Galaksi

(Elekezwa kutoka Magalaksi)

Galaksi (ing. galaxy) ni kundi la nyota nyingi zinazoshikamana pamoja katika anga ya ulimwengu kutokana na graviti yao. Nyota hupatikana angani katika makundi kama mawingu makubwa sana.

Galaksi ya Andromeda yenye na. M 31 na galaksi mbili ndogo za kando M 32 na M 110

Kuna galaksi nyingi sana ulimwenguni. Kwa wastani kila galaksi imekadiriwa kuwa na nyota kama bilioni 100 lakini kuna galaksi kubwa na ndogo.

Galaksi yetu, ikiwemo mfumo wetu wa jua, imekadiriwa kuwa na nyota zaidi ya bilioni 300 (3·1011). Sehemu ya nyota hizi zinaonekana kama kanda la kung'aa kwenye anga la usiku linalojulikana kwa rangi yake kama njia nyeupe au "njia ya maziwa"[1]. Umbo lake linafanana na kisahani kikiwa na kipenyo cha miakanuru 100,000 na kikiwa na unene wa miakanuru 3,000.

Kwenye kitovu cha galaksi graviti ni kubwa sana kiasa cha kwamba galaksi nyingi huaminiwa kuwa na shimo jeusi kituvoni[2].

Galaksi zilizo karibu angani zinaitwa Mawingu ya Magellan ambayo ni galaksi mbili ndogo zilizopo kwenye umbali wa miakanuru 170,000 na 200,000. Galaksi kubwa ya jirani ni Andromeda na ina umbali wa miakanuru milioni 2.5.

Idadi kamili ya galaksi zote angani haijulikani. Kuna makadirio ya kwamba idadi ya galaksi zinazoweza kuangaliwa kwa vyombo vinavyopatikana ni mabilioni. Hadi sasa sehemu ndogo tu imehesabiwa lakini mara kwa mara galaksi mpya zinatambuliwa kwa njia ya darubini au vyombo vya angani.

Galaksi zinazojulikana zimepewa namba katika orodha ya kimataifa na wanasayansi wa astronomia.

Galaksi kati yao hujumuika pia zikiathiriana kwa njia ya graviti yao na kuzunguka kitovu cha graviti cha pamoja. Galaksi hadi 50 zinazoshikamana katika kipenyo cha miakanuru milioni 10 huitwa kundi la galaksi (ing. galaxy group). Kuna pia galaksi mamia hadi maelfu kadhaa zinazoshikamana na hii huitwa fundo la galaksi (ing. galaxy cluster) linaweza kuwa na kipenyo cha miakanuru milioni 10 - 20.

Marejeo

  1. Maziwa (mfano maziwa ya ng'ombe) kwa Kigiriki huitwa "γάλα gala" na hapo asili ya jina "galaksi".
  2. Astronomers Get Closest Look Yet At Milky Way's Mysterious Core, tovuti ya National Radio Astronomy Observatory, Marekani, iliangaliwa Machi 2019