Günter Grass

(Elekezwa kutoka Gunter Grass)

Günter Wilhelm Grass (alizaliwa 16 Oktoba 1927 Danzig, alifariki 13 Aprili 2015 mjini Lübeck) alikuwa mchoraji, mchongaji na mwandishi kutoka nchi ya Ujerumani. Hasa ameandika riwaya na insha, na pia tamthiliya na mashairi. Mwaka wa 1999 alikuwa mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi.

Günter Grass (2004)
Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Utoto na ujana

hariri

Grass alizaliwa katika dola-mji Danzig (leo Gdansk, Poland) akiwa mwana wa mfanyabiashara Mjerumani na mke wa asili ya Kashubi. Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alijitolea kuwa mwanajeshi Mjerumani akiwa na umri wa miaka 15 na kwa umri wa miaka 17 alikuwa mwanajeshi wa kiosi cha SS.

Baada ya vita alijifunza uchongaji na kuongeza masomo ya fani hii pamoja na nakshi kwenye vyuo vya Düsseldorf na Berlin.

Maisha ya binafsi

hariri

1954 alifunga ndoa na Mswisi Anna Schwarz akaishi naye Paris, Ufaransa kati ya 1956 hadi 1960. Alizaa naye watoto wanne wakaachana 1972 na kuwa na talaka ya mwaka 1978. Baada ya kuaachana na Anna akawa na uhusiano wa kimapenzi na Veronika Schröter halafu Ingrid Kruger akazaa watoto nao pia. 1979 alimwoa Ute Grunert akakaa naye hadi mwisho. Wakati wa kifo chake alikuwa na wajukuu 18. [1]

Grass alikuwa mshabiki wa klabu ya soka ya Bundesliga SC Freiburg. [2]

Alikuwa mwanachama wa chama cha SPD (chama cha kijamii cha Ujerumani,Social Democratic Party).

Mafanikio kama mwandishi

hariri

Wakati wa kukaa Paris alitunga muswada wa riwaya yake ya kwanza "Die Blechtrommel" (ngoma ya bati) iliyompatia umaarufu mara ya kwanza katika Ujerumani. Katika riwaya hii sawa na vitabu vyake vilivyofuata alisimulia habari za Wajerumani wakati wa vita na chini ya utawala wa chama cha Nazi cha Adolf Hitler. Alijadili hapa swali la hatia ya Wajerumani kwa jinai zilizotendewa chini ya mfumo wa siasa ya miaka ya Hitler.

Riwaya za "Katz und Maus" (Paka na panya) na "Hundejahre" (miaka ya mbwa) zilifuata 1961 na 1963. Zote tatu zinasimulia maisha ya watu kutoka mji wake Danzig ambayo tangu 1945 imekuwa mji wa Poland ilhali wakazi wote Wajerumani walifukuzwa. Maandiko ya Grass yalisababisha majadiliano makali katika jamii ya Ujerumani juu ya historia ya taifa na swali la hatia ya kuvumilia na kushiriki katika mfumo wa kisiasa ya miaka ya Hitler.

Alipokabidhiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 1999 taasisi ya taaluma ya Sweden ilieleza: "Katika 'Ngoma ya Bati' Grass alichunguza historia ya kisasa kwa kukumbuka wale waliosahauliwa, wahanga na ule uwongo ambao watu wanataka kusahau kwa sababu waliwahi kuuamini".

Marejeo

hariri
  1. http://www.bloomberg.com/news/articles/2015-04-13/guenter-grass-german-writer-who-took-on-nazi-past-dies-at-87
  2. http://www.rp-online.de/politik/nobelpreistraeger-drueckt-dem-sc-freiburg-die-daumen-aid-1.2263002
  Makala hii kuhusu mwandishi fulani wa Ulaya bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Günter Grass kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.