Daniel Gabriel Fahrenheit

Daniel Gabriel Fahrenheit (24 Mei 1686 mjini Danzig (Ujerumani) - 16 Septemba 1736 mjini Den Haag (Uholanzi)) alikuwa mwanafizikia Mjerumani.

Nyumba alikozaliwa Fahrenheit mjini Danzig

Alipokuwa kijana alihamia mjini Amsterdam (Uholanzi). Alijifunza ufundi wa kioo akatengeneza vifaa vya vipimo vya kisayansi akaanza kujishughulisha mwenyewe na vipimo vya kitaalamu.

Alitambua hasa udhaifu wa vipimo vya joto na ugumu wa kulinganisha matokeo yake na vipimajoto vya siku zake. Hapa alibuni kipimajoto kilichokuwa kamili kuliko zote zilizotangulia na kuunda skeli ya kipimo.

Kwenye skeli ya Fahrenheit alitumia kiwango cha chini kilichopatikana katika mchanganyiko wa maji na chumvi kabla ya kuganda kilichokuwa sifuri kwenye skeli yake, halafu kiwango cha maji ya kawaida kuganda (kwake gredi 32) halafu kiwango cha joto mdomoni mwa mtu mwenye afya alichoita 96 gredi.

Skeli yake ilijulikana kama "Fahrenheit" ikatumiwa kimataifa hadi kupatikana kwa skeli ya Selsiasi au sentigredi. Skeli ya fahrenheit inatumiwa hadi leo katika Marekani.


Wikimedia Commons ina media kuhusu: