Shahini (lat. & ing. Alshain, pia β Beta Aquilae, kifupi Beta Aql, β Aql) ni kati ya nyota angavu za kundinyota ya Ukabu (Aquila). Iko karibu na Tairi

Shahini (Beta Aquilae, Alshain)
Shahini (Alshain) katika kundinyota yake ya Ukabu (Aquila)
Kundinyota Ukabu (Aquila)
Mwangaza unaonekana 3.7[1]
Kundi la spektra G9 IV
Paralaksi (mas) 73
Umbali (miakanuru) 44.7
Mwangaza halisi +3.03
Masi M☉ 1.26
Nusukipenyo R☉ 3.28
Mng’aro L☉ 6
Jotoridi usoni wa nyota (K) 5100
Majina mbadala 7 Aquilae, NLTT 25942, LTT 4040, HD 95272, BD-17° 3273, HIP 53740, HR 4287, FK5 1283, SAO 156375.

Nyota ya Shahini ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [2]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema الشاهين ash-shahin inayomaanisha ndege wa kipanga. Jina hili walipokea kutoka kwa Waajemi ilhali Almagesti haina jina hapa ikitaja tu mahali pake “shingoni”. [3].

Kwa matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulikubali jina la Kiarabu na kuorodhesha nyota hii kwa tahajia ya "Alshain" [4].

Beta Aquilae ni jina la Bayer ikiwa ni nyota angavu ya saba katika Ukabu ingawa Beta ni herufi ya pili katika Alfabeti ya Kigiriki. Hii ni mfano jinsi gani Bayer hakufuata mwangaza kikamilifu wakati wa kugawa majina ndani ya kundinyota.

Shahini ni nyota iliyo karibu ikiwa kwa umbali wa miaka nuru takriban 45 kutoka Jua letu. Mwangaza unaoonekana ni mag 4.2. Kwa darubini inaonekana ni nyota maradufu inayozungukwa na nyota kibete chekundu αAql B.

Nyota kuu inafanana kiasi na Jua letu lakini masi yake ni kubwa kwa kiwango cha robo moja. Haionyeshi dalili za kuwa na sayari. Mng'aro wake ni mara sita wa Jua na hii inachukuliwa kama dalili ya kwamba imeshamaliza kumemenyusha heliamu katika kiini chake ikielekea kulipuka na kuwa jitu jekundu.

Msindikizaji wake ni ndogo ina theluthi moja ya masi ya Jua pekee na mwangaza unaonekana wa mag 11.4.

Tanbihi

hariri
  1. Vipimo kufuatana na Bruntt, H.; et al. (July 2010)
  2. ling. Knappert 1993
  3. Allen, Star-Names (1899), uk. 60 na Tooner, Almagest (1984), uk 350 “
  4. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017

Viungo vya Nje

hariri


Marejeo

hariri
  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 437 (online kwenye archive.org)
  • Bruntt, H.; et al. (July 2010), "Accurate fundamental parameters for 23 bright solar-type stars", Monthly Notices of the Royal Astronomical Society, 405 (3): 1907–1923 online hapa
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Ptolemy's Almagest, translated and annotated by G.J. Toomer, London 1984, ISBN 0-7156-1588-2 online hapa