Metali za udongo alikalini

(Elekezwa kutoka Metali ya udongo alkalini)

Metali za udongo alikalini ni mfulizo wa kikemia katika mfumo radidia unaounganisha elementi za kundi la pili yaani elementi thabiti Berili (Be), Magnesi (Mg), Kalisi (Ca), Stronti (Sr) na Bari (Ba) pamoja na elementi nunurifu ya radi (Ra) ambayo ni tokeo la mbunguo wa elementi nyingine.

Jina la "metali za udongo alikalini" linatokana na historia ya uchumbuzi wa elementi hizo. Zilianza kutambuliwa katika umbo la oksidi zake. Kampaundi hizo ziliitwa "udongo" au "ardhi" na wanakemia wa kale kama dutu zisizokuwa metali wala kuathiriwa na joto na zisiyomumunyika katika maji. Zikikorogwa katika maji zinaonyesha tabia ya alikalini.

Mfaransa Antoine Lavoisier alitambua mwaka 1789 ya kwamba ardhi hizo hazikuwa "elementi" bali kampaundi. Aliamini ya kwamba msingi wake zilikuwa elementi alizozitaja kama "elementi za udongo" zinazojenga chumvi mbalimbali akahisi ya kwamba labda udongo hizo ni oksidi za metali. Hii ilithibitishwa mwaka 1808 na Mwingereza Humphry Davy kwa njia ya elektrolisisi.

Metali za udongo alikalini ni metali laini zenye rangi nyeupe-fedha. Zinamenyuka na halojini kuwa aina za chumvi; mmenyuko na maji husababisha kutokea kwa hidroksidi alikalini.

Hazimenyuki haraka na vikali kama metali alikalini.

Zote zina elektroni mbili katika mzingo elektroni wa nje. Kwa hiyo zinaelekea kuachana na elektroni hizo kuingia katika hali kuwa ioni yenye chaji ya chanya.

Mmenyuko

hariri

Mmenyuko huongezeka kadiri ya namba atomia au ukubwa wa atomi:

  • Mmenyuko hewani:
    • Berili ni thabiti kwenye halijoto ya wastani pasipo na unyevu kwa sababu uso hufunikwa haraka na ganda la oksidi.
    • Magnesi hufunikwa pia na ganda la oksidi lakini vipande vyembaba vinawashwa kirahisi.
    • Kalisi, Stronti, Bari na Radi zinaoksidisha haraka na kuwaka mara moja katika umbo la unga.
  • Mmenyuko na Hidrojeni kwenye joto kali
    • Berili haimenyuki na hidrojeni pasipo na kichocheo.
    • Magnesi yamenyuka penye shinikizo ya juu.
    • Metali za udongo alikalini zote nyingine humenyuka na hidrojeni tayari kwenye shinikizo ya kawaida
    • Mmenyuko na maji
    • Berili haimenyuki na maji kutokana na ganda la oksidi usoni
    • Magnesi haimenyuki sawa na Berili lakini ganda hili layeyuka katika maji ya moto
    • Metali za udongo alikalini zote nyingine humenyuka vikali na maji kwenye halijoto ya wastani

Kutokea

hariri

Elementi hizo kwa jumla ni asilimia 4.16 za masi ya ganda la dunia. Kati ya metali za udongo alikalini ni:

  • 67 % Kalisi
  • 31 % Magnesi
  • 1,4 % Bari
  • 0,7 % Stronti
  • Berili kidogo sana na Radi kidogo zaidi