Kifinisia
Kifinisia ilikuwa lugha ya Kisemiti iliyozungumzwa kati ya 1100 KK hadi takriban 600 BK katika maeneo ya pwani la Kanaani na Shamu ya magharibi ambako leo hii kuna nchi za Israeli, Lebanoni na Syria.
Ilikuwa lugha ya Wafinisia ikaenea pamoja nao katika koloni zao hadi Afrika ya Kaskazini kama Karthago na Hispania.
Kifinisia ilikuwa lugha ya kwanza iliyoandikwa kwa aina ya alfabeti iliyoendelezwa baadaye katika alfabeti ya Kigiriki. Hali halisi mwandiko huu ulikuwa abjadi ukawa mama wa miandiko yote ya Kisemiti (kama herufi za Kiarabu na Kiebrania) na pia wa alfabeti zote zilizofuata alfabeti za Kigiriki na Kilatini.