Wikipedia:Mwongozo (Viungo vya Wikipedia)

(Elekezwa kutoka Msaada:Viungo)
Utangulizi   Kuhariri   Kuanzisha Makala   Muundo   Viungo vya Wikipedia   Kutaja vyanzo   Kurasa za majadiliano   Kumbuka   Kujisajili    

Kuunga pamoja viungo vya makala za Wikipedia ni kazi nyepesi lakini muhimu sana. Inaruhusu watumiaji kupata habari nyingi zinazohusiana na makala wanayosoma. Inaongeza manufaa ya Wikipedia kwa wasomaji.

Mfano

Viungo vya buluu

Makala juu ya mji wa Misri inaweza kuonekana hivyo:

Giza (Kar.: الجيزة al-gīza) ni mji wa kaskazini mwa Misri unaopakana na mji mkuu Kairo. Inajulikana hasa kama mahali pa piramidi.

Maneno yenye rangi ya buluu yanaunga makala hii na makala nyingine kuhusu Kar. = Kiarabu, Misri, Kairo na piramidi. Ukibofya neno la buluu unapelekwa kwenye makala hizo.

Viungo vyekundu

Kuna pia viungo vyenye rangi nyekundu:

Mabata-bahari ni ndege wa maji wa familia ndogo ya Merginae katika familia ya Anatidae.

Katika sentensi hii makala za ndege, Merginae na Anatidae ziko tayari lakini "familia ndogo" haikuandikwa bado. Wakati wa kuandika makala unaweza kuanzisha viungo vyekundu ukiona hapa ni neno muhimu inayostahili makala yake.

Hapa unatakiwa kuwa mwangalifu

  • usiweke maneno hovyo katika mabano mraba na kuanzisha kiungo chekundu maana maneno yaleyale katika mabano yanatakiwa kuwa jina la makala mpya.
  • fanya utafiti kama mada iko tayari labda kwa tahajia tofauti; kwa mfano umetafuta nchi ya "Aljiria", kumbe: "Algeria" iko tayari!

Jinsi ya kuunga

Mabano mraba [[ ]]

Ili kuunganisha ukurasa mmoja na mwingine wa Wikipedia (inaitwa kiungo cha wiki), weka katika mabano mraba mawili, kama hivi:

Mfano: [[Televisheni]] = Televisheni.

Njia nyingine kwa kutumia puku ni kuangaza maneno husika na kubofya alama ya kwenye menyu ya dirisha la uhariri.

Kigawanyishi-kibomba "|" kwa umbo tofauti la neno

Mara kwa mara jina la makala inayoelekezwa ni tofauti kidogo na maneno katika makala unayoshughulikia kama tofauti umoja/uwingi.

Mfano: "Serengeti kuna viboko wengi...". Unataka kuweka kiungo kwenda makala ya mnyama "kiboko".

Hapa unaweza kugawa mabano mraba kwa kutumia alama ya kigawanyishi-kibomba "|" (SHIFT + BACKSLASH kwenye baobonye zenye ABC za Kiingereza). Sasa kuna sehemu mbili ndani ya mabano mraba. Nafasi ya kwanza unaandika jina la makala inayoelekezwa na nafasi ya pili nyuma ya kigawanyishi unaandika maneno jinsi yanavyofaa katika sentensi yako.

Mfano: [[Kurasa uliyoilenga|maandishi yanayoonekana]] = maandishi yanayoonekana

Pia unaweza kutengeneza kiungo kuelekea sehemu mahususi ya makala kama kuna vichwa vya ndani ya makala:

[[Makala unapolenga#Sehemu ya makala yenye kichwa kidogo|maandishi yanayoonekana]] = maandishi yanayoonekana

Kiungo kuonekana kama italiki au koze

Iwapo unataka "maandishi yanayoonekana" ya kiungo kuonekana kama "italiki" (yaani herufi mlazo), weka apostrofi mbili kabla na baada ya mabano mraba kama hivi:

''[[Mapinduzi ya Viwandani]]'' = Mapinduzi ya Viwandani

(ukizoea utaangaza sehemu ya mabano mraba na kubofya alama ya " I " kwenye menyu ya kuhariri. Vilevile kwa kiungo kuonekana kama koze).

Kuhakikisha viungo ni sahihi

Hapa tunatumia dirisha la "tafuta" upande wa kushoto. Tukitaka kujua kama kuna chochote tayari kuhusu "Pemba" tunaandika neno hili dirishani. Halafu tunabofya "tafuta" tutapata orodha ya makala 119 yote yaliyo na neno "Pemba" ama katika jina au katika maandishi ya makala, kama vile Pemba (kisiwa), Mkoa wa Pemba Kusini, Mkoa wa Pemba Kaskazini, kata zote za Pemba, makala za kihistoria zinazogusa Pemba na mengine. Kwa kuchungulia usigonge "makala" chini ya dirisha maana hii itakupa makala 1 tu ama ya Pemba (maana) au ya mahali 1 tu. Kwa njia hii unaweza kuunganisha na makala yaliyopo tayari ukitumia jina na umbo sahihi.

Tafadhali tazama viungo vyako ili kuhakikisha kwamba zimeelekezwa katika makala sahihi. Kwa mfano, Gibraltar imelengwa katika makala inayohusu eneo dogo la Kiingereza ndani ya Hispania, wakati Mlango wa Gibraltar ni jina la makala inayohusu mlango wa bahari kati ya Ulaya na Afrika karibu na Gibraltar.

