Ahmad Nassir Juma Bhalo (Kuze, Mombasa, 26 Mei 1936 - 9 Januari 2019) alikuwa malenga Mswahili wa Mombasa. Kwa upande wa babake alikuwa Mtangana na kwa mamake alikuwa Mkilindini. Haya ni miongoni mwa makabila ya asili ya Kiswahili Cha Kimvita, yaani Mombasa.

Kama watoto wengine wa Mombasa wa wakati huo aliingia chuoni kusoma Qurani na dini ya kiislamu. Mafunzo hayo aliyapata kwa babu yake Sheikh Muhammad Ahmad Matano, mpaka alipohitimu.

Baada ya mafunzo hayo, alikwenda shule ya kizungu kwa wakati huo ikijulikana kama Arab Boys (Serani Primary School) hapo hapo Mombasa,Kwa bahati mbaya hakumaliza masomo yake na aliwata (aliwacha) akiwa darasa la nne, na akaanza kufanya kazi.

Bwana huyu alikuwa mshairi mashuhuri katika uwanda (uwanja) wa mashairi, alijulikana sana kwa jina la Ustadh Bhalo. Bhalo ni lakabu ya babu yake mzaa baba yaani Juma Bhalo; na Ustadh ni cheo alichopewa na mhariri wa gazeti moja la Mombasa lilokuwa likiitwa Sauti ya Pwani, baada ya kupata diploma yake ya ushairi.

Utunzi wa mashairi hariri

Lugha aliyotumia Ahmad Nassir kutungia mashairi yake ni ile ya ki-Mvita , tena cha ndani. Kwa sababu hii, si rahisi kwa mtu mwenye ujuzi mdogo wa lugha ya Kiswahili kuyaelewa mashairi yake bila ya msaada.

Mtu yeyote anayesoma mashairi yake akaona jinsi alivyoichezea lugha ataelewa alikwasika na kuwa bingwa kweli katika mashairi mengi aliyotunga.

Baadhi ya mashairi hayo yamechapishwa na mengine bado. Kati ya mashairi yake pia yameimbwa na Mohamed Khamis Juma Bhalo al maaruf Professor Juma Bhalo katika nyimbo za taarabu, wawili hawa ni mtu na bin ammi yake.

Mashairi yake ya kwanza kuchapishwa ni yale yaliyomo katika kitabu kiitwacho Poems from Kenya kilichopigwa chapa na The university of Wisconsin Press ya Amerika katika mwaka wa 1966.

Mashairi hayo yalifasiriwa kwa kiingereza na kuhaririwa na mwena zake Profesa Lyndon harries wa chuo kikuu cha Wisconsin.

Kitabu cha pili cha mashairi yake ni kile kiitwacho Malenga wa Mvita, hiki kimehaririwa na al marhum Shihabuddin Chiraghdin na kupigwa chapa na Oxford University Press, humuhumu Kenya.

Kitabu hicho ndicho kilichopokeya Tuzo ya Kenyatta ya fasihi ya Kiswahili ya 1972 kuwa ni kitabu kizuri kuliko vyote vya Kiswahili vilivyotolewa mwaka huo. Vitabu vyake vyengine vilivyofwata baada ya Malenga wa Mvita ni; Taa ya umalenga pamoja na Irshad.

Kuhusu mashairi yake ambayo hayajachapishwa ni mengi sana.

Mbali na mashairi aliyonayo mwenyewe yako mengine kadha wa kadha yaliyo kwenye maktaba ya vyuo vikuu mbali mbali ulimwenguni kama Ujerumani, Dar es Salaam, London na hata Urusi.

Mbali na ubingwa wa mashairi pia alikuwa na kipawa cha uchoraji. Miongoni mwa kazi zake za uchoraji ni zile zilizokuwa katika vifua za baadhi ya fulana za nyakati hizo za nyuma, kama zile za Cruel world, Cruel hand, Please kiss me na Make love not war .

  Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ahmad Nassir kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.