Rasi Madusa (ar., lat. & ing. Algol pia β Beta Persei [2], kifupi Beta Per, β Per) ni nyota angavu zaidi katika kundinyota la Farisi (Perseus). Rasi Madusa ni nyota badilifu iliyotambuliwa tayari na wataalamu wa Misri ya Kale[3].

Rasi Madusa
(Beta Persei, Algol)
Kundinyota Farisi (Perseus)
Mwangaza unaonekana 2.12 – 3.5[1] (geugeu)
Kundi la spektra Aa1: B8 V Aa2: K0 IV Ab: A7
Paralaksi (mas) 36.27 ± 1.40
Umbali (miakanuru) 90
Mwangaza halisi Aa1: -0.07 Aa2: 2.9 Ab: 2.3
Masi M☉ Aa1: 3.17 Aa2: 0.7 Ab: 1.76
Nusukipenyo R☉ Aa1: 2.73 Aa2: 3.48 Ab: 1.73
Mng’aro L☉ Aa1: 182 Aa2: 6.9 Ab: 10
Jotoridi usoni wa nyota (K) Aa1: 13000 Aa2: 4500 Ab: 7500
Majina mbadala Gorgona, Gorgonea Prima, Demon Star, El Ghoul, 26 Persei, BD+40°673, FK5 111, GC 3733, HD 19356, HIP 14576, HR 936, PPM 46127, SAO 38592.
Mfano jinsi gani nyota badilifu inatokea kama nyota maradufu zinazungukana na kufunikana

Jina hariri

Rasi Madusa inayomaanisha “Kichwa cha Madusa” ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [4]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema kwa kawaida رأس الغول ras al-ghul inayomaanisha „kichwa cha zimwi " wakimfuata Klaudio Ptolemaio aliyeorodhesha nyota hii kama “ng’avu ya Gorgoni (zimwi)“ [5]. Katika mitholojia ya Kigiriki Madusa alikuwa mmoja wa „Gorgoni“ watatu waliokuwa zimwi wa kutisha; Madusa alikuwa na uso mbaya kiasi cha kila mmoja aliyemwona alibadilika kuwa jiwe. Farisi (Perseus) alifaulu kukata kichwa chake hivyo yuko angani kama kundinyoto akibeba Kichwa cha Madusa. Waarabu walitafsiri „Gorgoni“ ya Ptolemaio kama „al-ghul“ na jina lao lilipokelewa baadaye na wataalamu wa Ulaya kwa umbo la Algol. Kwa matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulikubali jina la Kiarabu na kuorodhesha nyota hii kwa jina la "Algol" [6] .

Beta Persei ni jina la Bayer kwa sababu Beta ni herufi ya pili katika Alfabeti ya Kigiriki na Rasi Madusa ni nyota angavu ya pili katika Farisi - Perseus.

Tabia hariri

Rasi Madusa iko kwa umbali wa miakanuru takriban 90 kutoka Jua letu. Ni nyota badilifu inayobadilisha mwangaza unaoonekana baina ya mag 2.3 na 3.5 kila baada ya karibu siku tatu [7]. Mabadiliko haya yalitazamiwa tangu kale na Waarabu waliita pia „Nyota ya Sheitani“. Tofauti za mwangaza zinatokana na tabia za Rasi Madusa kuwa nyota maradufu ambako nyota yenye mwangaza mdogo inazunguka nyota yenye mwangaza mkubwa. Hizi mbili zinatambuliwa kwa darubini na nyota kuu inaitwa Algol Aa1 iliyopo katika kundi la spektra B8 na mng’aro wa Lo 182 (yaani mara 182 kuliko Jua). Inazungukwa na Algol Aa2 ambayo ni jitu jekundu, ni kubwa zaidi lakini mwangaza wake ni mdogo. Nyota hizi mbili ziko karibu kwa umbali wa vizio astronomia 0.062 na kila safari nyota kubwa zaidi iko kati ya Dunia na Algol Aa1 tunaona kushuka kwa mwangaza.

Kuna bado nyota ya tatu Algol Ab yenye umbali wa vizio astronomia 2.69 na zote tatu zinazungukana katika muda wa siku 681. Masi ya nyota zote kwenye mfumo huu ni takriban Mo 5.8, ikiwa uhusiano kati ya sehemu tatu ni takriban 4.5 : 1 : 2.

Tanbihi hariri

  1. Namba kufuatana na Baron, F. & alii (2012)
  2. Persei ni uhusika milikishi (en:genitive) wa "Perseus" katika lugha ya Kilatini na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Beta, Beta, Gamma Persei, nk.
  3. Porceddu, S. & alii (2008)
  4. ling. Knappert 1993
  5. Tooner (1984) anatafsiri uk. 352 „Stars in the Gorgon-head; the bright one“ isipokuwa Ptolemaios mwenyewe hataji kichwa( taz. Heiberg 1903), uk 62
  6. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017
  7. Siku 2.87 yaani siki mbili na masaa 20 na dakika 48

Viungo vya Nje hariri

Marejeo hariri

  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 331 (online kwenye archive.org)
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Porceddu, S.; Jetsu, L.; Lyytinen, J.; Kajatkari, P.; Lehtinen, J.; Markkanen, T.; et al. (2008). "Evidence of Periodicity in Ancient Egyptian Calendars of Lucky and Unlucky Days". Cambridge Archaeological Journal. 18 (3): 327–339. online hapa
  • Baron, F.; Monnier, J. D.; Pedretti, E.; Zhao, M.; Schaefer, G.; Parks, R.; Che, X.; Thureau, N.; Ten Brummelaar, T. A.; McAlister, H. A.; Ridgway, S. T.; Farrington, C.; Sturmann, J.; Sturmann, L.; Turner, N. (2012). "Imaging the Algol Triple System in the H Band with the CHARA Interferometer". The Astrophysical Journal. 752: 20 online hapa
  • Heiberg, Johan Ludvig: Claudii Ptolemaei Opera quae exstant omnia, Syntaxis Mathematica Vol I pars II, Lipsia 1903
  • Ptolemy's Almagest, translated and annotated by G.J. Toomer, London 1984,

ISBN 0-7156-1588-2 online hapa