Ming (nasaba)

(Elekezwa kutoka Nasaba ya Ming)

Nasaba ya Ming ilitawala China kati ya 1368 na 1644.

Eneo la milki ya China chini ya nasaba ya Ming

Watawala wa Ming walichukua nafasi ya makaisari wenye asilia ya Mongolia wakafuatwa na nasaba yenye asili ya Manchuria.

Waming walijenga muundo wa serikali iliyodumu hadi mapinduzi ya 1911. Mamlaka yote yalikusanywa mkononi wa kaisari. Walihamisha mji mkuu kutoka Nanjing kwenda Beijing na kujenga Mji Haramu.

Muundo wa serikali

hariri

Wakazi wote waligawiwa katika vikundi vya wakulima, mafundi na wanajeshi na watoto walitakiwa kuendelea na kazi ya wazazi. Familia kumi walihesabiwa pamoja katika jumuiya ndogo iliyotakiwa kukusanya kodi kati yao. Wanajeshi walipewa mashamba wakatakiwa kujigharamia wenyewe.

Muundo huo uliongeza mapato ya serikali ukawezesha serikali kujenga jeshi kubwa na pia meli nyingi.

Siasa ya biashara

hariri

China ilikuwa kitovu cha biashara cha Asia lakini pia kimataifa kwa sababu Wahispania pamoja na Wareno walitumia fedha kutoka koloni zao mpya katika Amerika ya Kilatini kwa bidhaa za Kichina zilizobebwa hadi Ulaya. Kwa kurahisisha biashara hii Ureno ilipewa bandari ya Macau kama kituo cha biashara.

Jeshi na wanamaji

hariri

Hatua muhimu ilikuwa upanuzi wa kilimo kwa njia ya miradi ya kuongeza mashamba ya mpunga. Idadi ya watu katika China iliongezeka sana kufikia milioni 160 hadi 200.

Ming walijenga jeshi la kudumu la askari milioni moja wakatengeneza upya ukuta mkubwa wa China ulioleta usalama dhidi ya makabila wahamiaji wa kaskazini.

Kuanzia 1405 baharia mkuu Zheng He alianzisha safari za upelelezi kwenye Bahari ya China ya Kusini na Bahari Hindi hadi pwani za Afrika ya Mashariki. Zheng He alipewa kundi kubwa la meli na manowari lenye mabaharia makumi alfu. Alitembelea Mombasa na kuna uwezekano kuwa meli kadhaa za kikosi chake ziliingia katika Atlantiki labda hata kufika Amerika. Safari hizi zilisimamishwa kwa sababu ya gharama kubwa na pia kwa sababu China haikuwa na mipango ya kuanzisha koloni katika nchi za mbali. Tofauti na mataifa ya Ulaya zilizopanua duniani karne moja baadaye Wachina hawakuona vitu wala utajiri wa kuvutia katika sehemu za mbali kwa sababu walikuwa na vitu vingi wao wenyewe.

Matatizo na mwisho wa nasaba ya Ming

hariri

Mabadiliko ya uchumi yalileta upanuzi wa miji. Mapato makubwa ya fedha kutokana na biashara ya nje yalisababisha mfumko wa bei hasa kwa mazao ya kilimo. Pesa ilibaki mjini na wenye mashamba makubwa walijenga nyumba zao mjini badala ya kurudisha pesa mashambani. Hali ya maisha ya wakulima ilishuka vibaya hasa na kusababisha ghasia za wakulima za mara kwa mara.

Ghasia hizo ziliongezeka kukaribia mapinduzi na kuingia katika hali ya kuwa vita ya wenyewe kwa wenyewe katika majimbo kadhaa.

Mwishoni vita dhidi Manchuria pamoja na ghasia ya wakulima zilileta mwisho wa nasaba ya Ming.

Kaisari wa mwisho wa Ming Chongzhen Sizong alipinduliwa na wakulima chini ya kiongozi wao Li Zicheng aliyejitangaza kuwa kaisari mpya. Lakini alikosa uwezo wa kutawala hakuwa na uwezo wa kuzuia jeshi la Wamanjuria walioingia wakisaidiwa na maafisa wa jeshi jeshi la Ming katika kaskazini waliosikitika mapinduzi.

Wamanjuria waliteka Beijing na kuwa watawala wapya wa China hadi 1911.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ming (nasaba) kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.