Mdudu-kibibi
Mdudu-kibibi (Cheilomenes lunata)
Mdudu-kibibi (Cheilomenes lunata)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Cucujoidea
Familia: Coccinellidae
Latreille, 1807
Ngazi za chini

Nusufamilia 9:

Wadudu-kibibi (kutoka Kiing. lady beetle) ni mbawakawa wa familia Coccinellidae katika oda Coleoptera walio na madoa kwa kawaida. Mara nyingi madoa ni meusi juu ya mandharinyuma ya rangi kali kama nyekundu, machungwa au njano. Jina la mbawakawa hawa linatokana na Maria, mamake Jesu, anayeitwa Bibi Maryam mara nyingi.

Kwa kawaida mwili wa mdudu-kibibi ni mviringo au duaradufu na ana kichwa kidogo na miguu mifupi. Kichwa, miguu na vipapasio ni nyeusi lakini kichwa kinaweza kuwa na madoa meupe. Mabawa ya mbele ya wadudu-kibibi wengi yana rangi kali, kama nyekundu, machungwa au njano, pamoja na madoa meusi. Wengine wana mabawa meusi na madoa wenye rangi kali. Wengine tena wana milia badala ya madoa. Mwishowe kuna wadudu-kibibi weusi, kijivu au kahawia bila madoa wala milia.

Lava wa wadudu-kibibi ni mbuai wamilifu. Mwili wao umerefuka na wana miguu mirefu kiasi. Wengi ni weusi wenye madoa ya rangi kali. Wengine ni weusi, kahawia au weupe na wana miiba mingi mara nyingi.

Takriban spishi zote za wadudu-kibibi, wapevu pamoja na lava wao, hula wadudu wa nusuoda Sternorrhyncha, kama vile vidukari, wadudu-gamba na nzi weupe. Kwa hivyo wao ni marafiki wa wakulima na hupunguza matumizi ya dawa za kikemikali. Spishi nyingine hula matitiri, mayai ya arithropodi na wadudu wengine wadogo. Spishi kubwa hukamata viwavi na lava wa mbawakawa wengine. Lakini siyo spishi zote zinazokula wadudu. Spishi fulani za nusufamilia Epilachninae hula mimea na zinaweza kuwa wasumbufu sana katika kilimo, k.m. bungo wa mharagwe wa Meksiko, Epilachna varivestis. Spishi kadhaa za nusufamilia Coccinellinae hula nyoga. Na hata wadudu-kibibi walanyama hula dutu nyingine pia kama vile mana, mbelewele, mbochi, utomvu na kuvu.

Wadudu-kibibi hutumika katika uthibiti wa kibiolojia mara nyingi. K.m. Rodolia cardinalis hula spishi kadhaa za wadudu-gamba wakubwa (Monophlebidae). Cryptolaemus montrouzieri ni mbuai muhimu wa vidung'ata. Na spishi za Stethorus hula matitiri ya mimea ya jenasi Tetranychus.

Spishi zilizochaguliwa za Afrika ya Mashariki hariri

  • Brumoides nigrifrons
  • Cheilomenes aurora
  • Cheilomenes lunata
  • Cheilomenes propinqua
  • Cryptolaemus montrouzieri
  • Epilachna fulvosignata
  • Epilachna multinota
  • Epilachna sahlbergi
  • Exochomus ventralis
  • Harmonia axyridis
  • Hippodamia variegata

Picha hariri