Wakati
Wakati ni neno la kutaja ama mfuatano wa matokeo au muda ama kipindi ambamo jambo linatokea.
Tunaishi katika wakati na tunapanga maisha yetu kufuatana na wakati, lakini si rahisi kusema wakati ni kitu gani. Sayansi, hasa fizikia, pia falsafa na dini, zote zina njia mbalimbali za kuangalia na kueleza wakati.
Wakati kama mpito
haririKatika maarifa ya kila siku wakati ni utaratibu wa mfululizo wa matokeo. Tunaweza kuona ya kwamba jambo liliwahi kutokea (wakati uliopita), linaendelea sasa (wakati wa kisasa) na tunatarajia litatokea tena (wakati ujao). Ndivyo tunavyotazama maisha yetu tukikumbuka mambo yaliyopita, tunasikia hali au mambo yanayoendelea na kutegemea kuona siku inayokuja.
Kwa sababu hiyo kuna usemi kama "wakati unapita" au "wakati unakimbia".
Wakati kisayansi
haririSayansi hutumia wakati kwa vipimo vingi hata kama haijui wakati wenyewe ni kitu gani. Imeunda vipimo vya wakati wenyewe vinavyowezesha kuelewa matokeo na kuyalinganisha.
Hapa sayansi inajaribu kuona wakati kama wanda (dimensioni) moja ya ulimwengu pamoja na zile tatu za nafasi ya ulimwengu. Hapa huitwa "wanda wa nne" (the fourth dimension).
Tofauti yake na nyanda za nafasi ni kwamba wakati una mwendo na mwelekeo.
Vipimo vya kawaida vya wakati
haririVipimo vya wakati hutumia matokeo yanayorudia mara kwa mara bila mabadiliko.
Kipimo cha kawaida ni siku au, kwa lugha nyingine, muda wa mzunguko mmoja wa dunia yetu unaoonekana kwetu kutokana na mabadiliko ya mchana na usiku.
Muda huo wa mzunguko mmoja hugawiwa katika saa 24 na kuitwa "siku". Saa hugawiwa katika dakika 60 na kila dakika kwa sekunde 60.
Mbio moja ya dunia yetu kuzunguka jua huitwa "mwaka". Utaratibu wa miaka hupangwa kwa njia ya kalenda.
Vipimo vya kisayansi
haririSayansi hairidhiki tena na vipimo hivyo vya kawaida. Mizunguko ya dunia au siku havilingani kikamilifu. Hapo sayansi imeondoka katika siku kama msingi wa vipimo vya wakati. Badala yake imechukua muda wa sekunde na kukiliganisha kwa mwendo wa atomi.
Katika vipimo sanifu vya kimataifa sekunde imewekwa kama muda wa radidi (periodi) 9,192,631,770 za mnururisho wa atomi ya caesi ya 133Cs.
Kisayansi Saa ndiyo chombo maalum ambacho hutumika kupima wakati hasa saa za kronografia (chronograph watches) - saa zijulikanazo kwa Kingereza kama "Stop-Watch" za kupimia muda mfupi wakati tukio kama shindano la riadha zinafanyika.
Vipindi vya wakati
hariri- milenia = miaka 1000
- karne = miaka 100
- mwaka = miezi 12 = siku 365.25
- mwezi ≈ wiki 4 ≈ siku 30
- wiki (juma)= siku 7
- siku = masaa 24
- saa = dakika 60
- dakika = 60 sekunde
- sekunde = 1000 millisekunde
- milisekunde = 1000 mikrosekunde
- mikrosekunde = 1000 nanosekunde
- nanosekunde= 1000 pikosekunde
- pikosekunde= 1/1,000,000,000,000 sekunde
Marejeo
haririViungo vya Nje
hariri- Google Map
- World Clock
- U.S. Naval Observatory Ilihifadhiwa 30 Agosti 2010 kwenye Wayback Machine.
- Hexadecimal Time Ilihifadhiwa 10 Agosti 2011 kwenye Wayback Machine.