Alfabeti ya Kilatini

Alfabeti ya Kilatini (pia: Alfabeti ya Kirumi) ndiyo alfabeti inayotumiwa kwa lugha nyingi zaidi duniani. Hata Kiswahili siku hizi huandikwa kwa herufi za Kilatini kama kwa mfano kwenye ukurasa huu wa Wikipedia.

Nchi zinazotumia alfabeti ya Kilatini kwa lugha zao
Kijani nyeupe: Nchi zinazotumia herufi za Kilatini pamoja na alfabeti za kienyeji

Mwanzo wa alfabeti ya Kilatini

hariri

Asili ni namna ya kuandikwa kwa lugha ya Kilatini iliyokuwa lugha ya Roma ya Kale. Baadaye ilitumiwa kuandika hata lugha za Kirumi, Kigermanik, Kislavoni, Kituruki, lugha za Afrika na Kiasia.

Waroma walipokea alfabeti yao kutoka alfabeti ya Kigiriki lakini waliibadilisha hasa kwa kuacha kando herufi za kutaja sauti ambazo hazikuwa na maana katika Kilatini.

Alfabeti ya kwanza ya Kilatini ilikuwa na herufi 21 pekee:

A B C D E F Z H I K L M N O P Q R S T V X

Baada ya kuvamia Ugiriki Waroma wa Kale walianza kutumia maneno mengi ya Kigiriki katika lugha yao, hivyo wakaingiza herufi mbili za ziada kutoka Kigiriki kwa ajili maneno hayo mapya, yaani Y na Z.

Namna ya kuandika

hariri

Waroma wa Kale waliandika herufi kubwa tu. Tena hawakuacha nafasi kati ya maneno, hivyo maandiko yao si rahisi ya kusoma:

Mfano wa maandishi ya Kiroma:

AVREAPRIMASATAESTAETASQVAEVINDICENVLLO
SPONTESVASINELEGEFIDEMRECTVMQVECOLEBAT

Siku hizi inaandikwa hivyo:

Aurea prima sata est aetas, quae vindice nullo,
sponte sua, sine lege fidem rectumque colebat.

Nyongeza za baadaye

hariri

Baada ya mwisho wa Dola la Roma ni hasa mataifa ya Ulaya yaliyotumia alfabeti ya Kilatini. Wakati wa karne za kati herufi zifuatazo ziliongezwa kufuatana na mahitaji ya lugha za Wazungu:

  • herufi za I na V zilikuwa zikimaanisha konsonanti na pia vokali. Hapo herufi mpya za "J" na "U" ziliingizwa.
  • herufi ya W ilitokea baada ya kuandika VV mwanzoni

Hivyo alfabeti inayojulikana leo hii kama ya "Kilatini" imekuwa kama ifuatavyo:

A, B, C, D, E, F, G, H, I, J, K, L, M, N, O, P, Q, R, S, T, U, V, W, X, Y, Z.
a, b, c, d, e, f, g, h, i, j, k, l, m, n, o, p, q, r, s, t, u, v, w, x, y, z.

Herufi za nyongeza katika lugha mbalimbali

hariri

Kwa mahitaji ya lugha mbalimbali kuna nyongeza nyingi katika alfabeti ya Kilatini (mifano):

herufi za ä, ö, ü zinatumiwa katika Kijerumani, Kituruki na Kifini
herufi kama ã au ñ (Kireno)
herufi kama ž, č, š (lugha za Kislavoni)
herufi kama ng' (Kiswahili)

Hii ni mifano michache tu.

Uenezi wa alfabeti ya Kilatini

hariri

Uwezo wa kupokea alama mpya ni sababu ya uenezi wa alfabeti ya Kilatini. Kuna lugha mbalimbali zilizowahi kuandikwa kwa alfabeti tofauti lakini baadaye zilipokea ile ya Kilatini. Hata kama sababu muhimu ilikuwa utawala wa kikoloni katika sehemu nyingi za dunia kuna pia faida zilizosababisha kuendelea na alfabeti ya Kilatini hata baada ya nchi kupata uhuru.

Mfano ni lugha kama Kiswahili na Kituruki zilizowahi kuandikwa kwa mwandiko wa Kiarabu.

Kiswahili kilianza kuandikwa na Wazungu kama Ludwig Krapf kwa herufi za Kilatini katika karne ya 19. Katika karne ya 20 Waingereza walisanifisha lugha kwa kutumia alfabeti ya Kilatini. Faida yake ni ya kwamba sauti nyingi zinatajwa vizuri zaidi kuliko kwa Kiarabu.

Kituruki kilianza kutumia herufi za Kilatini baada ya mapinduzi ya Atatürk.

Hata Uchina kuna mwelekeo huu.