Graviti
Graviti (kutoka Kiingereza: "gravity"; pia: kani ya mvutano, kanimvutano, nguvu ya uvutano, nguvu mvutano) ni kani ya uvutano iliyopo kati ya magimba yote ya ulimwengu. Kila gimba lenye masi linavuta magimba mengine yote yenye masi.


Ndiyo sababu watu wanatembea ardhini ilhali hawawezi kuelea hewani: kwa sababu masi ya Dunia inawavuta kuelekea kiini chake. Inavuta kila kitu chenye masi kuelekea kiini chake. Na sisi watu tunaivuta Dunia, lakini kani hiyo ni ndogo mno kulingana na masi kubwa ya Dunia. Dunia yetu imeshikwa na mvuto mkali wa graviti ya Jua na ndiyo sababu ya Dunia kubaki karibu na Jua katika obiti na haiwezi kwenda mbali na Jua.
Graviti ni kani isiyo na kikomo lakini athira yake inapungua kadiri magimba yalivyo mbali. Inasababisha mata ya anga-nje kupangwa kwa nyota, mawingu, galaksi na makundi ya galaksi.
Isaac Newton anajulikana kama mtaalamu aliyeweza kueleza graviti kwa mara ya kwanza kama utaratibu wa msingi wa sayansi.
Mifano ya athira ya graviti
Jiwe likitupwa hewani, litaanguka chini. Hii ni kwa sababu, ingawa kani ya mkono ilipeleka jiwe kwenda juu, kani ya graviti ya Dunia inapunguza kasi ya jiwe na hatimaye inalirudisha ardhini.
Tabia ya kuvutana inaonekana vyema kati ya Dunia na Mwezi. Dunia ni kubwa, inauvuta Mwezi na kuushika kwenye njia yake ya kuzunguka Dunia. Lakini wakati huohuo Mwezi unavuta pia Dunia na hii inaonekana baharini katika mabadiliko ya maji kupwa na maji kujaa kila siku. Maji ya bahari huvutwa na Mwezi kiasi kwamba kwenye sehemu ya Dunia inayotazama Mwezi, maji ya bahari yaliyo moja kwa moja chini ya Mwezi huinuliwa kiasi cha nusu mita juu ya wastani wa usawa wa bahari yote.
Makala hii kuhusu mambo ya fizikia bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Graviti kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |