Makaa mawe

(Elekezwa kutoka Makaamawe)
Kwa makaa yanayotengenezwa kutokana na kuni tazama makaa

Makaa mawe ni aina ya mwamba mashapo au mwamba metamofia na fueli kisukuu muhimu. Ilitokea kutokana na mabaki ya mimea ya kale iliyogeuzwa kuwa aina ya mwamba katika mchakato wa miaka mamilioni.

Kipande cha makaa mawe
Kipande cha anithrasiti

Kikemia ni hasa kaboni. Kijiolojia inatokea kama kanda pana au nyembamba katikati ya miamba mengine. Huchimbwa mara nyingi katika migodi chini ya ardhi au kama iko karibu na uso wa ardi katika machimbo ya wazi yaliyo kama mashimo makubwa.

Asili ya makaa mawe

hariri

Asili ya makaa ni mabaki ya mimea iliyokufa miaka mingi iliyopita. Kama mabaki ya mimea yanafunikwa kwa maji au kuzama katika matope hayaozi jinsi ilivyo katika kutokea kwa mboji. Kinachotokea ni ganda la nyuzi za mimea zinazokauka wakati maji yanapungua tena. Maganda haya ni kitangulizi ya makaa mawe. Mabaki haya yalifunikwa tena na mashapo yaliyokuwa kanda la mawe juu yao. Uzito wao ulileta kanieneo na pia joto na hapo nyuzi za mimea zilikandamizwa kuwa mawe mashapo. Kama maganda ya mashapo juu ya makaa changa yaliongezeka sana kanieneo iliweza kutosha kuubadilisha mwamba kuwa mwamba metamofia.

Hatua ya kwanza ni makaa kahawia ambayo ni mwamba laini. Kama makaa kahawia imekaa muda mrefu zaidi na hasa kama ilifunikwa na maganda mapya ya mashapo hivyo kupata shindikizo kubwa zaidi yalibadilika kuwa makaa meusi. Kama kanieneo iliongezeka metamofia ilianza na kuleta makaa mawe meusi magumu na mazito sana inayoitwa anithrasiti.

Kwa hiyo ubora wa kiuchumi na kiwango cha nishati kilichomo katika makaa unaongezeka kadri ya umri wake na kina cha mahali panapochimbwa.

Matumizi

hariri

Kiasi kikubwa cha makaa mawe yanayopatikana duniani huchomwa katika vituo vya umeme; katika nchi za kaskazini kuna pia nyumba nyingi zinazotumia makaa mawe kwa kupasha moto wakati wa baridi. Lakini matumizi haya yamepungua kutokana na machafuko ya vumbi lake na gesi chafu wakati wa kuchoma.

Sehemu kubwa hubadilishwa pia kuwa mkaazimawe kwa kuipasha moto kiwandani; mkaazimawe hutumiwa katika utengenezaji wa chumapua (feleji).

Aina za makaamawe

hariri
 
Kipande cha makaa kahawia katika mgodi

Mabaki ya mimea yasiyoweza kuuoza yanaendelea hatua kwa hatua kuwa:

  1. Nyuzi za mimea zisizooza (en:Peat) zinazopatikana kama maganda manene kwa wingi hasa katika nchi za kaskazini na kutumiwa kiuchumi; katika Afrika kuna maeneo muhimu penye mafuriko ya kimajira kama Botswana au Mali.
  2. Makaa kahawia (en:lignite) ni makaa yenye thamani dogo zaidi huchomwa kwa kuzalisha umeme.
  3. Makaa meusi ni magumu zaidi; huchomwa pia katika vituo vya umeme na kwenye nyumba za watu. Inawezekana kuyabadilisha kuwa mafuta na petroli na mbinu hiyo ulitumiwa katika nchi zenye akiba za makaa hayo wakati kulikuwa na tatizo la kupata mafuta ya petroli kama huko Ujerumani wakati wa vita kuu ya pili ya dunia. Yalitumiwa pia kwa injini za mvuke viwandani na injinitreni zilizoendeshwa kwa mvuke.
  4. Anithrasiti ni aina ya makaa meusi yenye kiwango kikubwa cha nishati ndani yake.
  5. Kinywe (en:graphite) ni kiwango cha juu ya makaa; hupatikana mahali pachache duniani. Haiwaki kwa urahisi, hivyo hutumiwa zaidi kwa penseli au kisagwa ka ulainishaji kwenye mashine.

Athari kwa mazingira ya Dunia

hariri

Katika nchi zilizoendelea ulimwenguni, kuna harakati inayoongezeka ya kukomesha kabisa matumizi ya makaa ya mawe kwa uzalishaji wa umeme ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaotokana nayo.

 
Mgodi wa makaa ya mawe wa Opencast huko Garzweiler, Ujerumani. Panorama ya ubora wa juu.

Tazama pia

hariri

Tanbihi

hariri