Neema za msaada katika teolojia ya Kanisa Katoliki ni fadhili mbalimbali ambazo Roho Mtakatifu anasaidia akili na utashi wa mtu kuanza, kuendeleza na kutimiza kazi ya wokovu wake kwa kutenda mema na kuepuka mabaya. Neema kama hizo zinahitajika ili mtu aweze kutekeleza maadili na vipaji vya Roho Mtakatifu.

Msingi katika Biblia

hariri
  • Yoh 15:5 - "Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote".
  • Fil 2:13 - "Ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema".
  • 1Tim 2:4 - Mungu "hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli".

Haja ya neema za msaada

hariri

Hakuna kiumbe kinachotenda pasipo nguvu ya Mungu, aliye chanzo cha utendaji wote wa miili na wa roho: “Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu” (Mdo 17:28). Zaidi upande wa maisha yapitayo maumbile, ili tutende kwa maadili ya kumiminiwa na kwa vipaji, tunahitaji msukumo wa Kimungu unaoitwa neema ya msaada. Ni ukweli wa imani kwamba pasipo neema hiyo hatuwezi kujiandaa kuongoka, wala kudumu muda mrefu katika kutenda mema, hasa kudumu mpaka kufa katika neema inayotia utakatifu. Pasipo neema ya msaada hatuwezi hata tendo dogo linalostahili wokovu, wala zaidi kuufikia ukamilifu. Kwa hiyo Yesu alisema, “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yoh 15:5). “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu” (2Kor 3:5). “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Fil 2:13), akisukuma hiari yetu bila kuilazimisha. Ndiye anayetujalia tujiandae kupokea neema ya utakaso na halafu kustahili uzima wa milele.

Ndiyo sababu tunapaswa kusali daima. Haja ya kusali inatokana na haja ya kupata neema za msaada. Mbali na neema ya kwanza tunayojaliwa pasipo kuiomba (kwa kuwa ndiyo chanzo cha sala), sala ndiyo njia ya kawaida, ya hakika na ya jumla ambayo Mungu anataka tupate neema tunazozihitaji. Bwana ametusisitizia, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa” (Math 7:7-8). Kuna haja hiyo hasa katika kishawishi: “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Math 26:41). Tunaposali ni lazima tuamini kuwa Mungu ndiye asili ya mema yote, kwa hiyo tegemeo lolote lisilo na msingi katika sala ni la kipumbavu tu. “Mungu haagizi kamwe yasiyowezekana, bali akituagiza anatuambia tufanye tunayoyaweza, tuombe tusiyoyaweza, naye mwenyewe anatusaidia ili tuweze” (Mtaguso wa Trento), tena anatusaidia kusali pia. Kuna neema kadhaa tusizoweza kuzipata isipokuwa kwa kusali.

Haitatosha kamwe kusisitiza jambo hilo, kwa kuwa wengi mwanzoni wamejaa mawazo ya kibinadamu tu, wakidhani wanaweza kufanya lolote kwa utashi na bidii, pasipo neema za msaada. Watang'amua mapema ukweli wa maneno ya Yesu na ya Mtume Paulo, na kwamba tunapaswa kuomba ili tushike vizuri zaidi na zaidi amri za Mungu, hasa ile kuu ya upendo.

Aina za neema za msaada

hariri

Neema za msaada zina namna nyingi tofauti ambazo inafaa kuzijua, kwa kukumbushwa wazi iwezekanavyo kweli kadhaa ambazo ni za hakika, ingawa zinatokeza fumbo mojawapo la imani ambalo kuliko mengine mengi lina mchanganyiko wa mwanga na giza kwetu.

Mara nyingi tunapewa neema ya mwanga, k.mf. wakati wa masomo ya misa tunaangaziwa kwa ndani maana yake. Hiyo inafuatwa na neema ya mvuto, yaani tunavutiwa na tendo fulani, k.mf. katika kuzingatia Mwokozi anavyotupenda, tunajisikia kumrudishia upendo. Neema ya namna hiyo inatenda katika utashi na kuusukuma upendo hata tukajitoa kwa Mungu, tayari kupokea mateso yoyote na kufa kwa ajili yake. Hapo si neema ya mvuto tu, bali neema ya nguvu ambayo mara nyingi tunaipokea pasipo kuing'amua, lakini inatuwezesha kustahimili ukavu wa roho. Hata neema nyingine nyingi tunazozipokea hatuzitambui, kwa kuwa zinapita maumbile, hivyo zinapita njia zetu za kujua.

