi. Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1960, na mwanzoni mwa miaka ya 1970, tamthiliya zilianza kuonyesha mwelekeo mpya. Pia, falsafa na imani za Kiafrika kabla ya ubepari zilianza kudidimia kidogo.

Historia ya tamthiliya za KiswahiliEdit

Syango na Mazrui (1992) walipanga historia ya tamthiliya za Kiswahili katika vipindi vinne:

Tamthiliya za kwanza kuchapishwa zilikuwa kati ya miaka 1950-1960Edit

Baadhi ya tamthiliya hizo ni kama vile: Nakupenda Lakini... (Henry Kuria, 1957), Afadhali Mchawi, na pia Mgeni Karibu (Graham Hyslop, 1957), Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi (Ngugi 1961). Zilizungumzia masuala ya jamii chache zikiwa za upelelezi. Tamthiliya nyingine zilizungumzia masuala ya kutovunja sheria zikirejelea wakoloni. Pia zilibainisha mgongano baina ya jamii za makabila tofautitofauti. Nyingi zilikuwa na lengo za burudani. Pia ziliendelea kudunisha hadhi ya Waafrika ingawa ni za Kiswahili. Mwaka 1960 ndipo Little Theatres zilianzishwa kwa burudani ya Wazungu.

Tamthiliya baada ya 1960Edit

Tamthiliya hizi zilijaa maudhui ya kimapenzi, migogoro ya kitamaduni, maudhui ya kikoloni. Tamthiliya hizi ni kama vile: Wakati Ukuta na Kwenye Ukingo wa Thim (Hussein Ibrahim), Pambo (Peninah Muhando), na Tazama Mbele (Kitsau Jay).

Tamthiliya za mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970Edit

Maudhui yalikuwa: masuala ya ukoloni, historia ya Waafrika katika mapinduzi, haki za wanyonge. Kwa mfano: Mzalendo Kimathi (Ngugi), Mkwawa wa Hehe.

Tamthiliya za kuanzia 1970Edit

Zilikuwa na mwamko mpya. Zilichunguza jamii za Afrika Mashariki kwa mkondo mpya. Zilizungumzia: ukoloni mamboleo, uongozi, siasa na matatizo mengine kama vile ufisadi, unyanyasaji, uporaji n.k. Kwa mfano; Aliyeonja Pepo (Faruk Topan), Mashetani (Ibrahim Hussein), Kilio cha Haki (Alamin Mazrui).

Viungo vya njeEdit

  Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tamthilia kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.