Madusa
Madusa (pia: Medusa, gir. Μέδουσα medusa) ni jina la zimwi wa kike katika mitholojia ya Kigiriki. Alitazamiwa kuwa mmoja wa Gorgoni watatu, waliozaliwa kama watoto wa miungu wa bahari.
Katika masimulizi Madusa alikuwa na uso wa kutisha. Nywele zake zilikuwa nyoka za sumu, meno kama nguruwe mwitu na ulimi mrefu uliotoka nje ya mdomoni. Kila mtu aliyemtazama alikufa akibadilishwa kuwa jiwe.
Hata hivyo kuna pia picha ambako Madusa anaonekana kama mrembo kwa sababu kuna pia simulizi ya kwamba alizaliwa kama binti mzuri sana. Siku moja alifanya mapenzi na Poseidon mungu wa bahari (wengine walisema alibakwa na Poseidon) katika hekalu ya Athena. Athena alikasirika na kumpa Madusa uso wa kutisha.
Madusa alikatwa kichwa chake na shujaa Farisi (en:Perseus); Farisi alishindwa kupata zawadi za kutosha kwa harusi ya mfalme Polidektes hivyo mfalme huyu alidai ampatie kichwa cha Madusa, lakini kwa ukeli alitaka kumwua Farisi kwa njia hii.
Farisi alipata msaada wa miungu mengine na hasa Athena alimshauri kutomtazama Madusa moja kwa moja bali alimpa ngao yake iliyokuwa kama kioo upande wa ndani. Hivyo Farisi alisafiri hadi kisiwa ambako Gorgoni walikaa akawakarinia wakati wanalala; alikata kichwa cha Madusa kwa kumwangalia kupitia ngao akaweka kichwa mfukoni na kukimbia nayo.
Baadaye aliweza kutumia kichwa chaMadusa mara kadhaa kama silaha wakati aliposhambuliwa; hapa alitoa kichwa kutoka mfuko akigeuza kichwa kando na kuweka kichwa mbele ya washambulizi waliogeukiwa mara moja na kuwa jiwe.
Kwa njia aliweza kumshinda hata mungu Atlasi aliyegeukiwa kuwa milima ya Atlas.
Masimulizi ya Madusa inakumbukwa pia kwenye anga la usiku ambako kundinyota inatunza jina la Farisi na nyota angavu ndani yake hutazamiwa kama kichwa cha Madusa - kwa Kiswahili inaitwa Rasi Madusa, kwa Kiarabu na Kiingereza "Algol".
Viungo vya Nje
hariri- Gorgones and Medousa, tovuti ya Aaron Atsma theoi.com, iliangaliwa Novemba 2017
- Hadithi ya Perseus na Madusa, tovuti Star Tales ya Ian Ridpath, iliangaliwa Novemba 2017