Uthman ibn Affan kar.: عثمان بن عفان‎,‎ (* 574 mjini Makka - + 17 Julai 656 Madina) alikuwa khalifa wa tatu wa Uislamu aliyemfuata Umar ibn al-Khattab.

Ukoo wa Banu Umayya

hariri

Alizaliwa Makka katika familia tajiri ya koo la Banu Umayya بنو أمية katika kabila la Wakuraish. Biashara ya vitambaa ilimletea utajiri kabla hajajiunga na Uislamu. Alioa mabinti wawili wa Muhammad.

Uenezaji wa eneo la Uislamu

hariri

Uenezaji wa Uislamu uliendelea chini yake kwa kuvamia Libya ya leo na maeneo ya Uajemi wa mashariki. Alipanga utawala upya akiteua magavana kwa maeneo mapya badala ya viongozi wa jeshi tu waliowahi kutwaa sehemu zile. Alipendelea ndugu zake wa Banu Umayya hali iliyosababisha upinzani dhidi yake kwa sababu ya ugawaji wa mapato ya vita mbalimbali. Alishtakiwa pia kujitajirisha kutokana na mapato ya umma na kuwazawadisha ndugu zake.

Alimfanya binamu yake Muawiya aliyekuwa baadaye khalifa wa tano kuwa gavana wa Shamu mjini Dameski.

Kukusanya Kurani

hariri

Uthman akumbukwa hasa kwa kazi ya kukamilisha Kurani kama maandiko. Kufuatana na mapokeo ya Kiislamu Muhammad alikuwa alitangaza sura za Kurani zilizoshikwa na wasikilizaji na wengine waliandika walichosikia.

Wakati wa Uthman tofauti zilionekana kuhusu mapokeo ya sura mbalimbali kati ya maeneo mbalimbali. Madina, Dameski au Kufa zilianza kuonyesha mapokeo tofauti. Uthman aliunda kamati iliyoongozwa na Zaid ibn Thabit iliyopewa kazi ya kukusanya maandiko yote yenye sura au maneno ya Kurani na kuyachungulia. Kamati iliamua ni yapi yaliyofaa na kutengeneza hivyo nakala kamili ya Kurani mara ya kwanza.

Baadaye Uthman alituma nakala zake kote katika miji ya Waislamu akaamuru nakala za awali ziangamizwe.

Ieleweke ya kwamba maelezo haya hayakubaliwi na wataalamu wote; wengine walio nje ya nchi za Uislamu wanafundisha ya kuwa Kurani ilikamilika baada ya makhalifa wa kwanza.

Mwisho wake

hariri

Upendeleo wa ndugu zake ulisababisha chuki dhidi ya Uthman. Wapinzani walianza kukutana mbele ya nyumba yake waliodai ajiuzulu. Ugomvi uliongezeka mwishowe wapinzani walivunja nyumba ya khalifa wakamwua tar. 17 Julai 656.

Baada ya kifo chake Ali ibn Abi Talib akachaguliwa khalifa wa nne. Lakini uchaguzi huu haukutambuliwa na binamu yake Uthman Muawiya hasa kwa sababu ndugu za Ali walishtakiwa kuwa walishirikii katika mauaji ya Uthman.