Haubi
Haubi ni kata ya Wilaya ya Kondoa katika Mkoa wa Dodoma, Tanzania, yenye postikodi namba 41718[1].
Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi walihesabiwa 14,679 [2]. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 13,757 [3] waishio humo.
Baadhi ya vijiji vya kata ya Haubi vyenye shule ya msingi ni Kidulo, Soro, Mkonga, Kuuta, Mwisanga na Ntomoko. Asilimia kubwa za wakazi wa kata ni Warangi na Haubi . inajulikana kama shina la Warangi.
Wakazi wengi wa kata hiyo wanafuata dini ya Uislamu na Ukristo kadiri ya madhehebu ya Kanisa Katoliki.
Kata ya Haubi iko milimani mnamo futi 6000 juu ya usawa wa bahari. Jina lake limetokana na ziwa Haubi ambalo ni ziwa kubwa kiasi, kwa lugha ya Kirangi ni ihau.
Kwa jina jingine Haubi huitwa "Mʉʉmbʉ ya Mʉrɨɨndo" yaani sehemu ambapo kibuyu kilibaki. Jina hilo lilianza kutumika baada ya Muru aliyekuwa mganga wa jadi wa Warangi kufunga mvua kwa muda wa miaka saba (alifanya hivi kama adhabu kwa vile mpwa wake aliuawa na watu). Alipokwenda kwa waganga walimwambia kwamba maiti ya mtoto huyu imekuwa ikitumika kama kitu cha kulenga, "Kɨɨntʉ choo kwiiyerera".
Muru alipokwenda na kuona jinsi maiti ya mpwa wake ilivyokuwa ikitumika aliamua kutoa adhabu kwa watu wa Haubi kutokana na kosa walilofanya. Hivyo alimwambia dada yake ambaye ndiye alikuwa mama wa mtoto aliyeuawa kuwa ajitahidi kuhifadhi chakula kwani anataka kuwaadhibu watu wa Haubi. Hivyo walihifadhi chakula kwa miaka minne. Baada ya kuona chakula kinatosheleza alifunga mvua. Na kabla ya kufanya hivyo alichimbia vibuyu vilivyoitwa "Mʉʉmbʉ", ambavyo alivitia maji. Baada ya hapo aliondoka, na kwa kweli mvua haikunyesha hata kidogo kwa muda wa miaka saba. Katika kipindi hiki watu wengi walikufa njaa.
Kipindi hiki ndicho kilikuwa mwanzo hasa wa koo za Warangi, kwani wapo waliopona njaa kwa kufuata simba ambeye alikuwa huua wanyama na mabaki ya nyama hizo walichukua na kula mpaka wakapona njaa. Ukoo huu uliitwa "Veene Jiimba" yaani Wamiliki wa Simba au Ukoo wa Simba. Wapo waliopona kwa kunywa maziwa ya ngombe, hawa waliitwa "vawoomba ngʼoombe". Wapo waliokula aina ya mtama unaoitwa "Mʉsoongo" mpaka wakapona njaa. Hawa wanaitwa, "Vasoongo".
Baada ya Muru kurudi alifika kidundi kwa mzee Parapata, na watu walipomwona walimwosha kwenye lambo kwa kutumia pumba. Siku hiyo hiyo mvua ilinyesha sana. Na kwa sababu watu hawakuwa na mbegu iliyokuwa imebaki mtama uliota mashambani mwao. Ndiyo maana hata leo wapo watu wanaoitwa akina "mavere" (yaani mtama kwa lugha ya Kirangi). Jina hili lilitokana na mtama ulioota kipindi hicho.
Baada ya siku chache Muru alitembelea vibuyu vyake na kugundua kwamba sehemu nyingine zote, yaani, katika vijiji vya Kinyasi, Baura, Pahi, Kolo vibuyu vilikauka maji na kuliwa na mchwa ila Haubi vibuyu vyote vilibaki na vilikuwa na maji. Hivyo akasema hii ni "Mʉʉmbʉ ya Mʉrɨɨndo", maana yake kibuyu kilibaki.
Haubi pia ina maeneo mengi ya kuvutia kama sehemu za "Irumawii". Yaani sehemu ambapo mawe huvuma. Sehemu hii huaminika kwamba hukaliwa na mizimu, ambao huwalinda Warangi na huwapatia Warangi baraka zote.
Marejeo
hariri- ↑ "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2020-03-21. Iliwekwa mnamo 2017-10-08.
- ↑ https://www.nbs.go.tz
- ↑ "Sensa ya 2012, Dodoma - Kondoa DC" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2004-01-02. Iliwekwa mnamo 2016-05-18.
Kata za Wilaya ya Kondoa - Mkoa wa Dodoma - Tanzania | ||
---|---|---|
Bereko * Bumbuta * Busi * Changaa * Haubi * Hondomairo * Itaswi * Itololo * Kalamba * Keikei * Kikilo * Kikore * Kinyasi * Kisese * Kwadelo * Masange * Mnenia * Pahi * Salanka * Soera * Thawi |
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Dodoma bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Haubi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno. |