Barua ya kujiuzulu ualimu ya Julius Kambarage Nyerere

Barua ya kujiuzulu ualimu ya Julius Kambarage Nyerere ilikuwa barua ya kuacha kazi ya ualimu katika shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, Dar es Salaam.

Barua ya Nyerere kujiuzuru ualimu.

Mchakato wake na sababu zilizopelekea kujiuzulu hariri

Hotuba aliyotoa Nyerere pale Mnazi Mmoja ambapo aliwaeleza watu kuhusu safari yake kwenda Umoja wa Mataifa ilikuwa ndiyo mwanzo hasa wa historia mpya ya Tanganyika. Kabla ya hapo Waafrika wa Tanganyika hawakupata kuonyesha shauku na matumaini katika mustakabali wao. Katika viwanja vya Mnazi Mmoja Nyerere aliwaeleza halaiki ya watu wenye furaha na waliokuwa wakimsikiliza kwa makini kuwa miongoni mwa mataifa kumi na mbili yanayounda Baraza la Udhamini saba kati yao yalitoa idhini kuwa muda wa utawala wa ndani wa Tanganyika utakapowadia, Waafrika lazima wapewe nchi yao.

Katika hotuba yake Nyerere alitilia mkazo sera ya TANU kuhusu mahusiano mema baina ya Waafrika na watu wa mataifa mengine na aliwaonya wanachama wa TANU ambao walikuwa wameanza kuwabagua watu wa rangi tofauti kuwaambia kuwa hivyo haikuwa sawa. Alisisitiza juu ya umoja miongoni mwa wananachi na hatimaye aliwadhihaki wasikilizaji kwa kuwauliza ikiwa wangesubiri kwa miaka ishirini na tano kuwa huru. Halaiki hiyo ya watu kwa pamoja ilipiga kelele, "hapana". Wananachi kwa pamoja walijibu kwa sauti kubwa wakisema walitaka uhuru kesho au kesho kutwa.

Cheche za TANU na mshtuko kwa Padri Walsh hariri

 
Julius Nyerere akiwa UNO mwaka 1955.

Nyerere ambaye alikuwa akiogopa kuchukua uongozi wa TANU tangu 1953 alikuwa amefarajika sana na mshikamano huu ulioonyeshwa na wananchi. Sasa ilikuwa dhahiri kwake kwamba rafiki yake Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz, John Rupia na uongozi mzima wa TANU pamoja na lile Baraza la Wazee lilikuwa limemsafishia njia kuongoza harakati kwa niaba yao. Lakini Padri Walsh na Wamisionari katika shule ya Mtakatifu Francis, Pugu, walitazama harakati hizi kwa mtazamo mwingine kabisa. Wamishionari hawakuweza tena kumvumilia Nyerere kuwa mmoja wa walimu katika shule yao. Hatima ile ile iliyowasibu wazalendo wengine kabla yake sasa ilimkabili Nyerere. Aliambiwa ama abakie mtumishi mtiifu wa kanisa au ajiuzulu; Kanisa halikuweza kukaa kimya na kumuangalia Nyerere akiwatumikia mabwana wawili.

Nyerere alilipeleka tatizo hili kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU. Mtamila aliitisha mkutano wa kamati kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo. Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na Rupia na Kambona walikuwa Bibi Titi Mohamed na Bibi Tatu bint Mzee. Kamati Kuu ya TANU ilimshauri Nyerere ajiuzulu. Tafarani hii ilitokea wiki chache tu baada ya kurudi kutoka Umoja wa Mataifa katika wiki za mwisho za mwezi Machi. Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere alijiuzulu ualimu. Ilikuwa adhuhuri Nyerere alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si mwalimu wa shule tena. Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Abdulwahid katika soko la Kariakoo kumpasha habari rafiki yake. Nyerere alikaa na Abdulwahid katika nyumba yake namba 78 Mtaa wa Stanley. Baadaye kidogo Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma. John Hatch alipokuja Dar es Salaam kwa mwaliko wa TANU Nyerere alikuwa kwao kijijini. Utaona hapo baadaye kidogo jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha Schneider Abdillah Plantan kuhusu TANU kuwashirikisha wanawake katika harakati za kudai uhuru.

Hapa ndipo Nyerere alipoifikisha TANU katika uingozi wake wa miezi minane na hali ilianza moto Tanganyika nzima kiasi ya kuwa Nyerere hakuweza tena kuwatumikia mabwana wawili. Hii ndiyo iliyopelekea yeye kuandika barua ya kujiuzulu kazi ya ualimu.

Tafsiri ya barua ya Mwalimu Nyerere kwa Kiswahili hariri

S. Francis College, Pugu, 22 Machi, 1955.

Mwalimu Mkuu, St. Francis College Pugu.

Mpendwa Padri,

Nimelifikiria chaguo ulilonipa, kati ya kazi yangu shuleni na uanachama wangu katika T.A.N.U na nimefikia uamuzi kwamba lazima nijiuzulu katika nafasi yangu shuleni.

Lakini sasa najikuta nimekabiliwa na chaguo kama hilo. Kwa vile TANU inaingiliana na kazi yangu shuleni, suala hilo ni la kibinafsi na hivi karibuni au baadaye nitalazimika kupunguza shughuli zangu katika TANU au kuchagua kati ya TANU na shule. Katika hali hiyo chaguo lingekuwa la kweli; na kama ningegundua kwamba nisingeweza kuyafanya mambo yote hayo mawili kikamilifu ni dhahiri kwamba ningeiacha shule na kwenda kushughulika na TANU. Lakini iwapo kujiuzulu kutoka TANU kutanifanya niendelee na kazi yangu, suala hilo linakuwa ni la uamuzi wa kikanuni. Ni nani nchini Tanganyika yuko huru kujiunga na kuiongoza TANU? Kinadharia ni watu wote wasiokuwa waajiriwa wa serikali. Katika hali halisi nafahamu kwamba waajiriwa wa serikali za mitaa hawako huru, au ni kwamba hawana uhuru kuliko walimu wa mamlaka za kidini. Na kama uhuru wa walimu hao wa kidini utatiliwa mashaka, hali ingekuwa ya mashaka kwani sioni sababu yoyote kwa nini kila mwajiri asitoe masharti kama hayo kwa waajiriwa wake; na uwezekano huo ungekuwa wa kusikitisha. Kwa hiyo, ni lazima nijiuzulu kama njia ya kupinga hali hiyo.

Ninasikitika kwamba shughuli zangu katika TANU ni dhahiri zimeathiri utendaji wangu wa kufundisha; ninasikitika kuhusu matatizo ambayo yatajitokeza kwako na kwa wenzangu kwa muda kutokana na kujiuzulu kwangu; ninasikitika pia kwa matokeo ya kiuchumi ambayo yataikumba familia yangu.

Ningekuwa katika nafasi yako, Padri, ningefanya kama ulivyofanya wewe; tumaini langu pekee ni kwamba utaona inawezekana kwamba ungekuwa katika nafasi niliyo nayo mimi ungechukua hatua kama ambayo nimeichukua.

Nakushukuru wewe na Mapadri wengine kutokana na kushirikiana nami siku zote. Nitazihitaji sala zenu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo nyuma. Endelea, Padri, kuniombea.

Mwanao mpendwa katika Kristo,

Julius Nyerere.

Tazama pia hariri

Viungo vya Nje hariri