Mbege ni kileo asili cha Wachagga, wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro.

Mgomba (Ndizi) unaotumika kutengeneza mbege

Mbege hutengenezwa kwa ndizi mbivu, kimea cha ulezi, na maji.

Mara nyingi mbege hutengenezwa na wanawake na hutumika katika sherehe na matukio mbalimbali kama vile harusi, misiba, kipaimara, kuzaliwa kwa mtoto, n.k. Mbege hutumiwa pia kama faini kwenye mahakama za jadi. Utengenezaji wa mbege hufanywa pia kwa biashara. Hapo huuzwa katika vilabu vya pombe na pia nyumbani.

Utengenezaji na unywaji Edit

Kinywaji hicho hutengenezwa kwa kuchemsha ndizi mbivu kama vile ndizi songea, ndizi uganda, kibungara, kisukari (kama zinapatikana sana) n.k. Ndizi hizo zikishachemshwa huachwa kwa kipindi cha kama tatu au zaidi ili zichache.

Baada ya hapo unga wa ulezi hupikwa na kuachwa upoe. Ndizi zilizochemshwa na kuchacha huchanganywa na maji, kisha kukamuliwa ili kupata juisi yake. Juisi hiyo huchanganywa na unga wa ulezi uliopikwa na tunapata (kivuo, kifue, togwa) na kuachwa usiku mzima. Kesho yake mbege huwa tayari kunywewa.

Kinywaji hicho kama haitanyewa na kumalizika siku hiyo basi ikilala tunapata kitu kinachooitwa ngera, ambayo ni chachu sana, ila ngera pia huweza kuzimuliwa na kuwa kinywaji kifaacho tena kwa kuchanganya na unga uliopikwa na unga kidogo usiopikwa, ila ngera ikilala tena humwagwa kwani haitafaa kunywea tena.

Watengenezaji wengi wa mbege huwa wanaweka gamba la mti wa msesewe (Rauvolfia Caffra), hasa maeneo ya Kibosho, Machame na Rombo ili kuongeza ladha ya uchachu na kupunguza kasi ya mbege kuchacha.

Chombo maalum kiitwacho kata hutumiwa kunywea mbege, ila mara nyingi sehemu za mijini hutumia vyombo vya plastiki, vikiwa na ujazo tofauti, navyo huitwa chubuku na kitochi. Katika maeneo ya vijijini mbege hunywewa kijamaa kwa kupokezana kata. Mtu mmoja anakunywa kisha anampatia mwingine anayekunywa na kumpa mwingine.

  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mbege kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.