Christiaan Huygens
Christiaan Huygens (14 Aprili 1629 – 8 Julai 1695) alikuwa mtaalamu wa fizikia, hisabati na astronomia kutoka nchini Uholanzi aliyezaliwa mjini Den Haag.
Alizaliwa kama mtoto wa Constantijn Huygens aliyekuwa mshairi mashuhuri wa Uholanzi. Hivyo kupitia babake alipata kujua watu maarufu kama vile Rembrandt, Peter Paul Rubens na René Descartes. Alipokuwa mdogo alifundishwa na baba akaendelea kusoma sheria kwenye chuo kikuu cha Leiden baadaye akahamia masomo ya hisabati na sayansi.
Alikuwa kati ya watu wa kwanza waliofikiri ya kwamba nuru ina tabia ya wimbi. Kutokana na nadharia yake juu ya tabia za nuru aliweza kuboresha umbo la lenzi. Mwaka 1655 alitengeneza darubini iliyoboreshwa na kuchungulia sayari ya Zohali (Saturnus). Alitambua mwezi wa Titan na mwaka uliofuata aliweza kutangaza ya kwamba bangili za Zohali zinafanywa kwa miamba. Alibuni pia saa makini kushinda saa nyingine za wakati wake.
Chombo cha angani Cassini–Huygens kimepokea jina lake kwa heshima ya Huygens pamoja na Mwitalia Giovanni Domenico Cassini.