Neema ya msaada inayohusu utashi inaweza kuuathiri kwa namna mbili: kwa kuupendekezea jambo la kuuvutia, na kwa kuusukuma kwa ndani. Bila shaka Mungu anaweza kuelekeza utashi wetu kwenye uadilifu kwa kuupendekezea jambo fulani, k.mf. heri ya milele au ustawi wa upendo. Ndivyo mama anavyomvuta mtoto wake atende mema; hata malaika mlinzi anaweza kufanya hivyo kwa kututia mawazo mazuri. Lakini Mungu tu anaweza kuusukuma kwa ndani utashi wetu utende mema. Mungu yumo ndani mwetu kuliko nafsi yetu, akidumisha roho yetu, pamoja na akili na utashi alivyoviumba; ndiyo sababu anaweza kuvisukuma kwa ndani kadiri ya maelekeo ya maumbile aliyovipatia, si kwa kuvilazimisha bali kwa kuvitia nguvu mpya. Mama akitaka kumfundisha mtoto atembee anamsaidia si tu kwa kumuita, huku akimuonyesha kitu cha kukifikia, bali pia kwa mikono akimuinua. Mungu anaweza kufanya hivyo upande wa roho, akiinua utashi wetu ufikie uadilifu. Ndiye Muumba wa utashi, aliyeuelekeza ulenge uadilifu, naye peke yake anaweza kuusukuma kwa ndani kadiri ya elekeo hilo. Ndivyo anavyotenda ndani mwetu akitufanya tutake na kutenda. Atafanya hivyo kadiri tutakavyomuomba kwa ukakamavu atustawishie upendo tunaopaswa kuwa nao kwake.

Neema ya msaada inaitwa ya kutangulia ikisababisha ndani mwetu wazo au mguso mwema, kabla hatujafanya lolote kusababishia kitu hicho. Tusipoikaidi Mungu atatuongezea neema ya kuchangia itakayousaidia utashi wetu kutekeleza tendo linalohitajika ili kutimiza mpango wetu mzuri.

Mungu anatusukuma kutenda mara kufuatana na uamuzi tulioukata kwa utaratibu wa kibinadamu, mara kwa uvuvio maalumu kutoka juu, bila sisi kukata shauri kwa utaratibu huo. Mfano wa namna ya kwanza ni pale ninapoamua kusali rozari saa niliyozoea kufanya hivyo; hapo natenda kwa neema ya msaada ya kawaida inayoitwa ya kushiriki tendo kwa kuwa inashirikiana nami katika kutenda kwa kuamua kibinadamu. Mfano wa namna ya pili ni pale ambapo ghafla, wakati wa kazi nzito, najisikia kusali, nami nafanya hivyo mara: neema hiyo inaitwa ya kutenda, kwa kuwa inatenda ndani mwangu pasipo mimi kukata shauri, ingawa nakubali kwa hiari na kustahili tuzo. Kwa namna ya kwanza Mungu anatusukuma kutenda namna ya kibinadamu ya maadili. Kwa namna ya pili anatusukuma kutenda namna ipitayo utu ya vipaji vya Roho Mtakatifu; hapo chombo chetu kinakwenda si kwa kasia tu, bali kwa msukumo wa upepo: tunatendewa kuliko kutenda wenyewe, na kazi yetu hasa ni kukubali ile ya Mungu, kumuacha Roho Mtakatifu atuongoze, kufuata mara na kwa juhudi uvuvio wake wowote. Lakini hata tukiwa na neema ya kushiriki tendo tu, kila tendo linalostahili tuzo ni lote la Mungu kama asili kuu, na lote la kwetu kama asili ya pili.

Uaminifu kwa neema

hariri

Ni muhimu tuwe waaminifu kwa neema, tena waaminifu zaidi na zaidi kwa neema ya msaada ya sasa hivi, ili tutimize wajibu wa dakika hiyo unaotudhihirishia matakwa ya Mungu kwetu. Tukumbuke maneno ya Augustino, “Aliyekuumba pasipo wewe, hatakufanya mwadilifu pasipo wewe” kwa kuwa lazima ukubali na kuzitii amri. Mungu anatusaidia si kusudi tusifanye chochote, bali tutende kwa kustahili wokovu. Yeye anatutolea mfululizo neema za msaada ili tutimize wajibu wa sasa hivi, kama vile hewa inavyoyafikia mapafu yetu tuweze kupumua kila nukta. Kama tunavyotakiwa kuingiza hewa inayosafisha damu, tunatakiwa pia kupokea kwa mikono miwili neema inayozifanya mpya nguvu zetu za Kiroho ili tumuelekee Mungu. Kama vile asiyepumua anakufa, vivyo hivyo roho isiyopokea neema inakufa kwa kukosa hewa yake.

“Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1). Tunapaswa kuiitikia na kushirikiana nayo kwa bidii. Ndio ukweli mwepesi ambao tukiutekeleza siku hadi siku utatufikisha kwenye utakatifu. Kwa hakika Mungu ndiye wa kwanza kupiga hatua kwetu kwa neema ya kutangulia, halafu anatusaidia kuikubali; anatuongoza katika njia zetu zote hadi saa ya kufa. Upande wetu tunapaswa kuwa waaminifu. Namna gani? Mosi kwa kupokea kwa furaha mianga ya awali; halafu kwa kufuata kwa makini maelekezo yake; hatimaye kwa kufanya juu chini kuyatekeleza, bila kujali gharama. Hapo tutashiriki kazi ya Mungu, na utendaji wetu utakuwa tunda la neema yake na papo hapo la hiari yetu.

