Barua ni ujumbe wa kimaandishi unaotumwa kwa mtu mwingine au watu wengine. Inawezekana kumwachia mtu ujumbe wa kimaandishi yaani barua mahali fulani lakini mara nyingi barua inatumwa kwa njia ya mtume au shirika linalofanya kazi hii kibiashara.

José Olaya (17891823), shujaa wa uhuru wa Peru, alisafirisha barua kwa wapiganaji wa uhuru katika vita dhidi ya Hispania.

Kwa kawaida siku hizi barua inaandikwa kwenye karatasi ama kwa kalamu ama kwa taipureta ama kwa kutumia kompyuta na printa. Karatasi ya barua hukunjwa na kuwekwa ndani ya bahasha yenye jina na anwani ya mpokeaji juu yake. Siku hizi idadi kubwa ya ujumbe inaandikwa kwa njia ya baruapepe.

Neno barua

hariri

Neno barua linatokana na Kiarabu cha Omani ٻروۑ barwe [1].

Neno lingine, pia lenye asili ya Kiarabu, ni waraka [2], linatumiwa zaidi kwa ujumbe wa maandishi maalumu, si barua ya kawaida.

Barua katika historia

hariri
 
Barua kutoka Mesopotamia, iliandikwa kwa mwandiko wa kikabari, mnamo 1300 KK.

Barua za kale kabisa zinazojulikana zimehifadhiwa kutoka Mesopotamia ya Kale ambako watu waliandika juu ya vigae vya mwandiko wa kikabari kwa kutumia mwandiko wa kikabari. Labda kulikuwa na barua za kale zaidi lakini hazikuhifadhiwa hadi leo.

Wamisri wa kale walituma barua zilizoandikwa juu ya papiri, Wagiriki na Waroma wa Kale waliandika ujumbe juu ya bapa za ubao zilizofunikwa kwa ganda la nta. Baadaye barua muhimu ziliandikwa juu ya vipande vya ngozi nyembamba vilivyoandaliwa kwa kusudi hii.

Watu wa kwanza wa kutumia karatasi walikuwa Wachina wa Kale, baadaye teknolojia ikasambaa duniani.

Katika dunia ya kale barua zilisafirishwa na watu waliotumwa moja kwa moja na mwandishi mwenyewe.

Katika falme kubwa, kama vile Uajemi ya Kale, China ya Kale, Misri ya Kale au Dola la Roma, kulikuwa na mfumo wa watarishi wa serikali waliobeba barua rasmi kati ya ofisi ya mfalme na sehemu mbalimbali za ufalme, lakini hii ilikuwa kwa ujumbe rasmi hasa. Watu wengine walihitaji kutumia huduma za wasafiri kama wafayabiashara na misafara yao.

Mara nyingi kulikuwa na vituo vya pekee kila baada ya kilomita kadhaa ambako watarishi walisubiri kufika kwa barua pamoja na farasi waliotunzwa katika vituo hivyo. Kwa njia hii Waroma waliweza kusafirisha ujumbe takriban kilomita 80 kila siku, yaani ilichukua takriban siku 60 kupeleka barua kutoka Roma hadi Misri kwa njia nchi kavu (kilomita 3,200). Kama hali ya hewa iliruhusu, usafiri kwa jahazi muda huo uliweza kufupishwa kiasi.

Katika miaka 400 iliyopita makampuni ya binafsi na za serikali zimepanua huduma za kusafirisha na kufikisha barua. Kama ni taasisi ya serikali kwa kawaida huitwa posta.

Kuhusu gharama, kuna mbinu mbiliː ama mpokeaji analipa gharama za usafirishaji wakati wa kupokea barua, au mwenye kutuma barua analipa gharama wakati wa kutuma. Nchi nyingi huwa na mfumo ambako mwenye kutuma ananunua stempu kwa gharama ya usafirishaji; stempu hizo ni vipande vya karatasi vyenye thamani maalumu ambavyo vinabandikwa kwa gundi kwenye bahasha na kugongwa mhuri ili zisitumiwe tena.

Umbo la barua

hariri

Katika historia ndefu ya matumizi ya barua ilitokea kawaida namna ya kutunga na kuandika barua. Bahasha au sehemu ya nje ya barua huwa na majina ya mpokeaji na pia ya mwandishi pamoja na anwani zao. Barua yenyewe huwa na habari kuhusu tarehe na mahali pa kuandikwa, jina au sahihi la mwandishi, jina la mwandikiwa.

Barua zinatofautiana kama ni barua za binafsi ndani ya familia, kati ya marafiki au wapenzi, kati ya wafanyabiashara au wateja na wauzaji, kati ya ofisi na raia na kadhalika.

Muundo wa barua ya kirafiki umegawanyika katika sehemu sita ambazo ni: Anwani ya mwandishi, Tarehe, Mwanzo wa barua, Kiini cha barua, Mwisho wa barua na Jina la mwandishi.

Barua na jamii

hariri

Barua ni chombo muhimu katika utamaduni wa kila jamii. Zinategemea kuwepo kwa watu wanaojua kusoma na kuandika. Si lazima ya kwamba kila mtu anayetuma barua au kuipokea anajua kuandika au kusoma, maana inawezekana kutumia msaada wa watu wengine. Lakini mawasiliano kwa barua ni uhamasisho mkubwa kwa watu kujifunza na kuboresha elimu hiyo.

Marejeo

hariri
  1. Tazama Sacleux, Dictionnaire Français—Swahili, "barua", anayerejea neno kwa lahaja ya Kiarabu cha Omani
  2. kutoka kar. ورق "karatasi"