Chonga
Chonga-mnazi (Oryctes monoceros)
Chonga-mnazi (Oryctes monoceros)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Polyphaga
Familia ya juu: Scarabaeoidea (Wadudu kama bungo-mavi)
Familia: Scarabaeidae (Wadudu walio na mnasaba na bungo-mavi)
Nusufamilia: Dynastinae
MacLeay, 1819
Ngazi za chini

Kabila 7:

Chonga ni mbawakawa wa nusufamilia Dynastinae ya familia Scarabaeidae katika oda Coleoptera ambao madume yao wana pembe kubwa kichwani na mara nyingi pia kwenye mbele ya pronoto (kidari). Kwa sababu ya hii huitwa “bungo-kifaru” (rhinoceros beetles) kwa Kiingereza.

Zaidi ya jenasi 225 na spishi 1500 za chonga hujulikana. Spishi kadhaa ni miongoni mwa mbawakawa wakubwa kabisa duniani.

Maelezo

hariri
 
Chonga wa Ulaya: hatua tatu kutoka buu hadi mpevu:
buu (nyuma), bundo (kati), mpevu (mbele)

Chonga wanaweza kuwa wakubwa sana na kufikia zaidi ya sm 15, lakini hawana madhara kabisa kwa wanadamu kwa sababu hawawezi kung'ata au kudunga. Spishi fulani zimedaiwa katika hekaya kuinua mizigo hadi mara 850 ya uzito wao wenyewe. Madume wana pembe juu ya kichwa na kwa kawaida pembe nyingine inayoelekeza mbele kutoka katikati ya toraksi. Pembe hutumiwa katika kupigana na madume wengine wakati wa msimu wa kupandana na kwa kuchimba. Ukubwa wa pembe ni kiashirio kizuri cha lishe na afya ya mwili.

Mwili wa chonga mpevu umefunikwa na kiunzi nje kinene. Jozi ya mabawa mazito ya mbele lipo juu ya jozi ya mabawa ya nyuma kama viwambo, inayoruhusu chonga kuruka juu, ingawa sio vizuri sana kwa sababu ya saizi yake kubwa. Ulinzi wao bora kutoka kwa mbuai ni saizi na tambo yao. Zaidi ya hiyo, kwa kuwa hukiakia wakati wa usiku, wanaepuka mbuai wao wengi wakati wa mchana. Ikiwa jua limekucha, hujificha chini ya magogo au katika uoto ili kujificha kutoka kwa mbuai wachache walio wakubwa wa kutosha ili kutaka kuwala. Chonga wakisumbuliwa wengine wanaweza kutoa sauti kubwa kama sss. Sauti hizo hutengenezwa kwa kusugua fumbatio yao dhidi ya mwisho wa vifuniko vyao vya mabawa. Chonga huwa sugu kiasi: dume mpevu mzima anaweza kuishi hadi miaka 2-3. Majike huishi kwa kawaida muda mfupi baada ya kupandana.

Hatua za mabuu za mbawakawa hao zinaweza kudumu miaka kadhaa. Mabuu hula ubao uliooza na mpevu hula mbochi, utomvu wa mimea na matunda. Kwanza mabuu hutoka kwenye mayai na baadaye hukua kuwa bundo kabla ya kufikia hatua ya mpevu (angalia picha kushoto). Majike hutaga mayai 50 kwa wastani. Kinyume na kile saizi yao inaweza kumaanisha, chonga wapevu hawali mingi sana, tofauti na mabuu yao ambayo hula kiasi kikubwa cha ubao unaooza.

Madume wanapigana kutawala maeneo yao. Wanatumia pembe zao kuwatoa madume wanaopingana kutoka eneo, ambayo huwapa nafasi ya kupandana na majike. Madume wakubwa wenye pembe kubwa hupanda mara nyingi, kwani hushinda mashindano mengi. Madume wadogo mara nyingi huepuka madume wakubwa na huonyesha mikakati mingine ya kupata majike.

Chonga na binadamu

hariri

Kama chakula

hariri

Katika sehemu za Afrika mabuu ya chonga ni maarufu kama chakula. Imedokezwa kuwa mabuu yana protini nyingi zaidi (40%) kuliko nyama ya kuku (20%) na ya ng'ombe (takriban 18%), ambayo inamaanisha kama ni chanzo muhimu cha protini kwa watu wanaowakula.

Kama wanyama-kipenzi

hariri

Chonga wamekuwa wanyama-kipenzi maarufu katika sehemu za Asia kwa sababu ya kuwa safi, rahisi kutunza na salama kushughulikia. Pia huko Asia, madume wa chonga hutumiwa kwa mapigano ya kamari. Kwa sababu madume kiasili wana tabia ya kupigana kwa uangalifu wa majike, ndio wao hutumika kwa mapigano. Ili kuwafanyia chonga wawili wa kiume wafungie mapigano, chonga wa kike hutumiwa au kifaa kidogo cha kipiga kelele kinachoiga mwito wa kupandisha wa jike.

Kama wasumbufu

hariri

Spishi nyingine zinaweza kuwa wasumbufu wakuu, k.m. katika migunda ya miti. Ingawa, kwa kawaida, idadi ya chonga sio kubwa kama wadudu wasumbufu wengine na miti ya chakula hupendelewa ambayo tayari ni migonjwa au inakufa kwa sababu nyingine. Mabuu ya spishi kadhaa, hata hivyo, yatashambulia miti yenye afya au hata mboga za mizizi, na yanapotokea kwa idadi kubwa yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa kiuchumi. Kuvu Metarhizium anisopliae ni wakala wa uthibiti wa kibiolojia uliohakikishwa wa uvamizi wa chonga katika mazao.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki

hariri