Kiesperanto
Kiesperanto ni lugha ya kupangwa inayozungumzwa zaidi duniani kati ya lugha hizi. Ilipangwa na Ludwik Lejzer Zamenhof, myahudi aliyetoka mjini Białystok, nchini Urusi (siku hizi ni sehemu ya nchi ya Poland). Alitoa kitabu cha kwanza cha lugha hii mwaka 1887 baada ya kuitengeneza kwa miaka karibu kumi. Nia yake ilikuwa kutengeneza lugha rahisi ili iwe lugha saidizi ya kimataifa, lugha ya pili kwa kila mtu duniani. Waesperanto wengine bado wanataka hiyo, lakini wengine wanapenda kuitumia tu bila nia ya kuieneza duniani kote.
Waesperanto wanakitumia Kiesperanto kwa ajili ya kukutana na wageni na kujifunza kuhusu nchi na tamaduni nyingine. Siku hizi, maelfu ya watu wanaitumia mara kwa mara ili kuwasiliana na watu popote duniani.
Chunguzi za kitaalamu zimeonyesha kwamba Kiesperanto kinaweza kujifunzwa rahisi zaidi sana kuliko lugha asilia, na pia kwamba kujifunza Kiesperanto kwanza kunarahisisha kujifunza kwa lugha nyingine.
Sifa za kiisimu
haririKwa kuwa lugha ya kupangwa, Kiesperanto hakiko katika familia yoyote a lugha. Maneno yake yanatoka hasa lugha za Kirumi (kama Kifaransa na Kilatini), lakini pia lugha za Kigermaniki (kama Kiingereza na Kijerumani) na lugha za Kislavoni (kama Kirusi na Kipolandi). Maneno mengi yanaumbwa kwa kuunganisha mzizi wa neno moja na viambishi au kwa kuunganisha mizizi ya maneno mbalimbali. Kwa mfano kuna kiambishi awali "mal-" inayoonyesha kinyume: "bona" ni "-zuri" na "malbona" ni "-baya". Kwa hiyo inawezekana kusema mambo mengi baada ya kujifunza maneno machache tu.
Matamshi na maandishi
haririKatika Kiesperanto kuna harufi 28 na kuna sauti 28. Kila harufi inaweza kutamka kwa sauti moja tu, na kila sauti inaandikwa kwa serufi moja tu. Harufi za Kiesperanto ni zifuatazo:
Irabu zote (a, e, i, o, u) zinatamka kama kwa Kiswahili.
Kwa upande wa konsonanti, b, d, f, g, h, k, l, m, n, p, r, s, t, v na z zinatamka kama kwa Kiswahili. c inatamka kama ts. ĉ inatamka kama ch. Matamshi ya ĝ yanafanana na matamshi ya j kwa Kiswahili (ni sawasawa na matamshi ya j katika neno la Kiswahili "njia"); j ya Kiesperanto inatamka kama y ya Kiswahili. ĵ inatamka kama j ya Kifaransa (inafanana na sh ya Kiswahili, lakini inatamka na sauti, kama z). ŝ inatamka kama sh. ŭ inatamka kama w; ŭ inatumika baada ya a na e tu, ingawa Zamenhof wenyewe na Waesperanto wengine waiunganisha na irabu yoyote, k.m. "sŭahila" (Kiswahili), "ŭato" (wati), tena jina la herufi yenyewe ni "ŭo"; tofauti kati ya au na aŭ ni kwamba au inatamka kwa silabi mbili na aŭ kwa silabi moja.
Serufi
haririNomino (majina) zote zinahitimu kwa kiambishi tawali -o, kwa mfano "arbo" (mti). Wingi wa nomino unahitimu kwa -oj (arboj = miti).
Vivumishi vinahitimu kwa kiambishi tawali -a, kwa mfano "alta" (-refu). Vivumishi kwa kawaida vinawekwa kabla ya nomino inayohusu, lakini pia inaweza kuwa baada yake. Wingi pia unaonyeshwa katika vivumishi kwa harufi "j": altaj arboj = miti mirefu.
Vitenzi vina viambishi tamati mbalimbali:
- -i inatumika kwa vitenzi-jina (kwa mfano "fari" = "kufanya")
- -as inatumika kwa njeo ya wakati uliopo (kwa mfano "mi faras" = "ninafanya"
- -is inatumika kwa njeo ya wakati uliopita (kwa mfano "mi faris" = "nilifanya" au "nimefanya")
- -os inatumika kwa njeo ya wakati ujao (kwa mfano "mi faros" = "nitafanya")
- -us inatumika kwa hali a masharti (kwa mfano "mi farus" = "ningefanya")
- -u inatumika kwa hali ya kuamuru (kwa mfano "faru!" = "fanya!"; "li faru" = "afanye")
Viungo vya nje
hariri- makala za OLAC kuhusu Kiesperanto Ilihifadhiwa 25 Aprili 2015 kwenye Wayback Machine.
- lugha ya Kiesperanto katika Glottolog
- http://www.ethnologue.com/language/epo
- Maelezo mengine kuhusu Kiesperanto Ilihifadhiwa 17 Februari 2006 kwenye Wayback Machine.
- Jifunze Kiesperanto Ilihifadhiwa 5 Februari 2007 kwenye Wayback Machine.
- Tangazo la Praha la jamii ya kiesperanto Ilihifadhiwa 5 Aprili 2007 kwenye Wayback Machine.
- TANGAZO LA PRAHA LA JAMII YA KIESPERANTO (Word-doc.) Ilihifadhiwa 15 Machi 2012 kwenye Wayback Machine.
- esperanto-afriko.org
- Jifunze lugha ya Kiesperanto, 2007, Ilihifadhiwa 13 Septemba 2011 kwenye Wayback Machine.
- Kozi ya kimataifa Kurso Saluton!
- Lernu!