Mabasi ya mwendokasi
Mabasi ya mwendokasi (kwa Kiingereza: bus rapid transit, kifupi: BRT) ni mfumo wa usafiri wa mjini ambako kuna njia za pekee za mabasi kwenye barabara zinazofungwa kwa magari madogo, mabasi ya kawaida na baisikeli. Katika mfumo huu mabasi ya mwendokasi hupewa kipaumbele kwenye njiapanda. Kuna pia mbinu za kuwezesha abiria kuingia na kuondoka pamoja na kukata tiketi haraka.
Kwa njia hiyo uwezo wa mabasi ya kubeba abiria wengi huongezwa na kuepukana na matatizo ya mabasi ya mjini ya kawaida ambayo yanaweza kukwama katika msongamano wa magari.
Kwa njia hiyo mfumo wa mabasi ya mwendokasi ina faida zinazopatikana vinginevyo kwa mfumo wa metro (usafiri kwenye njia za reli) au tramu (usafiri kwa reli ndogo mjini) lakini kwa kuepukana na gharama kubwa kutengeneza njia za reli juu au chini ya ardhi. Hata hivyo mifumo ya mabasi ya mwendokasi haifikii uwezo wa metro wa kusafirisha abiria wengi kwa wakati mfupi.