Kuni ni sehemu za mti uliokatwa zinazotumiwa kama fueli zikichomwa motoni kwa kupikia au pia kwa kupashia nyumba moto.

Kuni zinapelekwa sokoni katika nchi mojawapo ya Afrika.
Kuni kwa umbo la donge hutengenezwa kutokana na mbao zilizosagwa.
Wanawake wa kiafrika wakibeba kuni
Katika sehemu nyingi za Ulaya watu huandaa kuni kwa ajili ya majira ya baridi na kuzipanga kwa namna inayosaidia kukauka na kupatikana kwa urahisi; huu mfungo utafunikwa baadaye kwa plastiki.
Mashine ya kupasua miti minene kiasi kuwa kuni inatumia hidrauliki.

Kwa kawaida kuni zinakusanywa penye miti kwa kutafuta sehemu ziliokauka au kwa kukata miti inayopasuliwa kuwa vipande vya ukubwa unaofaa.

Kwa kutumia teknolojia mpya, kuna pia kuni zinazopitishwa kwenye mashine na kupewa umbo maalumu unaofaa kwa majiko ya kisasa. Miti huweza kukatwa na msumenonyororo na baadaye kukatwa vipande vidogo kuwa kuni kwa mashine zinatotumia umeme, petroli au hidrauliki. [1]

Matumizi ya kuni

hariri

Watu wengi duniani kwenye nchi za joto hutumia kuni kwa kupikia chakula na kuchemsha maji ya kuoga au kuosha nguo.

Tangu karne ya 19 na hasa ya 20 watu wengi wamehamia matumizi ya fueli nyingine kama makaa mawe, gesi na madawa yanayotengenezwa kutokana na mafuta ya petroli au pia umeme.

Lakini hata katika nchi za baridi zilizoendelea kuna watu wengi kidogo katika mazingira ya misitu wanaopendelea kuendelea kutumia kuni kama mababu zao. Wengine wanafanya hivyo kwa sababu wana maeneo ya miti au msitu, hivyo kuni kwao ni bure; wengine wamefuata majadiliano juu ya ekolojia na wanaona ni bora kimaadili kutumia fueli ya nishati mbadala kuliko fueli ya kisukuku‎; wengine wameona ya kwamba ubao ni fueli nafuu kama wanakaa karibu na misitu na wana uwezo wa kununua majiko ya kisasa kwa nyumba zao.

Kuni na mazingira

hariri

Kuni ni fueli inayokua maana mti unazidi kukua na kuandaa kuni mpya kwa matumizi ya binadamu. Lakini matumizi yanaweza kuzidi kasi ya ukuaji upya kwa eneo fulani na hapo kuna hatari ya kuharibu mazingira.

Sheria ya uchumi wa misitu ni kuondoa kuni katika eneo fulani sawa na kiwango cha ubao kinachokua kila mwaka katika eneo hili. Hata hivyo katika nchi mahitaji ya kuni na makaa pamoja na usimamizi hafifu upande wa serikali vimesababisha kupungukiwa kwa misitu na upotevu wa udongo, kukauka kwa visima, kupungukiwa kwa mvua na kuongezeka kwa mafuriko makali.[2]

Tabia za kuni

hariri

Sifa muhimu ya kuni ni uwezo wake wa kutoa joto. Hapa kuni kavu huwaka na kutoa joto vizuri kushinda kuni mbichi yaani kuni zenye asilimia kubwa ya unyevu ndani yake.

Inasaidia kama kuni zinakatwa wakati miti inapumzika, kwa mfano wakati wa ukame au wakati wa baridi katika nchi nje ya tropiki. Katika vipindi hivyo ubao hauna majimaji mengi ndani yake. Vinginevyo kuni zinahitaji muda mwingi hadi zikauke.

Pamoja na hii tabia kama herufi na namna ya kuchoma zinatazamiwa pia, kwa mfano inapendeza zikiwaka kimyakimya bila cheche nyingi.

Tabia nyingine inayoangaliwa ni unene wa ubao, maana watu wasio na vifaa wana matatizo katika kupasua miti minene lakini penye mashine si kitu.

