Mke wa Kurusi (kundinyota)

(Elekezwa kutoka Mke wa Kurusi)


Mke wa Kurusi (Cassiopeia kwa Kilatini na Kiingereza) [1]. ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kaskazini ya dunia yetu. Kundinyota hili ni maarufu kwa umbo lake la “M” au “W” kwa hiyo inaitwa pia “W ya angani” kwenye nchi upande wa kazkazini wa Dunia. Lakini kwa mtazamaji katika Afrika ya Mashariki inaonekana daima kwa umbo la “M”.

Nyota za kundinyota Mke wa Kurusi (Cassiopeia) katika sehemu yao ya angani
Nyota za kundinyota Mke wa Kurusi (Cassiopeia) jinsi lilivyochorwa mnamo mwaka 1824 pale Ulaya

Mahali pake

Mke wa Kurusi ni kundinyota la angakaskazi, hivyo haiwezi kupaa sana juu ya upeo wa macho. Katika Afrika ya Mashariki huonekana upande wa kaskazini. Ncha ya “M” wake hudokeza kaskazini kabisa.

Makundinyota jirani yake ni Mara (Andromeda), Farisi (kundinyota) (Perseus), Twiga (Camelopardalis), Kifausi (Cepheus) na Mjusi (Lacerta)..

Jina

Mke wa Kurusi lilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi na mabaharia Waswahili walioitumia kupata njia baharini wakati wa usiku.[2] Jina la Mke wa Kurusi lina sehemu mbili; “mke” ni kifupi cha mwanamke na “kurusi” linamaanisha “kiti” kutokana na jina la Kiarabu كرسي kursiy. Jina lote ni tafsiri ya Kiarabu ذات الكرسي dhaat al-kursiy yani “Bibi wa kiti” ambayo tena ni tafsiri tu ya Kilatini “mulier sedis” yenye maana hiyihiyo. Yote inarejelea mitholojia ya Ugiriki ya Kale iliyoona hapa picha ya malkia maridadi Cassiopeia akikalia kiti chake cha kifalme. Cassiopeia alikuwa mke wa mfalme Kifausi (Cepheus) akajivunia kuwa yeye mwenyewe na binti yake Mara (Andromeda) ni wazuri kushinda mabinti wa Poseidon mungu wa bahari. Hapo Poseidon aliamua kumwadhibu kwa kutuma dubwana Kestusi dhidi yake. Cassiopeia pamoja na mumewe mfalme Kifausi waliamua kumtua binti Mara-(Andromeda) kama sadaka kwa Ketusi kwa kumfunga kwenye ufuko wa bahari ili aliwe na dubwana huyu lakini shujaa Farisi (Perseus) akaingia kati na kumwokoa. Baadaye wote waliinuliwa angani kama nyota [3] kwa hiyo tunaona Mke wa Kurusi (Cassiopeia) jirani na makundinyota ya Kifausi na Mara, halafu Ketusi na Farisi aliyekuja kumwokoa Mara katika simulizi ya mitholojia..

Mke wa Kurusi ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK kwa jina Kassiopeia. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [4] kwa jina la Cassiopeia. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Cas'.[5]

Nyota

Kwa jumla kuna nyota 157 zenye mwangaza unaoonekana wa 6.5 na zaidi (zinazoweza kutazamiwa kwa macho matupu) [6]

Sehemu ya kundinyota hili penye nyota 5 angavu zaidi inaonyesha umbo la W au M (kutegemeana na mahali pa mtazamaji) na nyota hizi ni Alpha, Beta, Gamma, Delta na Epsilon Cassiopeiae[7] Nyota tatu kati ya hizi ni nyota kigeugeu zinazotambuliwa kwa macho bila darubini, maana mwangaza unaonekana tofautitofauti wakati wa kuziona. Hasa Gamma Cassiopeiae inaweza kung’aa kushinda alpha Cassiopeiae.

Nyota angavu zaidi kwa kawaida ni en:Schedar (α Alfa Cassiopeiae) ikiwa na uangavu unaoonekana wa 2.2 mag na umbali wake na dunia ni miaka nuru 228 [8]

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Cassiopeia" katika lugha ya Kilatini ni " Cassiopeiae " na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Cassiopeiae, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. ling. Allen, Star-Names and their Meanings uk, 117
  4. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  5. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy. 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R.
  6. Bortle, John E. (Februari 2001). "The Bortle Dark-Sky Scale". Sky & Telescope. Sky Publishing Corporation. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-03-31. Iliwekwa mnamo 6 Juni 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  7. The Photographic Atlas of the Stars. Boca Raton, Florida: CRC Press. 1999. uk. 20. ISBN 978-0-7503-0654-6. {{cite book}}: Cite uses deprecated parameter |authors= (help)
  8. van Leeuwen, F. (2007). "Validation of the New Hipparcos Reduction". Astronomy and Astrophysics. 474 (2): 653–64. arXiv:0708.1752. Bibcode:2007A&A...474..653V. doi:10.1051/0004-6361:20078357.

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 75 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mke wa Kurusi (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.