Neema ya kwanza inayotutia wazo jema inatosha kufanya utashi ukubali kutenda kwa uadilifu, kwa maana inatuwezesha kulitekeleza. Lakini tukikaidi wazo hilo tunajinyima neema ya msaada ambayo ingesababisha kwa hakika tulikubali. Ukaidi unaangukia neema ya kutosha kama mvua ya mawe inavyonyeshea maua yanayotarajiwa kuzaa matunda mengi: maua yakiharibika, matunda hayataundwa kamwe. Neema ya hakika inatolewa kwetu katika ile ya kutosha kama tunda katika ua; ni lazima tusiharibu ua ili tupate tunda. Tusipoikaidi neema ya kutosha tutapewa ile ya hakika na kwa njia yake tutaendelea bila wasiwasi katika njia ya wokovu. Hivyo neema ya kutosha inatuzuia tusijisingizie, na ile ya hakika haituruhusu tujivunie; kwa njia hiyo tunasonga mbele kwa unyenyekevu na juhudi.

Ndilo fumbo la neema ambalo mwanga wake umo katika kweli mbili, wakati giza lake limo katika namna ya kuzilinganisha. Upande mmoja Mungu haagizi kamwe yasiyowezekana (angekuwa hana haki wala huruma), bali kwa upendo anawezesha kweli wote watimize wajibu wao. Hakuna mtu mzima anayenyimwa neema ya lazima kwa wokovu asipoikataa kwa kukaidi mwaliko wa Mungu. Upande mwingine, “kwa kuwa upendo wa Mungu kwetu ni asili ya mema yote, hakuna mtu anayeweza kuwa mwema kuliko mwingine asipopendwa zaidi na Mungu” (Thoma wa Akwino). Kwa maana hiyo Yesu alisema kuhusu wateule, “Hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu” (Yoh 10:29). “Ikiwa baadhi wanaokolewa ni kwa zawadi ya Mwokozi: ikiwa wengine wanapotea ni kwa kosa lao” (Mtaguso wa Quiercy wa mwaka 853). Kukaidi neema ni ovu linalotokana na sisi wenyewe tu; kutoikaidi ni jema linalotokana na Mungu, chemchemi ya mema yote. Ndiyo sura mbili za fumbo lilelile; kila moja ni ya hakika, kama ile ya kwamba wote wanaweza kuokoka, na ile ya kwamba mtu akiwa bora kuliko mwenzake ni kwa sababu amependwa zaidi na Mungu. Lakini hakuna kiumbe anayeweza kuona kweli hizo mbili zinavyolingana kabla hajamuona Mungu mbinguni, kwa sababu ni sawa na kuona jinsi haki isiyo na mipaka, huruma isiyo na mipaka, na hiari yake kuu zinavyolingana katika ukuu wa Umungu.

Tusikatae ukarimu wa Mungu ambaye ametujalia neema ya maadili na vipaji, tena kila siku anatuvuta kwake. Tusiridhike na maisha ya wastani wala na kuzaa matunda yasiyoiva, wakati Mwokozi wetu mwema alisema, “Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yoh 10:10) hadi kufurahia milele heri yake. Mungu ana moyo mkuu, basi tuwe nao sisi pia.

Uaminifu huo unahitajika kwanza ili kutunza uzima wa neema, na kukwepa dhambi ya mauti. Uzima huo una thamani isiyo na kifani, hata Mwokozi alikabili kifo ili kuturudishia. Tungejaliwa kuona wazi mng'ao wa ajabu wa neema inayotia utakatifu, tungejisahau. Uaminifu unahitajika pia ili tustahili na kupata ustawi wa uzima huo, unaotakiwa kukua mpaka tutakapoingia mbinguni, kwa sababu tunapohiji kuelekea umilele tunasonga mbele kwa kukua tu katika upendo wa Mungu.

Kwa hiyo tunahitaji kutakasa matendo yetu yote, hata ya kawaida zaidi, tukiyatenda kwa nia safi na kwa lengo lipitalo maumbile. Tungekuwa waaminifu saa zote, siku zetu zingejaa na kufurika matendo ya upendo kwa Mungu na kwa jirani, katika nafasi yoyote, ya furaha na ya uchungu, na kufikia jioni muungano wetu na Mungu ungekuwa wa dhati na imara zaidi. Kwa yeyote hakuna njia rahisi na ya hakika ya kupata utakatifu kuliko ile ya kuinua kila tendo juu ya maumbile, kwa kumtolea Mungu pamoja na Yesu, kwa utukufu wake na kwa wokovu wa watu.

Marejeo

hariri
  • Catholic Answers, Grace: What it is and What it Does
  • Catholic Teaching on Sin & Grace (Center for Learning, 1997), ISBN|1-56077-521-1
  • George Hayward Joyce, The Catholic Doctrine of Grace (Newman, 1950), ASIN|B0007E488Y
  • "Grace." The Catholic Encyclopedia. Vol. 6. New York: Robert Appleton Company, 1909.
  • Stephen J. Duffy, The Graced Horizon: Nature and Grace in Modern Catholic Thought (HPAC, 1992), ISBN|0-8146-5705-2
  • Vincent Nguyen, The Pauline Theology of Grace from the Catholic Perspective, ASIN|B0006S8TUY
  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Neema za msaada kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.