Pia kuna kurasa za kutofautisha "maana" -- hizi siyo makala, bali kurasa zenye viungo vya makala zenye majina ya karibu. Tazama Msaada:Maana kwa kuanzisha makala hizi.

Makosa ya mara kwa mara

Makosa yanatokea kwa urahisi usipoangalia vema yote ndani ya mabano mraba. Usiweke mabano ya kiungo bila kutafakari. Usimwage matokeo ya google translate bila kuchungulia kwanza!

Kwa mfano kuingiza alama za . au , ndani ya kiungo inabadilisha marejeo na kuharibu kiungo. [[Afrika,]] haiwezi kuunganisha na Afrika kwa sababu ya koma ndani ya mabano.

Lingine ni kutumia umbo la neno lisilo kawaida kwa mfano wingi badala ya umoja au kinyume. Hapa ni sharti kuchungulia kupitia dirisha la tafuta au jamii: je, umbo la kawaida hapa ni nini? Vilevile tahajia isiyo kawaida.

Jaribu kutafuta majina ya kikamusi; usiweke kiungo kwa "biashara haribifu ya watumwa". Jina la kikamusi ni "biashara ya watumwa".

Viungo vya picha

Picha au michoro huonekana katika makala kwa njia ya viungo. Kwa maelezo zaidi soma Msaada:Picha

Wakati wa kuunga

Kuongeza viungo kwenye makala kunaleta maana zaidi, lakini viungo vingi mno huleta vurugu. Utaratibu ni huu: fanya neno fulani mara moja tu kuwa kiungo katika makala moja, usirudie neno hili kama kiungo. Unapaswa kuchagua mara ya kwanza ambako neno hilo linatokea kwenye makala.

Kuchungulia kwenye viungo vingine vya makala za Wikipedia pia inaweza kukusaidia kujifunza wakati wa kuweka viungo. Tazama ukurasa wa makala nzuri kwa orodha ya makala zenye ubora mkubwa.

Jamii au Category

Kila makala inatakiwa kuungwa katika jamii na makala nyingine zinazojadili mada za karibu.

Andika [[Jamii:]], na weka jina la jamii nyuma ya "nukta pacha" baina ya mabano ya miraba miwili.

Ni muhimu sana kuweka jamii sahihi, kwa kuwa hivyo itakuwa rahisi kwa watu wengine kupata kazi yako. Njia iliyo bora ya kutafuta jamii gani inayotakiwa iwekwe kwenye makala ni kuchungulia kurasa zenye kuelezea suala moja, na tazama jamii gani walizotumia.

Mfano: Unaandika makala kuhusu mnyama fulani. Chungulia kwa kuandika "jamii:wanyama" katika dirisha la "tafuta" na angalia vijamii vidogo vilivyopo tayari na makala zilizo ndani ya vijamii hivi.
Kwa habari zaidi, rejea katika ukurasa wa Jamii.

Interwiki

Bofya hapa kuona picha vizuri zaidi

Interwiki ni orodha ya viungo vya mada fulani na makala za kufanana katika Wikipedia za lugha mbalimbali. Katika ukurasa unaosoma sasa hivi orodha ipo upande wa kushoto nje ya makala chini ya kichwa "Lugha nyingine". Hapo unaona majina kama Alemannisch, العربية, Català, Česky, English na kadhalika. Zote ni za rangi ya buluu maana ni viungo vya kwenda kurasa za "Mwongozo wa Wikipedia" kwa lugha hizo.

Ukianzisha makala mpya na kuihifadhi utaona hakuna majina ya lugha ya buluu bado. Ukibofya pembeni "Add links" utaona dirisha dogo. Humo unaandika juu "enwiki" na kuthibitisha, chini yake unaandika jina la makala husika katika Wikipedia ya Kiingereza. Thibitisha tena mara mbili na sasa makala yako ya Kiswahili imeunganishwa na namba ya mada yake katika orodha "Wikidata" inayoorodhesha makala za Wikipedia zote. Sasa itaonyesha lugha nyingine kwa rangi ya buluu na makala yetu ya Kiswahili inaonekana pia kwa wasomaji wa lugha hizo nyingine. Huu ni msaada mkubwa kwa wahariri wanaoweza kusoma lugha mbalimbali na kuongeza habari kutoka huko.

Ukikuta kiungo cha Interwiki kisicho sahihi (mtumiaji aliyetangulia alikosa kuteua namba sahihi) unaweza kubofya "Hariri viungo". Sasa unafika katika ukurasa wa Wikidata, angalia sanduku ya "Wikipedia", bofya "edit" halafu alama ya ndoo ya takataka ili kufuta neno la Kiswahili. Sasa bofya "publish" na kufunga Wikidata. Ukiita sasa makala yako utaona haionyeshi interwiki tena (inaweza kuchukua dakika kadhaa hadi mabadiliko yanaonekana). Sasa unaweza kuanza upya kuweka interwiki sahihi.

Hatua hizo utatekeleza katika mtazamo wa dawati (Desktop view) inayopatikana kwa kubofya maandishi madogo "dawati" kwenye dirisha la simu yako, chini kabisa.

Jaribu ulichojifunza katika sanduku la mchanga

Endelea mwongozo na Kutaja vyanzo