Kazi ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu, hivyo ina nafasi kubwa katika anthropolojia, falsafa, teolojia,fizikia na sosholojia.

Wachimbaji wa mfereji wa maji kwenye mto Cedar, Washington (1899).
Wanawake wengi pamoja katika kazi ya ofisini.
Mwanafalsafa kazini alivyoonyeshwa na sanamu ya August Rodin, "Le penseur" (= "Mwenye kufikiri").
Mfanyakazi akishughulikia mashine (picha ya Lewis Hine, 1920).

Inafafanuliwa kama utendaji unatumia nguvu ya akili au ya mwili ili kufikia lengo fulani, ambalo mara nyingi ni faida ya kiuchumi ili kuweza na kuwezesha kuendelea kuishi.

Lakini thamani yake halisi haiishii katika uzalishaji wa vitu, bali inategemea hasa ustawishaji wa utu katika vipawa vyake vyote kulingana na maadili na maisha ya kiroho.

Kwa msingi huo, ni wajibu wa kila mtu aliyefikia ukomavu fulani.

Ni pia mchango muhimu katika jamii na inayostahili kuheshimiwa na kutunzwa na wote kuanzia serikali hadi watu binafsi.

Kwa kuwa ni wajibu, kazi ni vilevile haki ya msingi ya binadamu. Bila kuwa nayo, mtu anaelekea kunyong'onyea na kujiona hama maana, hasa kama utovu wa kazi unadumu muda mrefu na kumzuia asiweze kupanga maisha yake, kwa mfano upande wa ndoa na familia, kwa sababu ya kutojitegemea.

Sheria mbalimbali zinaratibu mahusiano kazini, hasa kama kuna mwajiri na mwajiriwa.

Kazi katika Biblia

Biblia inazungumzia maisha halisi ya watu, hivyo haikuweza kuisahau kazi. Toka kitabu cha Mwanzo (1:1-2:4a) inaonyesha heshima ya kufanya kazi kwa kumchora Mungu akitenda kazi kama binadamu kwa siku sita, akipumzika ile ya saba.

Ndiye aliyewaagiza Adamu na Eva wafanye kazi katika dunia ili kuistawisha (Mwa 2:15).

Baada ya dhambi ya asili waliyoifanya wajibu huo umebaki, ila kama adhabu sasa unachosha (Mwa 3:17-19).

Pamoja na hayo, Yesu alikubali kufanya kazi kwa mikono yake kama fundi (labda seremala) kwa sehemu kubwa kabisa ya maisha yake, alipoishi na familia yake au walau mama yake kijijini Nazareti (Mk 6:3).

Mtume Paulo alipinga kwa nguvu uzembe wa waliodai kazi haihitajiki tena kwa sababu eti, ufalme wa Mungu umefika. Aliandika, "Asiyetaka kufanya kazi, asile chakula" (2Thes 3:10). [1] Mwenyewe, pamoja na kuhubiri Injili alikuwa akiendelea na kazi yake ya kushona mahema ili kupata mahitaji yake bila kulemea wengine.

Marejeo

  1. "Aya kuhusu kazi".

Viungo vya nje

  • [1] Tovuti rasmi ya International Labour Organization
  • [2] Ushauri kuhusu kazi toka Unesco
  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kazi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.