Kwa maana mengine ya jina hili angalia hapa Tanga

Nyota za kundinyota Tanga (Vela) katika sehemu lao ya angani

Tanga (kwa Kilatini na Kiingereza Vela) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu. Lipo jirani na kundinyota la Mkuku (Carina) na si mbali na Salibu (Crux).

Jina

Hadi karne 19 kundinyota hili lilitazamiwa kuwa sehemu ya kundinyota kubwa zaidi lililoitwa Argo Navis, mara nyingi pekee "Navis" (yaani merikebu) iliyokuwa moja ya makundinyota 48 yaliyoorodheshwa na Klaudio Ptolemaio. Lacaille alihesabu ndani yake nyota 180 na hivyo alianza tayari kugawa Argo Navis kwa sehemu tatu za Mkuku (Carina), Shetri (Puppis) na Tanga (Vela). Hii ilithibitishwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia katika orodha ya kundinyota 88 za kisasa iliyotolewa mwaka 1930. [2]

“Vela” inataja matanga ya merikebu. Katika Vela hakuna nyota zinazoitwa Alfa au Beta kwa sababu majina haya yaligawiwa kati ya nyota ya Argo Navis yote kufuatana na uangavu.

Nyota

Nyota ng'avu zaidi ni Gamma Velorum ambayo inaonekana kama nyota yenye uangavu wa 1.83 mag. Hali halisi hii ni mfumo wa nyota mbalimbali zinazoonekana kwa macho kama nyota 1 lakini ziko tofauti katika darubini.

γ Gamma na λ Lambda Velorum ziliitwa "Suhail" na Waarabu - hili ni jina lilelile kama Suheli (Canopus) katika kundinyota la Mkuku (Carina). Sababu yake ni ya kwamba Waarabu walitumia jina hili kwa nyota tatu katika kundinyota la Argos iliyovunjika baadaye. Kwa Lambda Vel pekee UKIA uliamua kutumia jina hili rasmi, lakini Knappert alipata jina hili kati ya mabaharia Waswahili kwa ajili ya nyota angavu zaidi.


Jina la
Bayer
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
γ Suheli (γ Vel) 1.8 1000 B1 IV
δ Alsephina 1.93 80 A1 V
λ Suhail 2.14 hadi 2.30 573 K4 Ib-II
κ Markeb 2.47 540 B2 IV-V
μ 2.69 116 G5 III SB + G2 V

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya "Vela" katika lugha ya Kilatini (ambayo ni uwingi wa Velum) ni "Velorum" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Gamma Velorum, nk.
  2. "The IAU list of the 88 constellations and their abbreviations" ya mwaka 1922, iliangaliwa Mei 2017