Wokovu
Wokovu kwa jumla unamaanisha kuondolewa hali isiyopendeza au ya hatari kabisa.
Kwa namna ya pekee, katika Ukristo Historia ya Wokovu ni wazo la msingi: maana yake ni kwamba, katika mfululizo wa matukio ya dunia hii, Mungu anawakomboa binadamu kutoka dhambi zao na kutoka matokeo yake katika maisha ya duniani na katika uzima wa milele.
Biblia ya Kikristo inatamka kuwa neema ya Mungu ndiyo inayookoa watu, kwa kuwa hao hawawezi kujikomboa peke yao, lakini wanapokea wokovu kama zawadi (neema, dezo) kwa njia ya imani.
"Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu" (Waraka kwa Waefeso 2:8).
Wokovu katika Agano la Kale
haririKatika Biblia neno "wokovu" linatafsiri maneno mbalimbali yanayohusu kuondolewa mabaya ya kimwili na ya kiroho vilevile. Daima Mungu ndiye asili yake. Ndiye anayeokoa kwenye vita (Kutoka 15:2), ajali (Zaburi 34:6), mikono ya adui (2 Samueli 3:10), uhamisho (Zaburi 106:47), kifo (Zaburi 6:4), dhambi (Ezekieli 36:29).
Kwanza Waisraeli walifikiria hasa wokovu wa kidunia kwa taifa lao, lakini polepole kwa kuzingatia uovu, walifikia hatua ya kuona wokovu upande wa maadili na kuhusu mataifa mengine pia (Isaya 49:5,6; 55:1-5).
Kadiri yao, wokovu unapatikana kwa njia ya uadilifu uliotazamwa kama utekelezaji kamili wa Torati.
Wokovu katika Agano Jipya
haririManeno ya Kigiriki yanayotumiwa na Agano Jipya kumaanisha "kuokoa" na "wokovu" ni: σώζω (sōzō) e σωτηρία (sōtēria). Maana yake asili ni kuopoa kwa nguvu kutoka hatari (k.mf. ya ugonjwa).
Kwa kawaida Yesu alionyesha wokovu kuwa ni ukombozi kutoka dhambi ambao uanze kung'amuliwa mapema, ingawa utakamilika ahera: "Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka" (Injili ya Mathayo 10:22; 24:13).
Hasa Mtume Paulo alisisitiza wokovu ni tunda la kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, aliyeleta baraka zote kumpitia Roho Mtakatifu, kama vile wongofu, kuzaliwa upya, utakaso, kufanywa mwana, utakatifu na utukufu.
Ndiyo utatuzi wa tatizo la dhambi uliotolewa na Mungu.
Siku ya mwisho matokeo ya wokovu yatahusu ulimwengu wote ambao utajumlishwa pamoja na historia yote katika Kristo, aliye Alfa na Omega (Waraka kwa Warumi 8:21,22; Waefeso 1:10).
Wokovu katika teolojia ya Kikristo
haririKutokana na mwelekeo wa watu wa magharibi, suala la masharti ya wokovu limeshika nafasi kubwa katika teolojia kuanzia Agostino wa Hippo, wakati masuala ya kinadharia zaidi yakitawala Ukristo wa mashariki.
Ni suala hilo lililosababisha Matengenezo ya kiprotestanti katika karne ya 16 na linaendelea kujadiliwa sana katika nchi zilipokea Ukristo kutoka nchi za magharibi.
Hata hivyo katika miaka ya mwisho, Wakatoliki, Walutheri, Wamethodisti, Wakalvini na Waanglikana wamefaulu kukubaliana kuhusu suala hilo.
Wanaobaki na mitazamo ya pekee ni baadhi ya madhehebu mengine, hasa yale yanayokataa Umungu wa Yesu Kristo, kama Wamormoni.
Tanbihi
haririMarejeo
hariri- Atkin, James. The Salvation Controversy. San Diego, Calif.: Catholic Answers, 2001. ISBN 1-888992-18-2
- Jackson, Gregory Lee. Justification by Faith: Luther versus the U.O.J. [i.e. "Universal Objective Justification" Lutheran] Pietists. [Glendale, Ariz.]: Martin Chemnitz Press, 2012. ISBN 978-0-557-66008-7
- Lutheran World Federation and Roman Catholic Church. Joint Declaration on the Doctrine of Justification. English language ed. Grand Rapids, Mich.: W. B. Eerdmans Publishing Co., 2000. ISBN 978-0-8028-4774-4
Viungo vya nje
hariri- God's plan of Salvation
- Salvation- Catholic encyclopaedia
- Pohle, Joseph (1913). "Controversies on Grace". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company.
- wokovu Ilihifadhiwa 2 Julai 2019 kwenye Wayback Machine.
- Salvation Checklist Ilihifadhiwa 7 Desemba 2013 kwenye Wayback Machine. - Beliefs in Christianity for salvation
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wokovu kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |