Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli
Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli ndio wa pili katika orodha ya mitaguso ya kiekumene ya Kanisa wakati wa mababu wake. Uliitishwa na kaisari Theodosius I ukafanyika Konstantinopoli mwaka 381.
Maaskofu 150 waliohudhuria walilaani aina mbalimbali za uzushi, hasa ule wa Masedoni wa Konstantinopoli aliyekanusha umungu wa Roho Mtakatifu, wakathibitisha maamuzi ya mtaguso mkuu wa kwanza (Mtaguso wa kwanza wa Nisea), uliofanyika mwaka 325.
Hivyo walikiri kwamba Roho Mtakatifu pia, kama vile Yesu Mwana wa Mungu, anachanga dhati ileile ya Baba.
Pamoja na hayo, walikamilisha kanuni ya imani ya Nisea ambayo kwa sababu hiyo inaitwa sasa kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli na ambayo inatumika sana hata leo katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo, hasa katika liturujia.