Chipsi kuku ni mlo maarufu wa hotelini. Chakula cha chipsi kuku kimekuwa mashuhuri, ingawa vipo vingi kama mbatata za urojo, badia, kachori na chatne (Zanzibar mix au viazi vya karai).

Chipsi na kuku wenye pilipili

Neno maakuli linatokana na chimbuko la Kiarabu likimaanisha mlo rasmi au maalum. Utamaduni wa Waswahili ambao hupatikana Afrika mashariki kwenye masuala ya maakuli, umemezwa na vibanda vya chipsi kuku katika mitaa mingi ya Uswahilini.

Biashara ya chipsi kuku imepanda chati, kwani inavutia wengi hasa kwenye michapuzo ya nguvu ambayo hukolezwa kwenye kilaji hicho cha chipsi kuku kama tomato sosi, chili sosi, rojo zitozito la embe bichi au ukwaju na pilipili juu yake. Watafutaji ajira hamkani katika harakati za kuwaridhisha wateja wao, na wateja nao wake kwa waume humiminika kujipatia huduma hiyo, Alhamdulilah tumbo halilali na njaa.

Mandhari ya biashara hizi hutofautiana kutokana na vipato vya watafutaji ajira, kuna sehemu ambazo utastarehe na kiyoyozi juu yake, lakini sehemu nyingine kutokana na mazingira yake, fumba macho tu kama una njaa au Waswahili wanasema ‘usimchungue kuku atakushinda kumla'.

Lakini mafuta yanayochomewa chipsi kuku mwenye karai au fraya, yakipelekwa kwa mkemia mkuu atasema nini? Faida ni kushiba lakini hasara hatuifahamu na ni lazima tujiulize.

Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Chipsi kuku kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.