Umememaji

umeme unaozalishwa kwa njia ya maji

Umememaji ni umeme unaozalishwa kwa kutumia mwendo wa maji.

Lambo la majiumeme

Kwa kawaida mwendo asilia wa maji huzuiliwa kwa kujenga lambo. Maji hufuata mvutano wa graviti yanataka kuteremka chini zaidi kila mahali yalipo kama kuna njia.

Ukuta wa lambo huzuia mwendo wa mto. Kama nafasi ndogo inafunguliwa maji yanateremka mle kwa nguvu nyingi. Mwendo huu wa maji hupitishwa kwenye rafadha au parapela inayozungushwa. Mwendo wa rafadha unaendelea kuzungusha jenereta ya kutoa umeme.

Umememaji huwa na faida mbalimbali: gharama yake si kubwa, kiwango cha uzalishaji umeme unaweza kubadilishwa haraka bila matatizo kulingana na mabadiliko ya mahitaji kwa mfano baina ya mchana na usiku. Kama mahitaji ya umeme ni madogo maji hupitishwa kando la rafadha. Uzalishaji huu hauchafushi mazingira maana hakuna kuchoma kwa fueli.

Kwa hiyo umememaji ni nishati mbadala inayotumiwa zaidi duniani.

Njia ya pekee ya kuzalisha umememaji ni kutumia bwawa la juu linalojazwa kwa pampu. Mbinu hii inatumia umeme uliopatikana wakati watumiaji wana matumizi madogo. Umeme uliopo sasa kwa ziada huendesha pampu kubwa na kusukuma maji kutoka sehemu ya chini kwenda bwawa lililoandaliwa juu zaidi kwa mfano juu ya mlima. Wakati wa mahitaji makubwa maji haya yanateremshwa kupitia rafadha na kuzalisha umeme.