Vilevile aina tofauti za miti huleta kuni tofauti. Kuna aina zinazowaka haraka na hizi zinafaa sana kwa upishi. Aina nyingine huwaka polepole, ni afadhali kwa majiko ya kupasha moto nyumba katika nchi zenye baridi.

Uzito wa ubao ni pia tabia muhimu kwa ajili ya matumizi yake kama kuni. Kuni nyepesi zinachukua nafasi kubwa wakati wa kuzibeba sokoni kushinda kuni nzito zaidi; kiasi cha joto hutegemeana na uzito yaani kilogramu 1 ya kuni inaleta kiasi fulani cha joto, ila tu kama kuni ni nyepesi zinatumia nafasi kubwa zaidi.

Kuandaa kuni

hariri

Katika sehemu nyingi za Afrika kuni huchukuliwa kutoka kwa miti myembamba au matawi. Hii hukatwa kwa kutumia panga au shoka. Pale ambapo miti minene hukatwa kwa ajili ya kuni watu hutumia msumeno ama wa mkono au wa mashine.

Baadaye vipande hukatwa kwa urefu unaofaa kuisafirishwa hadi nyumbani au sokoni. Urefu huo unategemea usafiri na pia ukubwa wa majiko ya kawaida.

Pale ambapo miti minene hutumiwa kama kuni ni lazima kupasua vipande vikubwa. Hii inafanywa mara nyingi na wakatamiti wenyewe lakini watu wanaotumia kuni kwa wingi wamejipatia vifaa vya kupasulia ili wanunue kuni zao kwa bei nafuu.

Katika nchi za kaskazini kuna watu wanaotumia kuni kwa kupashia moto nyumba wakati wote wa baridi na hapa teknolojia mpya imesambaa. Kwa wale wanaopenda kutumia kuni kwa sababu za ekolojia au gharama bila kazi ya kupasua na kujaza jiko mara kwa mara kuna teknolojia inayotumia kuni kwa umbo la donge. Hapo kuni husagwa kwanza, halafu kushindiliwa kwa umbo la donge. Madonge hayo yanajazwa katika tangi na kuingia ndani ya jiko mfululizo karibu kama mafuta. Madonge ya kuni yanapatikana katika maeneo ya misitu mingi penye viwanda vya kupasulia miti. Viwanda hivyo hutumia unga wa mbao pamoja na mabaki yote yasiyouzwa kama mbao vinatengeneza madonge hayo.

Namna ya pekee ya kuandaa kuni ni kuzichoma kuwa makaa. Hasa katika miji mikubwa ya Afrika makaa yamechukua mara nyingi nafasi ya kuni zenyewe kwa sababu yanawaka kwa moto safi zaidi na hii ni muhimu katika msongamano wa watu wengi mjini.

Pamoja na hayo kuni zinachukua nafasi kubwa kuliko makaa kwa kiasi kilekile cha joto kinachotakiwa na bei za kusafirisha kuni mjini pamoja na gharama za kutunza akiba za sokoni ndani ya mji imeleta makaa kuwa nafuu.

Kutunza kuni

hariri

Katika nchi za Afrika kuni kwa kawaida hazitunzwi. Zinakatwa au kununuliwa jinsi inavyohitajika.

Hali hii ni tofauti katika nchi baridi. Huko kuna haja ya kuwa na akiba ya kutosha kwa kupashia nyumba moto maana hata siku mbili bila kuni wakati wa baridi zinaweza kuwa hatari. Kwa hiyo kuni huandaliwa na kuwekwa tayari kama akiba kwa majira yote ya baridi.

Ni muhimu kuziweka kwa namna inayoruhusu upepo kupitia kwenye vipande vya kuni na kuzikausha vizuri; penye mvua nyingi sehemu za paa hutengenezwa kwa kuni lakini siku hizi vipande vikubwa vya plastiki vinatosha.

Madonge ya kuni kwa majiko ya kisasa huwekwa katika vyumba au matangi na kutoka hapa vinapelekwa kwa njia ya mitambo hadi jikoni.

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri
  1. "Mashine za kukata kuni
  2. " Uharibifu wa mazingira kiini cha umaskini Tanzania, Habarileo 1.6.2014 Archived 17 Septemba 2021 at the Wayback Machine.

Viungo vya nje

hariri
 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: