Kigermanik
Lugha za Kigermanik ni kikundi cha lugha zenye asili ya Ulaya ya Kaskazini.
Lugha za Kigermanik zenye wasemaji wengi ni Kiingereza (milioni 380) na Kijerumani (milioni 120). Lugha nyingine za Kigermanik ni lugha za Skandinavia, halafu Kiholanzi na Kiafrikaans wa Afrika Kusini.
Historia hariri
Mwanzo wa lugha hizi uko gizani. Wataalamu wamejaribu kutambua sifa za lugha asilia kwa kulinganisha lugha mbalimbalimbali zilizo karibukaribu ikiwa habari zao zimejulikana.
Kutokana na makisio hayo Kigermanik kilianza Ulaya ya Kaskazini, labda Sweden ya Kusini katika miaka elfu ya kwanza K.K..
Wasemaji wa Kigermanik walianza kuhamahama wakati wa Dola la Roma na ndipo habari za kwanza za kihistoria zimepatikana.
Matembezi ya Wagermanik yalifika hadi Urusi wa Kusini na Afrika ya Kaskazini.
Lugha za Kigermanik hugawanywa katika aina tatu:
a) Kigermanik ya Kaskazini: Kiswidi, Kidenmark, Kinorwei, Kiiceland na Kifaroe
b) Kigermanik ya Magharibi: Kiingereza, Kijerumani (Kidachi), Kiholanzi, Kiafrikaans, Kijerumani ya Kaskazini, Kifrisia, Kiyiddish (Kiyahudi cha Ulaya)
c) Kigermanik ya Mashariki: lugha hizi kama Kivandali au Kigoti zimekufa zote zinajulikana kama lugha za kihistoria tu