Zheng He
Zheng He (pia: Cheng Ho; 1371-1433) alikuwa baharia, kiongozi wa kijeshi na mpelelezi kutoka China wakati wa nasaba ya Ming. Akiwa mkuu wa jeshi la maji la China aliongoza misafara ya majahazi yake hadi pwani za Afrika hadi Msumbiji akapeleleza Bahari Hindi na visiwa vya Asia ya Kusini-Mashariki.
Maisha yake
haririZheng He alizaliwa kwa jina la Ma He katika familia ya Wachina Waislamu kwenye jimbo la Yunnan[1]. Baba yake aliwahi kusafiri Maka kwa hajj.
Alipozaliwa Yunnan ilikuwa chini ya utawala wa Wamongolia lakini mnamo mwaka 1381 jeshi la Ming lilivamia na kuteka Yunnan. Kwenye vita hiyo kijana alikamatwa kama mfungwa akafikishwa kwenye makao makuu ya Kaisari wa China. Huko alihasiwa kuwa towashi jinsi ilivyokuwa kawaida kwa watumishi wa wafalme huko China[2].
Alikuwa rafiki wa mtoto wa Kaisari akafundishwa mengi pamoja naye. Huyo alipokuwa Kaisari mwenyewe kwa jina la Yongle alimpa madaraka juu ya jeshi la maji[3] .
Safari
haririKati ya miaka 1405 na 1433 Zheng He aliongoza misafara 7 za baharini kama kiongozi wa vikundi vikubwa vya meli. Meli zake zilikuwa majahazi makubwa sana yaliyobeba hadi tani 1500. Kila safari Zheng He alipewa meli 50-60 na idadi ya wanajeshi na mabaharia ilikuwa takriban 25,000 - 30,000.
Safari tatu za kwanza zilipeleleza maeneo yanayoitwa leo Indonesia, Uhindi na Sri Lanka. Katika safari za tatu hadi saba aliendelea hadi pwani za Afrika.
Miaka 1413–1415 alisafiri mara ya kwanza Afrika ya Mashariki. Alitembelea Mogadishu na Malindi kwenye pwani ya Kenya. Sultani wa Malindi alimtuma balozi na meli za Zheng He aliyeleta twiga kama zawadi kwa Kaisari wa China. Mnyama huyo alisababisha Wachina kushangaa na kuna picha yake iliyochorwa wakati ule.
Kufika hadi Atlantiki na Amerika?
haririWataalamu kadhaa wamedai ya kwamba kwenye safari ya 1421 kundi dogo la meli zake liliingia Atlantiki na kuivuka hadi kufika Amerika. Lakini hii inapingwa na wataalamu wengi.
Hata hivyo kuna ramani ya dunia ya Mwitalia Fra Mauro ya mwaka 1459 aliyechora meli ya Kichina katika Atlantiki pamoja na maelezo ya kwamba yeye alipata habari kuhusu meli kubwa kutoka mashariki iliyoingia Atlantiki. Maelezo yale hayaeleweki kabisa kwa sababu wakati ule Wareno walikuwa hawajafika bado kusini mwa Afrika wala hawakuingia Bahari Hindi bado na Amerika haikujulikana, hivyo Fra Mauro hakuwa na majina kwa yale aliyosikia.
Zheng alikufa ama wakati wa safari yake ya mwisho au mara moja baada ya kurudi akazikwa karibu na mji wa Nanjing.
Mwisho wa safari
haririMakaisari wa baadaye walisimamisha safari. Mitindo wa Zheng He ilikuwa na gharama kubwa sana. Yote ililipiwa na serikali kuu na gharama zilipita faida ya bidhaa zilizoletwa. Tofauti na safari za Wareno na Wahispania waliofika Amerika, Afrika Mashariki na Uhindi miaka 60 baada ya Zheng He, China haikutafuta faida ya kiuchumi katika upelelezi wake na pia haikutambua nafasi za biashara katika nchi hizo za mbali.
Meli kubwa za Zheng He zilifungwa bandarini zikaoza polepole.
Marejeo
hariri- ↑ J. V. G. Mills (1970). Ying-yai Sheng-lan, The Overall Survey of the Ocean's Shores (1433), translated from the Chinese text edited by Feng Ch'eng Chun with introduction, notes and appendices by J. V. G. Mills. White Lotus Press. uk. 5. ISBN 974-8496-78-3.
- ↑ Edward L. Dreyer (2007). Zheng He: China and the Oceans in the Early Ming, 1405–1433. Longman. uk. 12. ISBN 0-321-08443-8.
- ↑ Tsai, Shih-shan Henry. "Zheng He." World Book Student. World Book, 2013. 4 December 2013.
Viungo vya nje
hariri- Ancient History Encyclopedia - The Seven Voyages of Zheng He
- Zheng He – The Chinese Muslim Admiral
- Zheng He 600th Anniversary
- BBC radio programme "Swimming Dragons".
- TIME magazine special feature on Zheng He (August 2001) Ilihifadhiwa 13 Septemba 2001 kwenye Wayback Machine.
- Virtual exhibition from elibraryhub.com
- Ship imitates ancient vessel navigated by Zheng He at peopledaily.com (25 September 2006)
- Kahn, Joseph. "China Has an Ancient Mariner to Tell You About", The New York Times.
- Newsletter, in Chinese, on academic research on the Zheng He voyages